Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wathesalonike 3:1-18

2 Wathesalonike 3:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanauamini ujumbe huu. Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu. Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni. Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo. Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa. Nyinyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu. Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, “Mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula.” Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe. Lakini nyinyi ndugu, msichoke kutenda mema. Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye, kusudi aone aibu. Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu. Bwana mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote. Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika. Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

2 Wathesalonike 3:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa kote kama ilivyo kwenu; na tukaokolewe kutoka kwa watu wasio haki, na waovu, maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda kutoka kwa yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza na kwamba mtaendelea kuyafanya. Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na subira ya Kristo. Ndugu, tunawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu kutoka kwa kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu. Mnajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu yeyote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulifanya kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. Si kwamba hatuna haki hiyo, ila kwa makusudi ya kuwapa mfano wa kuiga, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana tunasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi tunawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, wafanye kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema. Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la barua hii, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari; lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu. Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote. Salamu zangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila barua yangu, ndio mwandiko wangu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote.

2 Wathesalonike 3:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya. Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo. Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu. Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema. Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la waraka huu, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari; lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu. Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote. Salamu zangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila waraka, ndio mwandiko wangu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote.

2 Wathesalonike 3:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu. Ombeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini. Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu. Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza. Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo. Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa. Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi, wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu. Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe mfano wenu wa kufuata. Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.” Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi, bali hujishughulisha na mambo ya wengine. Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe. Lakini kwenu ninyi, ndugu, kamwe msichoke katika kutenda mema. Ikiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyo katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu. Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu. Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote. Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amen.