2 Samueli 20:1-24
2 Samueli 20:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa ikawa kwamba huko Gilgali kulikuwa na mtu mmoja mlaghai aitwaye Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini. Basi Sheba alipiga tarumbeta, na kusema, “Hatuna fungu lolote kwa Daudi, hatuna sehemu yetu katika huyo mwana wa Yese. Enyi watu wa Israeli, kila mmoja na ajiendee hemani kwake!” Hivyo, watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi, wakamfuata Sheba mwana wa Bikri. Lakini watu wa Yuda walimfuata mfalme Daudi kwa uaminifu toka mto Yordani mpaka mjini Yerusalemu. Hatimaye, Daudi aliwasili nyumbani kwake mjini Yerusalemu. Mfalme aliwachukua masuria wake kumi ambao alikuwa amewaacha kuangalia nyumba yake, akawaweka kwenye nyumba moja chini ya ulinzi, akawatunza vizuri, lakini hakulala nao. Hivyo, masuria hao wakawa wametiwa ndani hadi siku za kufa kwao, wakaishi kana kwamba, walikuwa wajane. Kisha, mfalme akamwambia Amasa, “Nikusanyie watu wote wa Yuda katika siku tatu, na wewe mwenyewe uwepo.” Basi, Amasa akaenda kuwaita watu wa Yuda. Lakini akachelewa kurudi katika wakati ule aliopangiwa na mfalme. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa, Sheba mwana wa Bikri, atatuletea madhara kuliko Absalomu. Chukua watumishi wangu, umfuatie Sheba asije akaingia kwenye miji yenye ngome akaponyoka, tusimwone tena.” Abishai akatoka akiwa pamoja na Yoabu, Wakerethi na Wapelethi pamoja na mashujaa wote. Hao wote waliondoka Yerusalemu kwenda kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. Walipofika kwenye jiwe kubwa lililoko huko Gibeoni, Amasa akatoka kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa vazi la kijeshi, na ndani ya vazi hilo kulikuwa na mkanda ulioshikilia upanga kiunoni mwake ukiwa kwenye ala yake. Yoabu alipokuwa anakaribia, upanga wake ulichomoka alani ukaanguka chini. Yoabu akamwambia Amasa, “Je, hujambo ndugu yangu?” Yoabu akamshika Amasa kidevuni kwa mkono wa kulia kana kwamba anataka kumbusu. Lakini Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu. Basi, Yoabu akamchoma Amasa upanga tumboni, matumbo yake yakatoka nje, akafa. Yoabu hakumchoma upanga mara mbili. Kisha, Yoabu na nduguye Abishai wakaendelea kumfuatilia Sheba mwana wa Bikri. Mtu mmoja wa Yoabu akaja akasimama karibu na mwili wa Amasa, akasema, “Yeyote anayempenda Yoabu na yeyote anayempenda Daudi, na amfuate Yoabu!” Amasa alikuwa bado anagagaa kwenye damu yake katikati ya barabara kuu. Kwa hiyo, kila mtu aliyepita hapo, alipomwona, alisimama. Lakini yule mtu alipoona kwamba watu wote walikuja na kusimama hapo, aliuondoa mwili wa Amasa barabarani, akaupeleka shambani na kuufunika kwa nguo. Amasa alipoondolewa kwenye barabara kuu, watu wote sasa waliendelea kumfuata Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. Sheba alipitia katika makabila yote ya Israeli mpaka mji wa Abeli wa Beth-maaka. Watu wote wa ukoo wa Bikri wakakusanyika na kumfuata. Watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakaenda kumzingira Sheba akiwa katika mji huo wa Abeli wa Beth-maaka. Walirundika kuuzingira mji, na ngome; halafu wakaanza kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini. Kisha, mwanamke fulani mwenye hekima alisikika kutoka mjini akisema, “Sikieni! Sikieni! Mwambieni Yoabu aje nizungumze naye.” Yoabu akaenda karibu naye, huyo mwanamke akamwambia, “Je, wewe ni Yoabu?” Yoabu akasema, “Naam! Ni mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Nisikilize mimi mtumishi wako.” Yoabu akamwambia, “Nasikiliza.” Huyo mwanamke akamwambia, “Hapo kale watu walikuwa wakisema, ‘Waacheni watake shauri kutoka mji wa Abeli’. Ndivyo watu walivyoweza kutatua matatizo. Mimi ni mmojawapo wa wale wanaopenda amani na uaminifu katika Israeli. Sasa wewe unakusudia kuuharibu mji ambao ni kama mama katika Israeli. Kwa nini sasa unataka kuuangamiza mji ulio mali yake Mwenyezi-Mungu?” Yoabu akamjibu, “Kamwe maishani mwangu! Sina nia kuangamiza wala kuharibu. Ulivyosema si kweli! Lakini mtu mmoja kutoka sehemu ya milima ya Efraimu aitwaye Sheba mwana wa Bikri anataka kumwasi mfalme Daudi. Mtoeni huyo kwangu nami nitaondoka mjini kwenu.” Yule mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake kitarushwa kwako kupitia ukutani.” Kisha, huyo mwanamke akaenda kwa watu wote mjini kwa busara yake. Wakamkata kichwa Sheba mwana wa Bikri, wakakitupa nje kwa Yoabu. Kwa hiyo, Yoabu akapiga tarumbeta, na kuwatawanya watu wake kutoka mji huo wa Abeli; kila mtu akaenda nyumbani kwake. Kisha Yoabu akarudi kwa mfalme Daudi, mjini Yerusalemu. Sasa Yoabu alikuwa mkuu wa jeshi lote la Israeli. Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi. Adoramu alikuwa msimamizi wa kazi za kulazimishwa; Yehoshafati alikuwa mwandishi wa kumbukumbu.
