Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 17:6-23

2 Samueli 17:6-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu alimwuliza, “Hivyo ndivyo alivyosema Ahithofeli. Je, tufanye kama alivyotushauri? Kama sivyo, basi, tuambie lako.” Hushai akamwambia Absalomu, “Wakati huu, shauri alilolitoa Ahithofeli si jema.” Zaidi ya hayo, Hushai akamwambia, “Wewe unajua kwamba baba yako na watu wake ni mashujaa na kwamba wamekasirishwa kama dubu jike nyikani aliyenyanganywa watoto wake. Mbali na hayo, unajua kwamba baba yako ni bingwa wa vita. Yeye hatakaa usiku kucha pamoja na watu wake. Hata sasa amekwisha jificha kwenye mojawapo ya mapango yaliyoko huko au mahali pengine. Mtu yeyote atakayesikia kuuawa kwa watu katika mashambulizi ya kwanza atasema kuwa mauaji yametokea katika kundi la wafuasi wa Absalomu. Watu wako watakaposikia hivyo, hata wale watu wako walio shupavu, wenye mioyo shupavu kama ya simba, watavunjika moyo kabisa kwa hofu. Maana, Waisraeli wote wanajua kuwa baba yako ni shujaa na wote walio pamoja naye ni watu hodari. Shauri langu ni kwamba, uwakusanye kwako watu wote wa Israeli tangu Dani hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wawe wengi kama mchanga wa bahari, na wewe mwenyewe binafsi uende vitani. Nasi tutamwendea Daudi mahali popote anapoweza kupatikana na tutamvamia kama umande unavyoiangukia ardhi. Basi, hakuna atakayesalia hata kama atakuwa yeye mwenyewe au watu wake wote walio pamoja naye. Iwapo atakimbilia mji fulani, basi, watu wote wa Israeli wataleta kamba na kuuburuta mji huo, hadi bondeni, kisibaki chochote hata jiwe dogo la mji huo.” Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai ni bora kuliko shauri la Ahithofeli.” Wakakataa shauri la Ahithofeli kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa amepanga kulishinda shauri jema la Ahithofeli ili aweze kumletea Absalomu maafa. Kisha Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari jinsi Ahithofeli na yeye mwenyewe walivyomshauri Absalomu na wazee wa Israeli. Akawaambia wampelekee Daudi habari upesi kwamba asilale usiku kwenye vivuko jangwani, bali, kwa njia yoyote ile, avuke na kuondoka ili asije akakamatwa na kuuawa, yeye pamoja na watu wake wote. Wakati huo, Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakimngojea karibu na Enrogeli, ili wasionekane na mtu yeyote wakiingia mjini. Kila mara mtumishi fulani wa kike alikuwa akiwapelekea habari nao wakaipeleka kwa mfalme Daudi. Lakini wakati huu, walionekana na kijana mmoja ambaye alikwenda na kumhabarisha Absalomu. Hivyo, Yonathani na Ahimaasi waliondoka haraka, wakaenda Bahurimu nyumbani kwa mtu fulani aliyekuwa na kisima uani kwake. Wakaingia humo kisimani na kujificha. Mwanamke mwenye nyumba hiyo akachukua kifuniko na kukifunika kisima hicho, halafu akaanika nafaka juu ya kifuniko. Habari hizo hazikujulikana. Watumishi wa Absalomu walipowasili kwa huyo mwanamke, wakamwambia, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Yule mwanamke akawaambia, “Wamekwenda ngambo ya kijito.” Walipowatafuta na kuwakosa, wakarudi mjini Yerusalemu. Baada ya watumishi wa Absalomu kuondoka, Yonathani na Ahimaasi walitoka kisimani, wakaenda kwa mfalme Daudi na kumpasha habari. Wakamwambia, “Ondoka, uende ngambo ya mto, kwa sababu Ahithofeli amemshauri Absalomu dhidi yako.” Kwa hiyo, Daudi akaondoka na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakavuka mto Yordani. Ilipofika asubuhi hakuna mtu aliyebaki nyuma bila kuvuka mto Yordani. Ahithofeli alipoona kwamba shauri lake halikufuatwa, alitandika punda wake, akaenda nyumbani, kwenye mji wake. Alipofika huko, alipanga vizuri mambo ya nyumbani kwake, akajinyonga. Akafariki na kuzikwa kwenye kaburi la baba yake.

