2 Samueli 13:1-39
2 Samueli 13:1-39 Biblia Habari Njema (BHN)
Absalomu, alikuwa na dada yake mzuri aliyeitwa Tamari. Muda si muda, Amnoni, mtoto mwingine wa kiume wa Daudi, akampenda sana Tamari. Amnoni aliteseka sana hata akajifanya mgonjwa kwa sababu ya dada yake Tamari hasa kwa vile Tamari alikuwa bikira, na ilionekana jambo lisilowezekana kwa Amnoni kufanya chochote naye. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki aliyeitwa Yonadabu, mtoto wa Shama, ndugu ya Daudi. Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. Yonadabu akamwambia Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme, kwa nini unakonda na unaonekana huna furaha kila siku? Mbona hutaki kuniambia.” Amnoni akamwambia, “Nampenda Tamari, dada ya ndugu yangu Absalomu.” Yonadabu akamwambia, “Wewe jilaze kitandani ukidai kuwa u mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona, wewe msihi ukisema, ‘Mruhusu dada yangu, Tamari, aje aniletee mkate nipate kula na aniandalie chakula mbele yangu ili nikione naye mwenyewe anilishe.’” Hivyo, Amnoni akaendelea kulala kitandani, akijifanya mgonjwa. Mfalme alipokwenda kumwona, Amnoni alimwambia, “Nakuomba, Tamari aje hapa anitengenezee mikate michache huku nikimwangalia. Halafu yeye mwenyewe anilishe.” Hivyo, Daudi alipeleka ujumbe kwa Tamari kwamba aende nyumbani kwa kaka yake Amnoni, akamtengenezee chakula. Tamari alikwenda huko, akamkuta Amnoni amelala. Akachukua unga, akaukanda, na kuoka mikate mbele ya Amnoni. Mikate hiyo ilipokuwa tayari, Tamari akaiopoa kutoka kikaangoni. Akampelekea Amnoni, lakini Amnoni alikataa kula, akasema kila mmoja na atolewe nje, na wote wakaondoka. Kisha, Amnoni akamwambia Tamari, “Sasa niletee mikate hiyo chumbani kwangu, halafu unilishe.” Tamari aliichukua mikate aliyoiandaa na kuipeleka chumbani kwa kaka yake Amnoni. Hapo, alipokuwa anampatia mikate hiyo, Amnoni alimkamata na kumwambia, “Njoo ulale nami.” Tamari akamwambia, “Sivyo, kaka yangu, usinilazimishe. Kitendo hiki hakifanyiki katika Israeli. Usifanye kitendo hiki cha kipumbavu. Kwa upande wangu, siwezi kuvumilia aibu hiyo. Na kwa upande wako, utakuwa mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, mimi nakusihi uzungumze na mfalme kwani hatakukataza kunioa.” Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza na kwa kuwa alimzidi nguvu, alimlazimisha, akalala naye. Kisha, Amnoni akamchukia Tamari kupita kiasi. Akamchukia Tamari kuliko alivyompenda hapo awali. Akamwambia Tamari, “Ondoka mara moja.” Tamari akamjibu, “Sivyo kaka yangu; ovu hili kubwa la kunifukuza ni baya zaidi kuliko lile ulilonitendea.” Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza. Akamwita kijana wake aliyemtumikia, akamwambia, “Mtoe mwanamke huyu mbele yangu. Na mlango uufunge kwa komeo.” Amnoni na yule kijana wakamtoa nje na kuufunga mlango kwa komeo. Tamari alikuwa amevaa vazi refu lenye mikono mirefu kwani hivyo ndivyo walivyovaa mabikira wa mfalme zamani hizo. Basi, Tamari alijipaka majivu kichwani, akalipasua vazi lake, akaweka mikono yake kichwani, halafu akaondoka huku analia kwa sauti. Kaka yake, Absalomu, alipomwona, alimwuliza, “Je, Amnoni kaka yako amelala nawe? Tulia dada yangu. Yeye ni kaka yako. Usilitie jambo hilo moyoni mwako.” Hivyo, Tamari aliishi katika nyumba ya Absalomu akiwa na huzuni na mpweke. Mfalme Daudi aliposikia jambo hilo alikasirika sana. Absalomu alimchukia Amnoni sana hata hakusema naye, kwa sababu alimshika kwa nguvu dada yake Tamari akalala naye. Baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na shughuli ya kuwakata kondoo wake manyoya mjini Baal-hasori, karibu na Efraimu. Akawaalika watoto wote wa kiume wa mfalme. Absalomu alimwendea mfalme Daudi, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako ninao wakata-kondoo manyoya. Nakuomba wewe mfalme pamoja na watumishi wako, mwende pamoja nami, mtumishi wako.” Mfalme akamjibu, “Sivyo, mwanangu, tusiende wote; tusije tukawa mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alizidi kumsihi baba yake aende, lakini mfalme alikataa, ila alimpa baraka zake. Halafu, Absalomu akamwambia, “Kama huendi, basi, mruhusu ndugu yangu Amnoni twende naye.” Mfalme akamjibu, “Lakini kwa nini aende pamoja nanyi?” Lakini Absalomu alizidi kumsihi, na mwishowe mfalme akamruhusu Amnoni na wanawe wengine waende kwenye sherehe hiyo. Absalomu akawaambia watumishi wake, “Mwangalieni Amnoni atakapokuwa amekunywa divai na kufurahi. Nitakapowaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ muueni. Hiyo ni amri yangu kwenu. Jipeni moyo na muwe hodari.” Hivyo, watumishi wa Absalomu walimtendea Amnoni kama