2 Samueli 5:1-25
2 Samueli 5:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha makabila yote ya Israeli yalimwendea Daudi huko Hebroni, na kumwambia, “Tazama, sisi ni mwili na damu yako. Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wetu wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu alikuambia ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli na utakuwa mkuu juu ya Israeli.’” Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme Daudi huko Hebroni; naye akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, na alitawala kwa muda wa miaka arubaini. Huko Hebroni, alitawala watu wa Yuda kwa muda wa miaka saba na miezi sita, na huko Yerusalemu alitawala watu wa Israeli pamoja na Yuda kwa muda wa miaka thelathini na mitatu. Baadaye mfalme na watu wake walikwenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Lakini wao wakamwambia, “Hutaingia mjini humu, kwani vipofu na vilema watakufukuzia mbali.” Walimwambia hivyo kwani walifikiri kuwa Daudi asingeweza kuingia mjini humo. Hata hivyo, mfalme Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi. Siku hiyo, Daudi alisema, “Mtu yeyote atakayewapiga Wayebusi na apitie kwenye mfereji wa maji ili kuwashambulia vilema na vipofu ambao roho yangu inawachukia.” Ndio maana watu husema, “Vipofu na vilema hawataingia nyumbani.” Daudi alikaa kwenye ngome hiyo, nao mji akauita, “Mji wa Daudi.” Daudi aliujenga mji kuuzunguka, akianzia Milo kuelekea ndani. Naye Daudi akazidi kuwa maarufu zaidi kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye. Kisha, mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi; alimpelekea pia mierezi, maseremala na waashi ambao walimjengea Daudi ikulu. Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ameukuza ufalme wake kwa ajili ya watu wake wa Israeli. Daudi alijitwalia masuria na wake zaidi wa huko mjini Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni. Hao, wakamzalia watoto zaidi wa kiume na wa kike. Yafuatayo ndiyo majina ya watoto wa kiume, wake zake waliomzalia huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia, Elishama, Eliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wote walitoka kwenda kumtafuta, lakini yeye alipata habari, akaingia ndani ya ngome. Wafilisti walifika na kujitawanya kwenye Bonde la Refaimu. Basi, Daudi alimwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Daudi, “Nenda, maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Basi, Daudi akafika Baal-perasimu, na kuwashinda Wafilisti; halafu akasema, “Mwenyezi-Mungu amepita katikati ya adui zangu kama mafuriko ya maji yaendayo kasi.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-perasimu. Wafilisti waliziacha sanamu zao za miungu mahali hapo, naye Daudi na watu wake wakazichukua. Kwa mara ya pili, Wafilisti walifika tena na kujitawanya kwenye bonde la Refaimu. Daudi alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiwashambulie kutoka hapa ulipo, bali zunguka na kuwashambulia kutoka mkabala wa miti na miforosadi. Na mara mtakaposikia vishindo vya gwaride kwenye vilele vya miforosadi hiyo, hapo jipe moyo kwani nitakuwa nimetoka ili kukutangulia kulipiga jeshi la Wafilisti.” Daudi alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, naye akawapiga Wafilisti kutoka Geba hadi Gezeri.
2 Samueli 5:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo watu wa kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli wakitoka nje kwenda, na kurudi vitani. Naye BWANA akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za BWANA; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arubaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda. Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; nao wakamwambia Daudi, hutaingia humu kamwe; maana hata vipofu na viwete watakufukuzia mbali; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. Lakini Daudi aliiteka ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. Naye Daudi alisema siku hiyo, Yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, na kuwapiga viwete, na hao vipofu, ambao roho yake Daudi inawachukia. Kwa sababu hii watu husema, Wako vipofu na viwete hawawezi kuingia nyumbani. Basi Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani. Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana BWANA, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye. Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba. Akajua Daudi ya kwamba BWANA amemweka imara awe mfalme juu ya Israeli, na ufalme wake ameutukuza kwa ajili ya watu wake, Israeli. Naye Daudi akazidi kujitwalia masuria na wake huko Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni; wakazaliwa zaidi kwa Daudi wana na binti. Na haya ndiyo majina ya hao waliozaliwa kwake huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani, na Ibhari, na Elishua; na Nefegi, na Yafia; na Elishama, na Eliada, na Elifeleti. Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai. Basi Daudi akauliza kwa BWANA, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye BWANA akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako. Basi Daudi akaja Baal-perasimu, naye Daudi akawapiga huko; akasema, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu. Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali. Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai. Naye Daudi alipouliza kwa BWANA, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi. Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo BWANA ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti. Ndivyo alivyotenda Daudi, vile vile kama BWANA alivyomwagiza; naye akawapiga Wafilisti toka Geba hata ujapo Gezeri.
2 Samueli 5:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye BWANA akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za BWANA; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda. Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. Naye Daudi alisema siku hiyo, Yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, na kuwapiga viwete, na hao vipofu, ambao roho yake Daudi inawachukia. Kwa sababu hii watu husema, Wako vipofu na viwete hawawezi kuingia nyumbani. Basi Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani. Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana BWANA, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye. Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba. Akajua Daudi ya kwamba BWANA amemweka imara awe mfalme juu ya Israeli, na ufalme wake ameutukuza kwa ajili ya watu wake, Israeli. Naye Daudi akazidi kujitwalia masuria na wake huko Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni; wakazaliwa zaidi kwa Daudi wana na binti. Na haya ndiyo majina ya hao waliozaliwa kwake huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani, na Ibhari, na Elishua; na Nefegi, na Yafia; na Elishama, na Eliada, na Elifeleti. Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai. Basi Daudi akauliza kwa BWANA, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye BWANA akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako. Basi Daudi akaja Baal-perasimu, naye Daudi akawapiga huko; akasema, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu. Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali. Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai. Naye Daudi alipouliza kwa BWANA, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi. Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo BWANA ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti. Ndivyo alivyotenda Daudi, vile vile kama BWANA alivyomwagiza; naye akawapiga Wafilisti toka Geba hata ujapo Gezeri.
2 Samueli 5:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu mwili wako na damu yako. Zamani, wakati Sauli alikuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani. Naye BWANA alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ” Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za BWANA, nao wakampaka Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli. Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli kwa miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na tatu. Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi humo. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.” Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi. Siku ile, Daudi akasema, “Yeyote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.” Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo kuelekea ndani. Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu BWANA Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye. Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mwerezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi. Naye Daudi akafahamu kuwa BWANA amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli, watu wake. Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana wengi wa kiume na wa kike walizaliwa kwake. Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani, Ibihari, Elishua, Nefegi, Yafia, Elishama, Eliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia kuwa Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akateremka kwenye ngome. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Warefai, kwa hiyo Daudi akamuuliza BWANA, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” BWANA akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Ndipo Daudi akaenda Baal-Perasimu, na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yanavyofurika, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu. Wafilisti wakaziacha sanamu zao huko, naye Daudi na watu wake wakazichukua. Wafilisti walikwea kwa mara nyingine na kusambaa katika Bonde la Warefai. Kwa hiyo Daudi akamuuliza BWANA, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi. Mara utakaposikia sauti ya kutembea kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa BWANA ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.” Basi Daudi akafanya kama BWANA alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Geba hadi Gezeri.