Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 24:1-24

2 Samueli 24:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa mara nyingine, Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia Waisraeli, akamchochea Daudi dhidi yao, akamwambia awahesabu watu wa Israeli na watu wa Yuda. Hivyo, mfalme akamwambia Yoabu, na makamanda wa jeshi waliokuwa pamoja naye, “Nendeni katika makabila yote ya Israeli kutoka Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu ili nipate kujua idadi yao.” Lakini Yoabu akamwambia mfalme, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa, nawe bwana wangu mfalme upate kuona ongezeko hilo kwa macho yako mwenyewe. Lakini, kwa nini wewe bwana wangu mfalme unapendezwa na jambo hili?” Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu na makamanda wa jeshi! Basi, Yoabu na makamanda wa jeshi wakaondoka mbele ya mfalme, wakaenda kuwahesabu Waisraeli. Walivuka mto Yordani wakianzia kuhesabu watu tangu Aroeri na mto ulioko bondeni kuelekea Gadi hadi Yazeri. Kisha, wakaenda Gileadi halafu Kadeshi katika nchi ya Wahiti, halafu wakawasili Dani na kutoka Dani wakazunguka kwenda Sidoni, na kufika kwenye ngome ya mji wa Tiro, wakaingia kwenye miji yote ya Wahivi na Wakanaani. Kisha, walitoka wakaenda Negebu ya Yuda huko Beer-sheba. Walipokwisha pitia katika nchi yote, walirejea Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. Halafu Yoabu alimpelekea mfalme idadi ya watu. Katika Israeli kulikuwamo wanaume mashujaa 800,000 wenye ujuzi wa kutumia mapanga; na katika Yuda, kulikuwa na wanaume 500,000. Lakini Daudi alisumbuliwa sana rohoni mwake baada ya kuwahesabu watu. Kwa hiyo, Daudi akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo nililolifanya. Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.” Daudi alipoamka kesho yake asubuhi, wakati huo Mwenyezi-Mungu alimpa ujumbe nabii Gadi mwonaji wa mfalme Daudi, akisema, “Nenda ukamwambie hivi Daudi: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Ninakupa mambo matatu, nawe ujichagulie mojawapo, nami nitakutendea.’” Hivyo, Gadi akamwendea Daudi na kumweleza, akisema, “Je, wapendelea njaa ya miaka saba iijie nchi yako? Au je, wewe uwakimbie adui zako kwa miezi mitatu wanapokufuatia? Au kuwe na siku tatu ambapo nchi yako itakuwa na maradhi mabaya? Fikiri unipe jibu nitakalompa yeye aliyenituma.” Daudi akamjibu Gadi, “Nina mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu, kuliko kutiwa mikononi mwa watu, maana yeye ana huruma sana.” Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi, tangu asubuhi hadi wakati uliopangwa. Watu 70,000 walikufa nchini kote kutoka Dani mpaka Beer-sheba. Lakini wakati malaika aliponyosha mkono wake kuelekea mji wa Yerusalemu ili kuuangamiza, Mwenyezi-Mungu alibadilisha nia yake. Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo malaika aliyetekeleza maangamizi kwa watu, “Basi! Yatosha; rudisha mkono wako.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna, Myebusi. Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa anawaua watu, alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama, Mimi ndiye niliye na hatia! Mimi mwenyewe nimekosa! Hawa watu wapole hawakufanya uovu. Nakusihi sana uniadhibu mimi na jamaa ya baba yangu.” Siku hiyohiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, “Panda juu, ukamjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Arauna, Myebusi.” Basi, Daudi akapanda juu kufuatana na neno la Gadi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru. Arauna alipoangalia upande wa chini alimwona mfalme akimkaribia pamoja na watumishi wake, naye akatoka, akaenda na kumsujudia mfalme, akainama mpaka chini ardhini. Kisha Arauna akamwuliza mfalme, “Kwa nini bwana wangu mfalme amenijia mimi mtumishi wake?” Daudi akamjibu, “Nimekuja kununua uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu ili tauni iliyowakumba watu ikome.” Naye Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme, chukua chochote unachoona kinafaa na utolee sadaka. Mimi nawatoa fahali hawa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na vifaa hivi vya kupuria na nira za ng'ombe kuwa kuni. Hivi vyote, ee mfalme, nakupa. Natumaini Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atapokea sadaka yako kwa wema.” Lakini mfalme akamwambia Arauna, “La! Wewe hutanipa chochote. Mimi nitavinunua kwako kwa thamani yake. Sitamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.” Hivyo, mfalme Daudi alinunua uwanja wa kupuria na fahali kwa fedha shekeli hamsini.

2 Samueli 24:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akamchochea Daudi juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu watu wa Israeli na Yuda. Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua idadi yao. Naye Yoabu akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na awaongeze watu, hesabu yao ikiwa yoyote, mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu, na juu ya majemadari wa jeshi. Basi Yoabu akatoka na majemadari wa jeshi machoni pa mfalme, kwenda kuwahesabu watu wa Israeli. Wakavuka Yordani, wakapiga kambi huko Aroeri, upande wa kulia wa mji ulioko kati ya bonde la Gadi, na mpaka Yazeri; kisha wakaja Gileadi, na nchi ya Wahiti huko Kadeshi; kisha wakaja Dani, na kutoka Dani wakazunguka mpaka Sidoni, wakaja ngomeni kwa Tiro, na kwa miji yote ya Wahivi, na ya Wakanaani; tena wakaenda katika Negebu ya Yuda huko Beer-sheba. Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa elfu mia nane wenye kufuta panga; nao wa Yuda walikuwa watu elfu mia tano. Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia BWANA, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee BWANA, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la BWANA likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, na kusema, Nenda, ukanene na Daudi, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Amua sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hadi wakati ulioamriwa; nao wakafa watu elfu sabini toka Dani mpaka Beer-sheba. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, BWANA akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa BWANA alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi, alipomwona malaika aliyewapiga watu, akanena na BWANA, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu. Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea kama alivyoagizwa na Gadi, kama BWANA alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifudifudi hadi chini. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumishi wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Nimekuja kununua kwako kiwanja hiki cha kupuria, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili tauni ipate kuzuiliwa kwa watu. Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, natoa ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni, vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa isiyonigharimu chochote. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha.

2 Samueli 24:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda. Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu. Naye Yoabu akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na awaongeze watu, hesabu yao ikiwa yo yote, mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu, na juu ya majemadari wa jeshi. Basi Yoabu akatoka na majemadari wa jeshi machoni pa mfalme, kwenda kuwahesabu watu wa Israeli. Wakavuka Yordani, wakapiga kambi huko Aroeri, upande wa kuume wa mji ulioko kati ya bonde la Gadi, na mpaka Yazeri; kisha wakaja Gileadi, na nchi ya Wahiti huko Kadeshi; kisha wakaja Dani, na kutoka Dani wakazunguka mpaka Sidoni, wakaja ngomeni kwa Tiro, na kwa miji yote ya Wahivi, na ya Wakanaani; tena wakatoka kusini kwa Yuda huko Beer-sheba. Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu mwisho wa miezi kenda na siku ishirini. Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu. Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia BWANA, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee BWANA, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la BWANA likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema, Nenda, ukanene na Daudi, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, BWANA akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa BWANA alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na BWANA, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu. Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama BWANA alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee BWANA madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu. Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng’ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng’ombe, viko kwa kuni, vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng’ombe kwa shekeli hamsini za fedha.

2 Samueli 24:1-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hasira ya BWANA ikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.” Kwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.” Lakini Yoabu akamjibu mfalme, “BWANA Mungu wako na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?” Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi; kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli. Baada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini mwa mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri. Walienda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni. Kisha wakaelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walienda Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda. Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. Yoabu akamtolea mfalme idadi ya wapiganaji: Katika Israeli kulikuwa wanaume wenye uwezo elfu mia nane ambao wangeweza kutumia upanga, na katika Yuda watu elfu mia tano. Dhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambia BWANA, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Ee BWANA, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.” Kabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno la BWANA lilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema: “Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ” Basi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.” Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa BWANA, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.” Basi BWANA akatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi hadi muda ulioamriwa, wakafa watu elfu sabini kuanzia Dani hadi Beer-Sheba. Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, BWANA akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa BWANA alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi. Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia BWANA, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.” Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengee BWANA madhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.” Kwa hiyo Daudi akakwea kama vile BWANA alivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi. Arauna alipotazama na kumwona mfalme na maafisa wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu, uso wake ukagusa chini mbele ya mfalme. Arauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?” Daudi akajibu, “Nimekuja kununua sakafu yako ya kupuria, niweze kumjengea BWANA madhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.” Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ngʼombe kwa ajili ya kuni. Ee mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “BWANA Mungu wako na akukubali.” Lakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha! Nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA Mungu wangu isiyonigharimu chochote.” Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha.