2 Samueli 13:30-34
2 Samueli 13:30-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Walipokuwa bado njiani, Daudi alipata habari kuwa Absalomu amewaua watoto wake wote hakuna hata mmoja aliyesalia. Mfalme Daudi aliinuka, akararua mavazi yake kwa huzuni akalala chini. Hata na watumishi wake wote waliokuwa wamesimama karibu naye walirarua mavazi yao. Lakini Yonadabu, mwana wa Shimea, ndugu ya Daudi akamwambia, “Bwana wangu, usifikiri kuwa wanao wote wameuawa. Amnoni pekee ndiye aliyeuawa. Haya Absalomu aliyakusudia kuyafanya tangu wakati ule Amnoni alipomshika kwa nguvu dada yake Tamari na kulala naye. Hivyo, bwana wangu, usifikiri moyoni mwako kwamba watoto wako wote wamekufa. Ni Amnoni pekee ndiye aliyeuawa.” Lakini Absalomu alikuwa amekwisha kimbia. Naye kijana aliyekuwa na zamu ya ulinzi, mara akaona kundi kubwa la watu wanakuja kutokea mlimani katika barabara ya kutoka Horonaimu.
2 Samueli 13:30-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamfikia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, nguo zao zikiwa zimeraruliwa. Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ni Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipomshika kwa nguvu dada yake, Tamari. Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa. Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake.
2 Samueli 13:30-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, wenye nguo zao zimeraruliwa. Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ndiye Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipotenzwa nguvu umbu lake, Tamari. Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa. Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake.
2 Samueli 13:30-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakiwa njiani, taarifa ilimjia Daudi, kusema: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme; hakuna hata mmoja aliyesalia.” Mfalme akasimama, akararua nguo zake, akalala chini ardhini; nao watumishi wake wote wakasimama kando yake na nguo zao zikiwa zimeraruliwa. Lakini Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akasema, “Bwana wangu asifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme; ni Amnoni peke yake ndiye alikufa. Hili limekuwa kusudi la moyo wa Absalomu tangu siku ile Amnoni alipomtendea jeuri Tamari, dada yake. Mfalme bwana wangu asisumbuliwe na taarifa kwamba wamewaua wana wote wa mfalme. Ni Amnoni peke yake aliyekufa.” Wakati huo, Absalomu akawa amekimbia. Basi mlinzi akaangalia, naye akaona watu wengi barabarani magharibi yake, wakishuka kutoka upande wa kilima. Mlinzi akaenda akamwambia mfalme, “Naona watu wakitokea upande wa Horonaimu, huko upande wa kilimani.”