2 Samueli 5:1-5
2 Samueli 5:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha makabila yote ya Israeli yalimwendea Daudi huko Hebroni, na kumwambia, “Tazama, sisi ni mwili na damu yako. Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wetu wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu alikuambia ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli na utakuwa mkuu juu ya Israeli.’” Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme Daudi huko Hebroni; naye akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, na alitawala kwa muda wa miaka arubaini. Huko Hebroni, alitawala watu wa Yuda kwa muda wa miaka saba na miezi sita, na huko Yerusalemu alitawala watu wa Israeli pamoja na Yuda kwa muda wa miaka thelathini na mitatu.
2 Samueli 5:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo watu wa kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli wakitoka nje kwenda, na kurudi vitani. Naye BWANA akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za BWANA; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arubaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda.
2 Samueli 5:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye BWANA akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za BWANA; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda.
2 Samueli 5:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu mwili wako na damu yako. Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye BWANA alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ” Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za BWANA, nao wakampaka Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli kwa miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na tatu.