Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 7:1-29

2 Samueli 7:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, naye Mwenyezi-Mungu amemuwezesha kuwa na amani na adui zake kila upande, mfalme Daudi akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama; mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa mierezi, lakini sanduku la Mungu linakaa hemani.” Nathani akamwambia mfalme, “Nenda ufanye chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu yu pamoja nawe.” Lakini usiku uleule neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Je, wewe utanijengea nyumba ya kukaa? Tangu siku ile nilipowatoa Waisraeli nchini Misri mpaka hivi leo sijaishi kwenye nyumba. Nimetembea kila mahali nikiwa ninakaa hemani. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli wote nimemwuliza mtu yeyote wa Israeli ambaye nilimwamuru awachunge watu wa Israeli: Kwa nini hajanijengea nyumba ya mierezi? Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulikokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli. Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza adui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine duniani. Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi, niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali, tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli, nami nitakulinda kutokana na adui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba. Siku zako zitakapotimia na utakapofariki na kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako wewe mwenyewe awe mfalme, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu na kiti chake cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Akifanya maovu, nitamrudi kama wanadamu wanavyowarudi wana wao kwa fimbo. Lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyoziondoa kwa Shauli, niliyemwondoa mbele yako. Ukoo wako na ufalme wako vitadumu imara daima. Kiti chako cha enzi kitakuwa imara milele.’” Nathani alimweleza Daudi kila kitu ambacho alioneshwa katika maono hayo na Mungu. Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu; halafu akaomba, “Mimi ni nani ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini hata ukaniinua mpaka hapa nilipo leo! Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Bwana Mungu; zaidi ya hayo umeiahidi jamaa yangu mambo makubwa katika miaka mingi ijayo; na kwamba umenijalia kuona hayo, Ee Bwana Mungu. Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi, mtumishi wako? Kwani wewe unanijua mimi mtumishi wako, ee Bwana Mungu! Kutokana na ahadi yako na kulingana na moyo wako, umetenda makuu hayo yote ili unijulishe mimi mtumishi wako. Kutokana na yale tuliyosikia, wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu; hakuna aliye kama wewe, na hakuna Mungu mwingine ila wewe. Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kufananishwa na watu wako wa Israeli, ambao Mungu wake alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ee Mungu ulijifanyia jina na kujitendea mambo makubwa na ya ajabu kwa ajili ya nchi yako mbele ya watu wako ambao kwa ajili yako mwenyewe uliwaokoa kutoka Misri, ukayafukuza mataifa na miungu yake mbele yao? Hata umewaimarisha watu wako wa Israeli kwa ajili yako mwenyewe, ili wawe watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu umekuwa Mungu wao. Basi, sasa, ee Mwenyezi-Mungu, ikamilishe ile ahadi uliyosema kuhusu mimi mtumishi wako na kuhusu jamaa yangu kama ulivyoahidi. Nalo jina lako litatukuzwa milele, nao watu watasema, ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni Mungu juu ya Israeli!’ Na jamaa yangu, mimi Daudi mtumishi wako, itaimarika mbele yako. Maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi mtumishi wako, ukisema ‘Nitakujengea nyumba;’ ndio maana nina ujasiri kutoa ombi hili mbele yako. Sasa, ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ni kweli na umeniahidi mimi mtumishi wako jambo hili jema; kwa hiyo, nakuomba nyumba yangu mimi mtumishi wako ipate kudumu milele mbele yako; kwani wewe umesema hivyo, pia kwa baraka zako nyumba yangu itabarikiwa milele.”

2 Samueli 7:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yuko pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, Nenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. Mahali kote nilikokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lolote na mtu yeyote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nilikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama ilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitaimarishwa milele. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi. Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumishi wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU. Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumishi wako, Ee Bwana MUNGU. Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumishi wako. Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee BWANA Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao. Nawe ulijifanyia imara watu wako wa Israeli, wawe watu wako milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, neno lile ulilolinena kuhusu mtumishi wako, na kuhusu nyumba yangu, uliimarishe milele, ukatende kama ulivyosema. Jina lako na litukuzwe milele, kwa kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumishi wako, Daudi, itaimarika mbele zako. Kwa kuwa wewe, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumishi wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumishi wako, nimepata ujasiri nikuombe ombi hili. Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumishi wako jambo hili jema basi, sasa, uwe radhi, ukaibariki nyumba ya mtumishi wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumishi wako na ibarikiwe milele.

2 Samueli 7:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi. Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU. Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumwa wako, Ee Bwana MUNGU. Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumwa wako. Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee BWANA Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao. Nawe ulijifanyia imara watu wako Israeli, wawe watu wako milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yangu, ulifanye imara milele, ukatende kama ulivyosema. Jina lako na litukuzwe milele, kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumwa wako, Daudi, itakuwa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii. Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele.

2 Samueli 7:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye BWANA akiwa amempa amani pande zote kutoka kwa adui zake, akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa ninaishi katika jumba la kifalme la mwerezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.” Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana BWANA yu pamoja nawe.” Usiku ule neno la BWANA likamjia Nathani, kusema: “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake? Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine na hema kama makao yangu. Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mwerezi?” ’ “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: Nilikutoa malishoni na kutoka kulisha mifugo, ili uwaongoze watu wangu Israeli. Nimekuwa pamoja nawe popote ulipoenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzoni, na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa amani mbele ya adui zenu wote. “ ‘BWANA akuambia kwamba BWANA mwenyewe atakujengea nyumba. Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitakiimarisha kiti cha ufalme wake milele. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu. Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako. Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha utawala kitaimarishwa milele.’ ” Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya. Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za BWANA, akasema: “Ee BWANA Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee BWANA Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee BWANA Mwenyezi? “Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee BWANA Mwenyezi. Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako. “Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee BWANA Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe, Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee BWANA, umekuwa Mungu wao. “Basi sasa, BWANA Mungu, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Fanya kama ulivyoahidi, ili jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘BWANA wa majeshi ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako. “Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hili. Ee BWANA Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee BWANA Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”