2 Samueli 22:1-25
2 Samueli 22:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Daudi alimwimbia Mwenyezi-Mungu maneno ya wimbo ufuatao siku ile Mwenyezi-Mungu alipomkomboa mikononi mwa adui zake, na mkononi mwa Shauli. Alisema, “Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu, ngome yangu, na mkombozi wangu. Mungu wangu, mwamba wangu, ninayemkimbilia usalama; ngao yangu, nguvu ya wokovu wangu, ngome yangu na kimbilio langu. Mwokozi wangu; unaniokoa kutoka kwa watu wakatili. Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie, nami naokolewa kutoka kwa adui zangu. “Maana mawimbi ya kifo yalinizingira, mafuriko ya maangamizi yalinivamia; kamba za kuzimu zilinizinga, mitego ya kifo ilinikabili. “Katika taabu yangu, nilimwita Mwenyezi-Mungu; nilimwita Mungu wangu. Toka hekaluni mwake aliisikia sauti yangu, kilio changu kilimfikia masikioni mwake. “Hapo, dunia ikatetemeka na kutikisika, misingi ya mbinguni ikayumbayumba na kuruka, kwani Mungu alikuwa amekasirika. Moshi ulifuka kutoka puani mwake, moto uunguzao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake. Aliinamisha anga, akashuka chini; na wingu jeusi chini ya miguu yake. Alipanda kiumbe chenye mabawa na kuruka, alionekana juu ya mabawa ya upepo. Alijizungushia giza pande zote, kifuniko chake kilikuwa mawingu mazito na mkusanyiko wa maji. Umeme ulimulika mbele yake, kulilipuka makaa ya moto. Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni, Mungu Mkuu akatoa sauti yake. Aliwalenga adui mishale, akawatawanya, alirusha umeme, akawatimua. Mwenyezi-Mungu alipowakemea, kutokana na pumzi ya puani mwake, vilindi vya bahari vilifunuliwa, misingi ya dunia ikaonekana. “Mungu alinyosha mkono wake toka juu, akanichukua, kutoka kwenye maji mengi alininyanyua. Aliniokoa kutoka kwa adui yangu mwenye nguvu, aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia maana walikuwa na nguvu nyingi kunishinda. Walinivamia nilipokuwa taabuni, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu. Alinileta, akaniweka mahali pa usalama, alinisalimisha, kwani alipendezwa nami. “Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu; alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia. Maana, nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu, wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu. Nimeshika maagizo yake yote, sikuacha kufuata masharti yake. Mbele yake sikuwa na hatia, nimejikinga nisiwe na hatia. Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu, yeye anajua usafi wangu.
2 Samueli 22:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na mkononi mwa Sauli; akasema, BWANA ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na kimbilio langu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri. Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu. Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nilimwita BWANA, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu; Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasukasuka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala; Makaa yakawashwa nao. Aliziinamisha mbingu akashuka; Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. Akapanda juu ya kerubi akaruka; Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo. Akafanya giza hema zake za kumzunguka, Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni. Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Makaa ya moto yakawashwa. BWANA alipiga radi toka mbinguni, Naye Aliye Juu akaitoa sauti yake. Akapiga mishale, akawatawanya; Umeme, naye akawatimua. Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Kwa kukemea kwake BWANA, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake. Alipeleka kutoka juu, akanishika; Akanitoa katika maji mengi; Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia; Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu; Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea kulingana na haki yangu; Kulingana na usafi wa mikono yangu akanilipa. Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. Maana hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu; Na kuhusu amri zake, sikuziacha. Nami nilikuwa mkamilifu kwake, Nikajilinda na uovu wangu. Basi BWANA amenilipa kulingana na haki yangu; Kulingana na usafi wa mikono yangu mbele zake.
2 Samueli 22:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake zote, na mkononi mwa Sauli; akasema, BWANA ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu; Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio yangu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri. Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu. Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita BWANA, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu; Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasuka-suka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala; Makaa yakawashwa nao. Aliziinamisha mbingu akashuka; Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. Akapanda juu ya kerubi akaruka; Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo. Akafanya giza hema zake za kumzunguka, Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni. Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Makaa ya moto yakawashwa. BWANA alipiga radi toka mbinguni, Naye Aliye juu akaitoa sauti yake. Akapiga mishale, akawatawanya; Umeme, naye akawatapanya. Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Kwa kukemea kwake BWANA, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake. Alipeleka kutoka juu, akanishika; Akanitoa katika maji mengi; Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia; Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu; Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa. Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi Mungu wangu. Maana hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu; Na kwa habari za amri zake, sikuziacha. Nami nalikuwa mkamilifu kwake, Nikajilinda na uovu wangu. Basi BWANA amenilipa sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.
2 Samueli 22:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Daudi alimwimbia BWANA maneno ya wimbo huu BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Akasema: “BWANA ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, Mungu wangu ni mwamba wangu, ninayemkimbilia, ngao yangu na pembe ya wokovu wangu. Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu na mwokozi wangu, huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri. “Ninamwita BWANA, anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu. Mawimbi ya mauti yalinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea. Kamba za Kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili. “Katika shida yangu nalimwita BWANA, nilimlilia Mungu wangu. Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika masikioni mwake. Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya mbingu ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika. Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yaliyowaka yakatoka ndani yake. Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake. Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mabawa ya upepo. Alifanya giza hema lake la kujifunika: mawingu meusi ya mvua ya angani. Kutokana na mwanga wa uwepo wake mwanga wa radi ukatoka. BWANA alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika. Aliipiga mishale na kutawanya adui, akawafukuza kwa umeme mkubwa wa radi. Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwake BWANA, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake. “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu. Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi. Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini BWANA alikuwa msaada wangu. Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami. “BWANA alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa. Kwa maana nimezishika njia za BWANA; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu. Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake. Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi. BWANA amenilipa sawasawa na uadilifu wangu, sawasawa na usafi wangu machoni pake.