walivyoamriwa na Absalomu, kisha wana wa kiume wengine wa mfalme wakaondoka kila mmoja akapanda nyumbu wake na kukimbia. Walipokuwa bado njiani, Daudi alipata habari kuwa Absalomu amewaua watoto wake wote hakuna hata mmoja aliyesalia. Mfalme Daudi aliinuka, akararua mavazi yake kwa huzuni akalala chini. Hata na watumishi wake wote waliokuwa wamesimama karibu naye walirarua mavazi yao. Lakini Yonadabu, mwana wa Shimea, ndugu ya Daudi akamwambia, “Bwana wangu, usifikiri kuwa wanao wote wameuawa. Amnoni pekee ndiye aliyeuawa. Haya Absalomu aliyakusudia kuyafanya tangu wakati ule Amnoni alipomshika kwa nguvu dada yake Tamari na kulala naye. Hivyo, bwana wangu, usifikiri moyoni mwako kwamba watoto wako wote wamekufa. Ni Amnoni pekee ndiye aliyeuawa.” Lakini Absalomu alikuwa amekwisha kimbia. Naye kijana aliyekuwa na zamu ya ulinzi, mara akaona kundi kubwa la watu wanakuja kutokea mlimani katika barabara ya kutoka Horonaimu. Yonadabu akamwambia Daudi, “Tazama mfalme, wanao wanakuja kama nilivyokuambia mimi mtumishi wako.” Mara tu yule mtumishi alipomaliza kusema, wana wa kiume wa mfalme wakaingia, wakaanza kulia kwa sauti. Mfalme na watumishi wake wote, wakalia kwa uchungu. Lakini Absalomu alikimbilia kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa mji wa Geshuri. Mfalme Daudi akamwombolezea mwanawe Amnoni kwa siku nyingi. Absalomu alikimbilia mjini Geshuri, akakaa huko kwa muda wa miaka mitatu. Baada ya mfalme Daudi kutulia kutokana na kifo cha Amnoni, alianza kutamani kumwona mwanawe Absalomu.
2 Samueli 13:1-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na dada yake mzuri, aliyeitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya yule dada yake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lolote. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, dada ya kaka yangu, Absalomu. Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake. Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake. Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula. Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate. Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Ndipo watu wote wakaondoka. Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoiandaa, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, dada yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinilazimishe; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Lakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamlazimisha, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunifukuza ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamtoa nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti. Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu. Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana. Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumlazimisha dada yake Tamari. Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme. Absalomu akamjia mfalme, akasema, Tazama sasa, mimi mtumishi wako ninao wakata manyoya ya kondoo; basi mfalme na aende, nakusihi, na watumishi wake pamoja nami mtumishi wako. Mfalme akamwambia Absalomu, Sivyo, mwanangu, tusiende sote, tusije tukakulemea. Akamsihi sana; asikubali kwenda, ila akambariki. Ndipo akasema Absalomu, Kama huji, nakusihi, mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi. Mfalme akamwambia, Kwa nini aende nawe? Lakini Absalomu akamsihi sana, naye akamwacha Amnoni na wana wote wa mfalme waende naye. Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, kisha mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, na wenye ujasiri. Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia. Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamfikia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, nguo zao zikiwa zimeraruliwa. Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ni Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipomshika kwa nguvu dada yake, Tamari. Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa. Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake. Ndipo Yonadabu akamwambia mfalme, Tazama, wana wa mfalme wamekuja; kama mimi mtumishi wako nilivyosema, ndivyo ilivyo. Ikawa alipokwisha kusema, tazama, wana wa mfalme walikuja, nao wakapaza sauti zao wakalia; mfalme naye akalia, na watumishi wake wote, kilio kikubwa mno. Lakini Absalomu akakimbia, akamwendea Talmai, mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Naye Daudi akamlilia mwanawe kila siku. Basi Absalomu akakimbia, akaenda Geshuri, akakaa huko muda wa miaka mitatu. Mfalme Daudi akatamani kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa.
