Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 17:1-14

2 Samueli 17:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Zaidi ya Hayo, Ahithofeli alimwambia Absalomu, “Niruhusu nichague watu 12,000, niondoke na kumfuatia Daudi leo usiku. Nitamshambulia akiwa amechoka na amevunjika moyo, nami nitamtia wasiwasi. Watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake, na kuwarudisha watu wengine wote kwako kama bibiarusi anavyokwenda nyumbani kwa mumewe. Wewe unayatafuta maisha ya mtu mmoja tu; na watu wengine watakuwa na amani.” Shauri hilo la Ahithofeli lilimpendeza Absalomu na wazee wote wa Israeli. Kisha, Absalomu akasema, “Mwiteni Hushai pia, yule mtu wa Arki, tusikie analotaka kusema.” Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu alimwuliza, “Hivyo ndivyo alivyosema Ahithofeli. Je, tufanye kama alivyotushauri? Kama sivyo, basi, tuambie lako.” Hushai akamwambia Absalomu, “Wakati huu, shauri alilolitoa Ahithofeli si jema.” Zaidi ya hayo, Hushai akamwambia, “Wewe unajua kwamba baba yako na watu wake ni mashujaa na kwamba wamekasirishwa kama dubu jike nyikani aliyenyanganywa watoto wake. Mbali na hayo, unajua kwamba baba yako ni bingwa wa vita. Yeye hatakaa usiku kucha pamoja na watu wake. Hata sasa amekwisha jificha kwenye mojawapo ya mapango yaliyoko huko au mahali pengine. Mtu yeyote atakayesikia kuuawa kwa watu katika mashambulizi ya kwanza atasema kuwa mauaji yametokea katika kundi la wafuasi wa Absalomu. Watu wako watakaposikia hivyo, hata wale watu wako walio shupavu, wenye mioyo shupavu kama ya simba, watavunjika moyo kabisa kwa hofu. Maana, Waisraeli wote wanajua kuwa baba yako ni shujaa na wote walio pamoja naye ni watu hodari. Shauri langu ni kwamba, uwakusanye kwako watu wote wa Israeli tangu Dani hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wawe wengi kama mchanga wa bahari, na wewe mwenyewe binafsi uende vitani. Nasi tutamwendea Daudi mahali popote anapoweza kupatikana na tutamvamia kama umande unavyoiangukia ardhi. Basi, hakuna atakayesalia hata kama atakuwa yeye mwenyewe au watu wake wote walio pamoja naye. Iwapo atakimbilia mji fulani, basi, watu wote wa Israeli wataleta kamba na kuuburuta mji huo, hadi bondeni, kisibaki chochote hata jiwe dogo la mji huo.” Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai ni bora kuliko shauri la Ahithofeli.” Wakakataa shauri la Ahithofeli kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa amepanga kulishinda shauri jema la Ahithofeli ili aweze kumletea Absalomu maafa.

2 Samueli 17:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu elfu kumi na mbili, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejesha kwako; kama bibi arusi anavyorudi nyumbani kwa mumewe. Kurudi kwa yule mtu umtafutaye ni kana kurudi kwa wote; maana watu wote watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli. Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia. Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako. Hushai akamwambia Absalomu, Ushauri huu alioutoa Ahithofeli si mwema wakati huu. Hushai akaendelea kusema, Unamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake. Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna mauaji katika watu wanaofuatana na Absalomu. Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe. Hivyo tutamfikia mahali popote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye. Tena, ikiwa amejitia katika mji wowote ule, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ushauri wa Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kuuvunja ushauri mwema wa Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu.

2 Samueli 17:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli. Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia. Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako. Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu. Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake. Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu. Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe. Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye. Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu.

2 Samueli 17:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Nipe ruhusa niwachague watu elfu kumi na mbili, nao waanze safari usiku huu huu kumfuatia Daudi. Nitamshambulia wakati akiwa amechoka na ni dhaifu. Nitampiga na hofu, na kisha watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake na kuwarudisha watu wote kwako. Kifo cha mtu yule unayemtafuta kitamaanisha kurudi kwa wote, hakuna hata mtu mmoja atakayeumizwa.” Mpango huu ulionekana mzuri kwa Absalomu na kwa wazee wote wa Israeli. Lakini Absalomu akasema, “Pia mwiteni Hushai, Mwarki, ili tuweze kusikia anachokisema.” Hushai alipokuja, Absalomu akasema, “Ahithofeli ametoa ushauri huu. Je, tufanye anavyosema? Kama sivyo, tupe maoni yako.” Hushai akamjibu Absalomu, “Ushauri alioutoa Ahithofeli haufai kwa wakati huu. Unamfahamu baba yako na watu wake, ni wapiganaji hodari, nao ni wakali kama dubu aliyepokonywa watoto wake. Zaidi ya hayo, baba yako ni mpiganaji jasiri, usiku hatalala pamoja na vikosi. Hata sasa, amefichwa ndani ya pango au mahali pengine. Kama atatangulia kushambulia vikosi vyako, yeyote asikiaye habari hii atasema, ‘Kuna machinjo makubwa miongoni mwa vikosi vinavyomfuata Absalomu.’ Basi hata yule askari hodari kuliko wengine wote, ambaye moyo wake ni kama wa simba, atayeyuka kwa hofu, kwa maana Israeli yote wanajua kwamba baba yako ni mpiganaji na kwamba wale walio pamoja naye ni watu hodari. “Kwa hiyo nakushauri: Israeli wote na wakusanyike kwako, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, wakiwa wengi kama mchanga wa ufuo wa bahari; wakusanyike kwako, nawe ukiwaongoza vitani. Ndipo tutakapomshambulia popote atakapoonekana, nasi tutamwangukia kama umande unavyoshuka juu ya ardhi. Yeye mwenyewe na watu wake hakuna atakayeachwa hai. Kama atakimbilia katika mji wowote, basi Israeli wote watazungushia mji ule kamba, nasi tutauburuta mji huo hadi bondeni, wala isionekane hata changarawe ya huo mji.” Absalomu na wanaume wote wa Israeli wakasema, “Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ule wa Ahithofeli.” Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kupinga ushauri mwema wa Ahithofeli, ili kuleta maafa kwa Absalomu.