2 Samueli 17:6-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako. Hushai akamwambia Absalomu, Ushauri huu alioutoa Ahithofeli si mwema wakati huu. Hushai akaendelea kusema, Unamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake. Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna mauaji katika watu wanaofuatana na Absalomu. Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe. Hivyo tutamfikia mahali popote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye. Tena, ikiwa amejitia katika mji wowote ule, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ushauri wa Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kuuvunja ushauri mwema wa Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu. Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha. Basi sasa pelekeni habari upesi, kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye. Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; ndipo wakamwambie mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini. Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake. Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lolote. Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu. Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu. Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki hata mmoja wao asiyevuka Yordani. Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa ushauri wake haukufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajinyonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye.

2 Samueli 17:6-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako. Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu. Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake. Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu. Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe. Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye. Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu. Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha. Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye. Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini. Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake. Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lo lote. Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu. Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu. Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki mmojawapo wao asiyevuka Yordani. Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye.

2 Samueli 17:6-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hushai alipokuja, Absalomu akasema, “Ahithofeli ametoa ushauri huu. Je, tufanye anavyosema? Kama sivyo, tupe maoni yako.” Hushai akamjibu Absalomu, “Ushauri alioutoa Ahithofeli haufai kwa wakati huu. Unamfahamu baba yako na watu wake, ni wapiganaji hodari, nao ni wakali kama dubu aliyepokonywa watoto wake. Zaidi ya hayo, baba yako ni mpiganaji jasiri, usiku hatalala pamoja na vikosi. Hata sasa, amefichwa ndani ya pango au mahali pengine. Kama atatangulia kushambulia vikosi vyako, yeyote asikiaye habari hii atasema, ‘Kuna machinjo makubwa miongoni mwa vikosi vinavyomfuata Absalomu.’ Basi hata yule askari hodari kuliko wengine wote, ambaye moyo wake ni kama wa simba, atayeyuka kwa hofu, kwa maana Israeli yote wanajua kwamba baba yako ni mpiganaji na kwamba wale walio pamoja naye ni watu hodari. “Kwa hiyo nakushauri: Israeli wote na wakusanyike kwako, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, wakiwa wengi kama mchanga wa ufuo wa bahari; wakusanyike kwako, nawe ukiwaongoza vitani. Ndipo tutakapomshambulia popote atakapoonekana, nasi tutamwangukia kama umande unavyoshuka juu ya ardhi. Yeye mwenyewe na watu wake hakuna atakayeachwa hai. Kama atakimbilia katika mji wowote, basi Israeli wote watazungushia mji ule kamba, nasi tutauburuta mji huo hadi bondeni, wala isionekane hata changarawe ya huo mji.” Absalomu na wanaume wote wa Israeli wakasema, “Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ule wa Ahithofeli.” Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kupinga ushauri mwema wa Ahithofeli, ili kuleta maafa kwa Absalomu. Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari, “Ahithofeli amemshauri Absalomu na wazee wa Israeli kufanya hivi na hivi, lakini mimi nimewashauri wao kufanya lile na lile. Sasa tumeni ujumbe haraka na kumwambia Daudi, ‘Usiku huu usilale kwenye vivuko katika jangwa; vuka bila kukosa, la sivyo, mfalme pamoja na watu wote waliofuatana naye watamezwa.’ ” Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakingoja huko En-Rogeli. Naye mjakazi mmoja alipaswa kuwapasha habari nao wakawa waende kumwambia Mfalme Daudi, kwa maana wasingetaka kujihatarisha kuonekana wakiingia mjini. Lakini kijana mmoja mwanaume akawaona, naye akamwambia Absalomu. Basi wote wawili wakaondoka haraka, wakaenda hadi kwenye nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu. Mtu huyo alikuwa na kisima uani mwake, nao Yonathani na Ahimaasi wakateremka ndani ya kisima hicho. Mkewe akachukua kifuniko, akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima na kuanika nafaka juu yake. Hakuna mtu yeyote aliyefahamu chochote kuhusu jambo hilo. Watu wa Absalomu walipofika kwa huyo mwanamke, wakamuuliza, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?” Huyo mwanamke akawajibu, “Walivuka kijito.” Watu wa Absalomu wakapekua lakini hawakuwaona hata mmoja, hivyo wakarudi Yerusalemu. Baada ya watu hao kuondoka, wale watu wawili yaani Yonathani na Ahimaasi wakapanda kutoka mle kisimani na kwenda kumpasha Mfalme Daudi habari. Wakamwambia, “Ondoka, uvuke mto haraka. Ahithofeli ameshauri hivi na hivi dhidi yako.” Kwa hiyo Daudi na watu wote aliokuwa nao waliondoka na kuvuka Yordani. Kufika wakati wa mapambazuko, hapakuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa hajavuka Mto Yordani. Ahithofeli alipoona kwamba ushauri wake haukufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani mwake kwenye mji wake. Akaiweka nyumba yake katika utaratibu, kisha akajinyonga mwenyewe. Hivyo akafa na akazikwa katika kaburi la baba yake.