2 Wathesalonike 1:1-10
2 Wathesalonike 1:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana. Ndio maana sisi tunajivunia nyinyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata. Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake, nyinyi mtastahili ufalme wake ambao kwa ajili yake mnateseka. Mungu atafanya jambo la haki: Atawalipa mateso wale wanaowatesa nyinyi na kuwapeni nafuu nyinyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake wenye nguvu na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu. Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu, wakati atakapokuja siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Nyinyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.
2 Wathesalonike 1:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, Silwano na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi. Hata na sisi wenyewe tunaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya subira yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili. Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa. Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi; na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake, katika muali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake; yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu).
2 Wathesalonike 1:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi. Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili. Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa. Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi; na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake; yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu).
2 Wathesalonike 1:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Paulo, Silvano na Timotheo. Kwa kanisa la Wathesalonike mlio katika Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi. Ndugu, inatupasa kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, na inastahili hivyo kwa sababu imani yenu inazidi kukua sana, nao upendo wa kila mmoja wenu kwa mwenzake unazidi kuongezeka. Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivunia saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili. Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili yake. Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi, na kuwapa ninyi mnaoteseka amani pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atadhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake, siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.