2 Samueli 7:10-13
2 Samueli 7:10-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi, niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali, tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli, nami nitakulinda kutokana na adui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba. Siku zako zitakapotimia na utakapofariki na kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako wewe mwenyewe awe mfalme, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu na kiti chake cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele.
2 Samueli 7:10-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama ilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele.
2 Samueli 7:10-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele.
2 Samueli 7:10-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzoni, na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa amani mbele ya adui zenu wote. “ ‘BWANA akuambia kwamba BWANA mwenyewe atakujengea nyumba. Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitakiimarisha kiti cha ufalme wake milele.