2 Samueli 13:1-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, umbu la ndugu yangu, Absalomu. Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake. Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake. Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula. Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate. Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Wakatoka kila mtu kwake. Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti. Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu. Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana. Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari. Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme. Absalomu akamjia mfalme, akasema, Tazama sasa, mimi mtumwa wako ninao wakata manyoya ya kondoo; basi mfalme na aende, nakusihi, na watumishi wake pamoja nami mtumwa wako. Mfalme akamwambia Absalomu, Sivyo, mwanangu, tusiende sote, tusije tukakulemea. Akamsihi sana; asikubali kwenda, ila akambariki. Ndipo akasema Absalomu, Kwamba huji, nakusihi, mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi. Mfalme akamwambia, Kwa nini aende nawe? Lakini Absalomu akamsihi sana, naye akamwacha Amnoni na wana wote wa mfalme waende naye. Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri. Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia. Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, wenye nguo zao zimeraruliwa. Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ndiye Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipotenzwa nguvu umbu lake, Tamari. Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa. Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake. Ndipo Yonadabu akamwambia mfalme, Tazama, wana wa mfalme wamekuja; kama mimi mtumwa wako nilivyosema, ndivyo ilivyo. Ikawa alipokwisha kusema, tazama, wana wa mfalme walikuja, nao wakapaza sauti zao wakalia; mfalme naye akalia, na watumishi wake wote, kilio kikubwa mno. Lakini Absalomu akakimbia, akamwendea Talmai, mwana wa Amihuri, mfalme wa Geshuri. Naye Daudi akamlilia mwanawe kila siku. Basi Absalomu akakimbia, akaenda Geshuri, akakaa huko muda wa miaka mitatu. Mfalme Daudi akatamani kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa.
2 Samueli 13:1-39 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ikawa baada ya hayo, Amnoni mwana wa Daudi akampenda Tamari, dada yake Absalomu mwana wa Daudi, aliyekuwa mzuri wa sura. Amnoni akasumbuka sana kuhusu Tamari hata akaugua, kwa kuwa Tamari alikuwa bikira, na ilionekana kwamba haiwezekani Amnoni kumfanyia jambo lolote. Basi Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi. Yonadabu alikuwa mtu wa hila nyingi sana. Akamuuliza Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme; kwa nini siku baada ya siku unaonekana kukonda? Hutaniambia?” Amnoni akamwambia, “Ninampenda Tamari, dada yake Absalomu ndugu yangu.” Yonadabu akamwambia, “Nenda ukalale kitandani na ujifanye kuwa mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona mwambie, ‘Ningependa Tamari dada yangu aje kunipatia chochote ili nile. Tafadhali mruhusu aje na kuniandalia chakula mbele yangu ningali ninamwona, ili nipate kula kutoka mkononi mwake.’ ” Kwa hiyo Amnoni akalala kitandani kujifanya mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia, “Ningependa dada yangu Tamari aje na kuniandalia mikate maalum mbele yangu, ili nipate kula toka mkononi mwake.” Daudi akampelekea Tamari ujumbe huko kwenye jumba la kifalme, kusema: “Nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni ukamwandalie chakula.” Kwa hiyo Tamari akaenda nyumbani mwa nduguye Amnoni, ndugu aliyekuwa amelala. Tamari akachukua unga uliotiwa chachu akaukanda, akaiandaa mikate mbele yake na kuioka. Tamari akaondoa mikate kwenye kikaango ili ampatie Amnoni, lakini akakataa kula. Amnoni akamwambia, “Mtoe nje kila mtu aliye hapa.” Kwa hiyo kila mmoja akaondoka. Ndipo Amnoni akamwambia Tamari, “Leta mkate hapa ndani ya chumba changu ili nipate kula kutoka mkononi mwako.” Basi Tamari akachukua mikate aliyoiandaa na kumletea Amnoni ndugu yake ndani ya chumba chake. Lakini alipompelekea ili ale, akamkamata kwa nguvu na kumwambia, “Njoo ulale nami, dada yangu.” Akamwambia, “Usifanye hivyo, ndugu yangu! Usinitende jeuri! Jambo la namna hii halistahili kufanyika katika Israeli! Usitende jambo hili ovu. Kwa upande wangu je, itakuwaje? Nitaipeleka wapi aibu yangu? Pia kwa upande wako, itakuwaje? Utakuwa kama mmoja wa wapumbavu waovu katika Israeli. Tafadhali zungumza na mfalme; hatakukatalia wewe kunioa.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, na kwa kuwa alikuwa na nguvu kuliko Tamari, akamtenda jeuri. Kisha Amnoni akamchukia Tamari, kwa machukio makuu sana. Kwa kweli, Amnoni alimchukia kuliko alivyokuwa amempenda. Amnoni akamwambia, “Inuka na utoke nje!” Tamari akamwambia, “Hapana! Kunifukuza itakuwa vibaya kuliko yale uliyonitendea.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza. Akamwita mtumishi wake mahsusi na kumwambia, “Mtoe huyu mwanamke hapa na ufunge mlango nyuma yake.” Kwa hiyo, mtumishi wake akamtoa nje na kufunga mlango nyuma yake. Tamari alikuwa amevaa joho lililopambwa vizuri, kwa maana lilikuwa aina ya mavazi yaliyovaliwa na binti za mfalme waliokuwa mabikira. Tamari akajitia majivu kichwani mwake na kurarua lile joho alilokuwa amevaa. Akaweka mkono wake kichwani, akaenda zake akilia kwa sauti. Absalomu nduguye akamuuliza, “Je, huyo Amnoni ndugu yako, amekutana nawe kimwili? Sasa nyamaza dada yangu; yeye ni ndugu yako. Usilitie jambo hili moyoni.” Naye Tamari akaishi nyumbani mwa Absalomu nduguye, akiwa mwanamke mwenye huzuni. Mfalme Daudi aliposikia mambo haya yote, akakasirika sana. Absalomu hakusema neno lolote, zuri au baya, kwa Amnoni; alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake. Miaka miwili baadaye, wakati wakata manyoya ya kondoo wa Absalomu walipokuwa huko Baal-Hasori karibu na mpaka wa Efraimu, alialika wana wote wa mfalme kuja huko. Absalomu akaenda kwa mfalme na kumwambia, “Mtumishi wako ninao wakata manyoya ya kondoo waliokuja. Tafadhali, je, mfalme na maafisa wake wanaweza kuungana nami?” Mfalme akajibu, “La, mwanangu. Si lazima sote tuje, tutakuwa tu mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alimsihi sana, mfalme alikataa kwenda, lakini akambariki. Basi Absalomu akasema, “Kama hutakuja, tafadhali mruhusu ndugu yangu Amnoni twende pamoja naye.” Mfalme akamuuliza, “Kwa nini aende pamoja nawe?” Lakini Absalomu alimsihi, kwa hiyo mfalme akamtuma Amnoni pamoja na wana wengine wa mfalme waliobaki. Absalomu aliagiza watu wake, “Sikilizeni! Amnoni atakapokuwa amekunywa mvinyo na kulewa sana nami nikiwaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ basi muueni. Msiogope. Je, si mimi niliyewapa amri hii? Kuweni hodari na wenye ushujaa.” Kwa hiyo watu wa Absalomu wakamtendea Amnoni kama vile Absalomu alivyokuwa amewaagiza. Ndipo wana wote wa mfalme wakainuka, wakapanda nyumbu zao, wakakimbia. Wakiwa njiani, taarifa ilimjia Daudi, kusema: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme; hakuna hata mmoja aliyesalia.” Mfalme akasimama, akararua nguo zake, akalala chini ardhini; nao watumishi wake wote wakasimama kando yake na nguo zao zikiwa zimeraruliwa. Lakini Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akasema, “Bwana wangu asifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme; ni Amnoni peke yake ndiye alikufa. Hili limekuwa kusudi la moyo wa Absalomu tangu siku ile Amnoni alipomtendea jeuri Tamari, dada yake. Mfalme bwana wangu asisumbuliwe na taarifa kwamba wamewaua wana wote wa mfalme. Ni Amnoni peke yake aliyekufa.” Wakati huo, Absalomu akawa amekimbia. Basi mlinzi akaangalia, naye akaona watu wengi barabarani magharibi yake, wakishuka kutoka upande wa kilima. Mlinzi akaenda akamwambia mfalme, “Naona watu wakitokea upande wa Horonaimu, huko upande wa kilimani.” Yonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wako hapa; imekuwa kama vile mtumishi wako alivyosema.” Mara alipomaliza kusema, wana wa mfalme wakaingia ndani wakiomboleza kwa makelele. Pia mfalme na watumishi wake wote wakalia sana kwa uchungu. Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Lakini Mfalme Daudi akaomboleza kwa ajili ya mwanawe kila siku. Baada ya Absalomu kukimbia na kwenda Geshuri, akakaa huko miaka mitatu. Roho ya Mfalme Daudi ikatamani kumwendea Absalomu, kwa maana mfalme alikuwa amefarijika kuhusu kifo cha Amnoni.