2 Samueli 9:1-10
2 Samueli 9:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Daudi aliuliza, “Je, kuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani.” Kulikuwa na mtumishi wa jamaa ya Shauli aliyeitwa Siba. Siba aliitwa kwenda kwa Daudi. Mfalme Daudi alimwuliza, “Je wewe ndiye Siba?” Naye akamjibu, “Naam, mimi mtumishi wako ndiye.” Mfalme akamwuliza, “Je, hakuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema wa Mungu.” Siba akamjibu, “Yuko mwana wa Yonathani, lakini yeye amelemaa miguu.” Mfalme akamwuliza, “Yuko wapi?” Siba akamjibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari.” Basi, mfalme Daudi akatuma watu, naye akaletwa kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari. Basi, Mefiboshethi mwana wa Yonathani, na mjukuu wa Shauli akaenda kwa mfalme Daudi, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme Daudi, akasujudu. Daudi akamwita, “Mefiboshethi.” Naye akamjibu, “Naam! Mimi hapa mtumishi wako.” Daudi akamwambia, “Usiogope. Mimi nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Ile ardhi yote iliyokuwa ya babu yako Shauli nitakurudishia. Nawe, daima utakula mezani pangu.” Mefiboshethi akasujudu, na kusema, “Mimi ni sawa na mbwa mfu; kwa nini unishughulikie hivyo?” Kisha, mfalme Daudi akamwita Siba mtumishi wa Shauli, akamwambia, “Ile mali yote iliyokuwa ya Shauli na jamaa yake nimempa mjukuu wa bwana wako. Wewe, watoto wako na watumishi wako mtakuwa mnamlimia Mefiboshethi na mtamletea mavuno ili mjukuu wa bwana wako awe daima na chakula. Lakini yeye atakula mezani pangu.” Wakati huo, Siba alikuwa na watoto wa kiume kumi na watano na watumishi ishirini.
2 Samueli 9:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani? Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumishi wako ndiye. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu yeyote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, na kumwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumishi wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, babu yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumishi wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumishi wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mjukuu wa bwana wako. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumishi wako; nawe utamletea mjukuu wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mjukuu wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu siku zote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumishi ishirini.
2 Samueli 9:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani? Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumwa wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mwana wa bwana wako. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumwa wako; nawe utamletea mwana wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mwana wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu sikuzote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumwa ishirini.
2 Samueli 9:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Daudi akauliza, “Je, hakuna mtu hata mmoja wa nyumba ya Sauli aliyebaki ambaye naweza kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani?” Basi palikuwa na mtumishi wa nyumba ya Sauli aliyeitwa Siba. Wakamwita aje mbele ya Daudi, naye mfalme akamuuliza, “Wewe ndiwe Siba?” Akamjibu, “Naam, mimi ndiye mtumishi wako.” Mfalme akamuuliza, “Je, hakuna yeyote ambaye amebaki wa nyumba ya Sauli ninayeweza kumwonesha wema wa Mungu?” Siba akamjibu mfalme, “Bado yupo mwana wa Yonathani; yeye ni kiwete kwenye miguu yote.” Mfalme akauliza, “Yuko wapi?” Siba akajibu, “Yuko nyumbani mwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-Debari.” Basi Mfalme Daudi akamtaka aletwe kutoka Lo-Debari, kutoka nyumbani mwa Makiri mwana wa Amieli. Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, alipofika kwa Daudi, akainama kumpa mfalme heshima. Daudi akamwita, “Mefiboshethi!” Mefiboshethi akajibu, “Ndimi mtumishi wako.” Daudi akamwambia, “Usiogope, kwa maana hakika nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Nitakurudishia ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli baba yako, nawe daima utakula chakula mezani pangu.” Mefiboshethi akasujudu, akasema, “Mimi mtumishi wako ni nini hata uangalie mbwa mfu kama mimi?” Ndipo mfalme akamwita Siba mtumishi wa Sauli na kumwambia, “Nimempa mwana wa bwana wako kila kitu kilichokuwa mali ya Sauli na jamaa yake. Wewe, wanao na watumishi wako mtamlimia mashamba Mefiboshethi na kumletea mavuno, ili mwana wa bwana wako apate mahitaji yake. Naye Mefiboshethi mwana wa bwana wako atakula chakula mezani pangu daima.” (Siba alikuwa na wana kumi na watano, na watumishi ishirini.)