2 Samueli 20:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ilitukia ya kwamba kulikuwapo mtu asiyefaa, jina lake akiitwa Sheba, mwana wa Bikri, Mbenyamini; naye akapiga tarumbeta, akasema, Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni kila mtu hemani kwake, enyi Israeli. Basi wakapanda watu wote wa Israeli kutoka kumfuata Daudi, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri; lakini watu wa Yuda wakaambatana na mfalme wao, toka Yordani hadi Yerusalemu. Basi Daudi akaja Yerusalemu nyumbani kwake; kisha mfalme akawatwaa wale wanawake kumi, masuria, aliowaacha kuitunza nyumba, akawatia nyumbani mwa kulindwa, akawalisha, ila asiingie kwao. Basi wakafungwa hadi siku ya kufa kwao, huku wakiishi hali ya ujane. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa. Amasa akaenda kuwakusanya watu wa Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa. Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kutuponyoka. Ndipo wakatoka nyuma yake watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, na mashujaa wote; wakatoka Yerusalemu, ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akienda, ukaanguka. Naye Yoabu akamwambia Amasa, Amani kwako, ndugu yangu. Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kulia ili ambusu. Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao tumboni, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri. Akasimama karibu naye mmoja wa vijana wa Yoabu, huyo akasema, Ampendaye Yoabu, na aliye wa Daudi, na amfuate Yoabu. Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya njia kuu. Basi yule mtu alipowaona watu wote wamesimama, akamwondoa Amasa toka njia kuu akamtia kondeni, akamfunika nguo, hapo alipoona ya kuwa kila mtu aliyefika kwake amesimama. Na alipoondolewa katika njia kuu, watu wote wakapita, wakamwandama Yoabu ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Naye akapita kati ya kabila zote za Israeli mpaka Abeli, na kwa Bethmaaka na Wabikri wote; nao wakakusanyika, wakaenda pia kumwandama. Na hao wakaja wakauzingira katika Abeli wa Bethmaaka, wakafanya kilima mbele ya mji, nacho kikasimama kuielekea ngome; na watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakavunjavunja ukuta, wapate kuubomoa. Ndipo akalia mwanamke mmoja mwenye hekima toka mjini, Sikieni, sikieni; mwambieni na Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye. Basi akamkaribia; na yule mwanamke akasema, Ndiwe Yoabu? Akajibu, Ndimi. Ndipo akamwambia Sikia maneno ya mjakazi wako. Akajibu, Mimi nasikia. Kisha akanena, akisema, Watu hunena zamani za kale, wakisema, Wasikose kuuliza huko Abeli; ndivyo walivyoleta suluhu. Mimi ni mmoja wa hao wenye amani, walio waaminifu katika Israeli; wewe unataka kuuharibu mji ulio kama mama wa Israeli; mbona unataka kuumeza urithi wa BWANA? Yoabu akajibu, akasema, Isiwe, isiwe kwangu, niumeze wala kuuharibu. Neno hili silo hivyo; lakini mtu mmoja wa milima ya Efraimu, jina lake, Sheba, mwana wa Bikri, ameinua mkono wake juu ya mfalme, naam, Daudi, basi mtoeni yeye tu, nami nitaondoka katika mji huu. Basi yule mwanamke akamwambia Yoabu, Tazama, kichwa chake utatupiwa juu ya ukuta. Ndipo yule mwanamke akawaendea watu wote katika hekima yake. Nao wakamkata kichwa Sheba, mwana wa Bikri, wakamtupia Yoabu huko nje. Ndipo akapiga tarumbeta, nao wakatawanyika kutoka mjini kila mtu hemani kwake. Naye Yoabu akarudi mpaka Yerusalemu kwa mfalme. Basi Yoabu alikuwa akiongoza jeshi lote la Israeli; na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa akiwaongoza Wakerethi, na Wapelethi; na Adoramu alikuwa akiwaongoza Shokoa; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mwekaji kumbukumbu
2 Samueli 20:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ilitukia ya kwamba kulikuwapo mtu asiyefaa, jina lake akiitwa Sheba, mwana wa Bikri, Mbenyamini; naye akapiga tarumbeta, akasema, Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni kila mtu hemani kwake, enyi Israeli. Basi wakapanda watu wote wa Israeli kutoka kumfuata Daudi, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri; lakini watu wa Yuda wakaambatana na mfalme wao, toka Yordani hata kufika Yerusalemu. Basi Daudi akaja Yerusalemu nyumbani kwake; kisha mfalme akawatwaa wale wanawake kumi, masuria, aliowaacha kuitunza nyumba, akawatia nyumbani mwa kulindwa, akawalisha, ila asiingie kwao. Basi wakafungwa hata siku ya kufa kwao, huku wakiishi hali ya ujane. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa. Amasa akaenda kuwakusanya Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa. Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kujiponya machoni petu. Ndipo wakatoka nyuma yake watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, na mashujaa wote; wakatoka Yerusalemu, ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akiendelea, ukaanguka. Naye Yoabu akamwambia Amasa, Amani kwako, ndugu yangu. Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao wa tumbo, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri. Akasimama karibu naye mmojawapo wa vijana wa Yoabu, huyo akasema, Ampendaye Yoabu, na aliye wa Daudi, na amfuate Yoabu. Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya njia kuu. Basi yule mtu alipowaona watu wote wamesimama, akamwondoa Amasa toka njia kuu akamtia kondeni, akamfunika nguo, hapo alipoona ya kuwa kila mtu aliyefika kwake amesimama. Na alipoondolewa katika njia kuu, watu wote wakapita, wakamwandama Yoabu ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Naye akapita kati ya kabila zote za Israeli mpaka Abeli, na kwa Bethmaaka na Wabikri wote; nao wakakusanyika, wakaenda pia kumwandama. Na hao wakaja wakamhusuru katika Abeli wa Bethmaaka, wakafanya chuguu mbele ya mji, nayo ikasimama kuielekea ngome; na watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakavunja-vunja ukuta, wapate kuubomoa. Ndipo akalia mwanamke mmoja mwenye akili toka mjini, Sikieni, sikieni; mwambieni na Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye. Basi akamkaribia; na yule mwanamke akasema, Ndiwe Yoabu? Akajibu, Ndimi. Ndipo akamwambia Sikia maneno ya mjakazi wako. Akajibu, Mimi nasikia. Kisha akanena, akisema, Watu hunena zamani za kale, wakisema, Wasikose kuuliza huko Abeli; ndivyo walivyomaliza shauri. Mimi ni wa hao wenye amani, walio waaminifu katika Israeli; wewe unatafuta kuuharibu mji, na mama wa Israeli; mbona wataka kuumeza urithi wa BWANA? Yoabu akajibu, akasema, Isiwe, isiwe kwangu, niumeze wala kuuharibu. Neno hili silo hivyo; lakini mtu mmoja wa milima ya Efraimu, Sheba, mwana wa Bikri, jina lake, ameinua mkono wake juu ya mfalme, naam, Daudi, basi mtoeni yeye tu, nami nitaondoka katika mji huu. Basi yule mwanamke akamwambia Yoabu, Tazama, kichwa chake utatupiwa juu ya ukuta. Ndipo yule mwanamke akawaendea watu wote katika akili zake. Nao wakamkata kichwa Sheba, mwana wa Bikri, wakamtupia Yoabu huko nje. Ndipo akapiga tarumbeta, nao wakatawanyika kutoka mjini kila mtu hemani kwake. Naye Yoabu akarudi mpaka Yerusalemu kwa mfalme. Basi Yoabu alikuwa juu ya jeshi lote la Israeli; na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi, na juu ya Wapelethi; na Adoramu alikuwa juu ya shokoa; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mkumbushi
2 Samueli 20:1-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Hatuna fungu katika Daudi, wala hatuna sehemu katika mwana wa Yese! Kila mtu aende kwenye hema lake, enyi Israeli!” Kwa hiyo wanaume wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini wanaume wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani hadi Yerusalemu. Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kutunza jumba la kifalme, na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane hadi kifo chao. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite wanaume wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.” Lakini Amasa alipoenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara kuliko Absalomu. Wachukue watumishi wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.” Hivyo watumishi wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na mashujaa wenye nguvu wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri. Walipokuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kiunoni wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka ala. Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri. Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!” Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani hadi kwenye shamba na kutupia nguo juu yake. Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walikusanyika na kumfuata. Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumzingira Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wakijaribu kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini, mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.” Yoabu alienda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?” Akamjibu, “Ndiye mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.” Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri. Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa BWANA?” Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu. Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Mkabidhini mtu huyu mmoja kwangu, nami nitajiondoa katika mji huu.” Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.” Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani mwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu. Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa; Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu