2 Samueli 22:1-51
2 Samueli 22:1-51 Biblia Habari Njema (BHN)
Daudi alimwimbia Mwenyezi-Mungu maneno ya wimbo ufuatao siku ile Mwenyezi-Mungu alipomkomboa mikononi mwa adui zake, na mkononi mwa Shauli. Alisema, “Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu, na mkombozi wangu. Mungu wangu, mwamba wangu, ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu ya wokovu wangu, ngome yangu na kimbilio langu. Mwokozi wangu; unaniokoa kutoka kwa watu wakatili. Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie, nami naokolewa kutoka kwa adui zangu. “Maana mawimbi ya kifo yalinizingira, mafuriko ya maangamizi yalinivamia; kamba za kuzimu zilinizinga, mitego ya kifo ilinikabili. “Katika taabu yangu, nilimwita Mwenyezi-Mungu; nilimwita Mungu wangu. Toka hekaluni mwake aliisikia sauti yangu, kilio changu kilimfikia masikioni mwake. “Hapo, dunia ikatetemeka na kutikisika, misingi ya mbinguni ikayumbayumba na kuruka, kwani Mungu alikuwa amekasirika. Moshi ulifuka kutoka puani mwake, moto uunguzao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake. Aliinamisha anga, akashuka chini; na wingu jeusi chini ya miguu yake. Alipanda kiumbe chenye mabawa na kuruka, alionekana juu ya mabawa ya upepo. Alijizungushia giza pande zote, kifuniko chake kilikuwa mawingu mazito na mkusanyiko wa maji. Umeme ulimulika mbele yake, kulilipuka makaa ya moto. Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni, Mungu Mkuu akatoa sauti yake. Aliwalenga adui mishale, akawatawanya, alirusha umeme, akawatimua. Mwenyezi-Mungu alipowakemea, kutokana na pumzi ya puani mwake, vilindi vya bahari vilifunuliwa, misingi ya dunia ikaonekana. “Mungu alinyosha mkono wake toka juu, akanichukua, kutoka kwenye maji mengi alininyanyua. Aliniokoa kutoka kwa adui yangu mwenye nguvu, aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia maana walikuwa na nguvu nyingi kunishinda. Walinivamia nilipokuwa taabuni, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu. Alinileta, akaniweka mahali pa usalama, alinisalimisha, kwani alipendezwa nami. “Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu; alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia. Maana, nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu, wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu. Nimeshika maagizo yake yote, sikuacha kufuata masharti yake. Mbele yake sikuwa na hatia, nimejikinga nisiwe na hatia. Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu, yeye anajua usafi wangu. “Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu, mwema kwa wale walio wema. Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu, lakini mkatili kwa watu walio waovu. Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu, lakini wawaangalia wenye majivuno kuwaporomosha. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe u taa yangu, Mungu wangu, unayefukuza giza langu. Kwa msaada wako, wakishambulia kikosi; wewe wanipa nguvu ya kuruka kuta zake. Anachofanya Mungu hakina dosari! Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika; yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia. “Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu? Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu? Mungu huyu ndiye kimbilio langu imara, na ameifanya njia yangu iwe salama. Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa, na kuniweka salama juu ya vilele. Hunifunza kupigana vita, mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba. Umenipa ngao yako ya kuniokoa; msaada wako umenifanya mkuu. Umenirahisishia njia yangu; wala miguu yangu haikuteleza. Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza, sikurudi nyuma mpaka wameangamizwa. Niliwaangamiza, nikawaangusha chini wasiweze kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha adui chini yangu. Uliwafanya adui zangu wakimbie, na wale walionichukia niliwaangamiza. Walitafuta msaada, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa, walimlilia Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwajibu. Niliwatwanga na kuwaponda kama mavumbi ya nchi, nikawaponda na kuwakanyaga kama matope barabarani. “Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu, umenifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea, mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. “Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wangu! Atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi na kuyatiisha mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka adui zangu. Ee Mwenyezi-Mungu, ulinikuza juu ya wapinzani wangu na kunisalimisha mbali na watu wakatili. “Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo aliyemweka wakfu, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.”
2 Samueli 22:1-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na mkononi mwa Sauli; akasema, BWANA ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na kimbilio langu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri. Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu. Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nilimwita BWANA, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu; Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasukasuka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala; Makaa yakawashwa nao. Aliziinamisha mbingu akashuka; Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. Akapanda juu ya kerubi akaruka; Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo. Akafanya giza hema zake za kumzunguka, Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni. Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Makaa ya moto yakawashwa. BWANA alipiga radi toka mbinguni, Naye Aliye Juu akaitoa sauti yake. Akapiga mishale, akawatawanya; Umeme, naye akawatimua. Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Kwa kukemea kwake BWANA, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake. Alipeleka kutoka juu, akanishika; Akanitoa katika maji mengi; Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia; Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu; Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea kulingana na haki yangu; Kulingana na usafi wa mikono yangu akanilipa. Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. Maana hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu; Na kuhusu amri zake, sikuziacha. Nami nilikuwa mkamilifu kwake, Nikajilinda na uovu wangu. Basi BWANA amenilipa kulingana na haki yangu; Kulingana na usafi wa mikono yangu mbele zake. Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionesha kuwa mkaidi. Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako huwapinga wenye kiburi, uwadhili. Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA; Na BWANA ataniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu ninaruka ukuta. Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya BWANA imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye Mungu, ila BWANA? Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu? Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake. Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu inaupanda upinde wa shaba. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako; Na unyenyekevu wako umenikuza. Umezifanyia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza. Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hadi walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenijaza nguvu ya kupigana vita; Ukawafanya adui zangu wafifie chini yangu. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni walinijia wakinyenyekea; Mara tu waliposikia habari zangu, Walinitii. Wageni nao waliishiwa nguvu, Wakatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA yu hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anilipiziaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kuniokoa kutoka kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Ukaniokoa kutoka kwa watu wajeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Yeye ni mnara wa wokovu kwa mfalme wake; Amfanyia fadhili masihi wake, Kwa Daudi na wazawa wake, hata milele.
2 Samueli 22:1-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake zote, na mkononi mwa Sauli; akasema, BWANA ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu; Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio yangu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri. Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu. Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita BWANA, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu; Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasuka-suka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala; Makaa yakawashwa nao. Aliziinamisha mbingu akashuka; Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. Akapanda juu ya kerubi akaruka; Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo. Akafanya giza hema zake za kumzunguka, Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni. Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Makaa ya moto yakawashwa. BWANA alipiga radi toka mbinguni, Naye Aliye juu akaitoa sauti yake. Akapiga mishale, akawatawanya; Umeme, naye akawatapanya. Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Kwa kukemea kwake BWANA, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake. Alipeleka kutoka juu, akanishika; Akanitoa katika maji mengi; Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia; Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu; Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa. Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. Maana hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu; Na kwa habari za amri zake, sikuziacha. Nami nalikuwa mkamilifu kwake, Nikajilinda na uovu wangu. Basi BWANA amenilipa sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake. Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako ni juu ya wenye kiburi, uwadhili. Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA; Na BWANA ataniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya BWANA imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye Mungu, ila BWANA? Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu? Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake. Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu yaupinda upinde wa shaba. Nawe umenipa ngao ya wokovu wako; Na unyenyekevu wako umenikuza. Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza. Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hata walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga-piga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu. Maana umenifunga mshipi wa nguvu kwa vita; Umenitiishia chini yangu walioniondokea. Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia. Walitazama, lakini hakuna wa kuokoa; Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu. Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya. Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia. Wageni watanijia wakinyenyekea; Kwa kusikia tu habari zangu, Mara watanitii. Wageni nao watatepetea, Watatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa mwamba wa wokovu wangu; Naam, Mungu anipatiaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu, Na kunileta nje nitoke kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Waniponya na mtu wa jeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu; Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake, hata milele.
2 Samueli 22:1-51 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Daudi alimwimbia BWANA maneno ya wimbo huu BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Akasema: “BWANA ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, Mungu wangu ni mwamba wangu, ninayemkimbilia, ngao yangu na pembe ya wokovu wangu. Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu na mwokozi wangu, huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri. “Ninamwita BWANA, anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu. Mawimbi ya mauti yalinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea. Kamba za Kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili. “Katika shida yangu nalimwita BWANA, nilimlilia Mungu wangu. Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika masikioni mwake. Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya mbingu ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika. Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yaliyowaka yakatoka ndani yake. Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake. Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mabawa ya upepo. Alifanya giza hema lake la kujifunika: mawingu meusi ya mvua ya angani. Kutokana na mwanga wa uwepo wake mwanga wa radi ukatoka. BWANA alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika. Aliipiga mishale na kutawanya adui, akawafukuza kwa umeme mkubwa wa radi. Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwake BWANA, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake. “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu. Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini BWANA alikuwa msaada wangu. Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami. “BWANA alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa. Kwa maana nimezishika njia za BWANA; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu. Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake. Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi. BWANA amenilipa sawasawa na uadilifu wangu, sawasawa na usafi wangu machoni pake. “Kwa yeye aliye mwaminifu unajionesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia unajionesha kutokuwa na hatia, kwa aliye mtakatifu unajionesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka unajionesha kuwa mkaidi. Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi ili uwashushe. Wewe ni taa yangu, Ee BWANA. BWANA hulifanya giza langu kuwa mwanga. Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta. “Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu; neno la BWANA halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake. Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya BWANA? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu? Mungu ndiye anivikaye nguvu, na kufanya njia yangu kuwa kamilifu. Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu. Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba. Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu; msaada wako umeniinua niwe mkuu. Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze. “Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta, sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa. Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu. Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu. Walipiga yowe, lakini hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia BWANA, lakini hakuwajibu. Niliwaponda kama mavumbi ya nchi; niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani. “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu; umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa. Watu ambao sikuwajua wananitumikia, nao wageni huja wakininyenyekea, mara wanisikiapo, hunitii. Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka. “BWANA yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu! Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, ayawekaye mataifa chini yangu, aniwekaye huru toka kwa adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri. Kwa hiyo nitakusifu, Ee BWANA, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako. “Humpa mfalme wake ushindi mkuu; huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.”