Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 13:1-22

2 Samueli 13:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Absalomu, alikuwa na dada yake mzuri aliyeitwa Tamari. Muda si muda, Amnoni, mtoto mwingine wa kiume wa Daudi, akampenda sana Tamari. Amnoni aliteseka sana hata akajifanya mgonjwa kwa sababu ya dada yake Tamari hasa kwa vile Tamari alikuwa bikira, na ilionekana jambo lisilowezekana kwa Amnoni kufanya chochote naye. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki aliyeitwa Yonadabu, mtoto wa Shama, ndugu ya Daudi. Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. Yonadabu akamwambia Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme, kwa nini unakonda na unaonekana huna furaha kila siku? Mbona hutaki kuniambia.” Amnoni akamwambia, “Nampenda Tamari, dada ya ndugu yangu Absalomu.” Yonadabu akamwambia, “Wewe jilaze kitandani ukidai kuwa u mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona, wewe msihi ukisema, ‘Mruhusu dada yangu, Tamari, aje aniletee mkate nipate kula na aniandalie chakula mbele yangu ili nikione naye mwenyewe anilishe.’” Hivyo, Amnoni akaendelea kulala kitandani, akijifanya mgonjwa. Mfalme alipokwenda kumwona, Amnoni alimwambia, “Nakuomba, Tamari aje hapa anitengenezee mikate michache huku nikimwangalia. Halafu yeye mwenyewe anilishe.” Hivyo, Daudi alipeleka ujumbe kwa Tamari kwamba aende nyumbani kwa kaka yake Amnoni, akamtengenezee chakula. Tamari alikwenda huko, akamkuta Amnoni amelala. Akachukua unga, akaukanda, na kuoka mikate mbele ya Amnoni. Mikate hiyo ilipokuwa tayari, Tamari akaiopoa kutoka kikaangoni. Akampelekea Amnoni, lakini Amnoni alikataa kula, akasema kila mmoja na atolewe nje, na wote wakaondoka. Kisha, Amnoni akamwambia Tamari, “Sasa niletee mikate hiyo chumbani kwangu, halafu unilishe.” Tamari aliichukua mikate aliyoiandaa na kuipeleka chumbani kwa kaka yake Amnoni. Hapo, alipokuwa anampatia mikate hiyo, Amnoni alimkamata na kumwambia, “Njoo ulale nami.” Tamari akamwambia, “Sivyo, kaka yangu, usinilazimishe. Kitendo hiki hakifanyiki katika Israeli. Usifanye kitendo hiki cha kipumbavu. Kwa upande wangu, siwezi kuvumilia aibu hiyo. Na kwa upande wako, utakuwa mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, mimi nakusihi uzungumze na mfalme kwani hatakukataza kunioa.” Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza na kwa kuwa alimzidi nguvu, alimlazimisha, akalala naye. Kisha, Amnoni akamchukia Tamari kupita kiasi. Akamchukia Tamari kuliko alivyompenda hapo awali. Akamwambia Tamari, “Ondoka mara moja.” Tamari akamjibu, “Sivyo kaka yangu; ovu hili kubwa la kunifukuza ni baya zaidi kuliko lile ulilonitendea.” Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza. Akamwita kijana wake aliyemtumikia, akamwambia, “Mtoe mwanamke huyu mbele yangu. Na mlango uufunge kwa komeo.” Amnoni na yule kijana wakamtoa nje na kuufunga mlango kwa komeo. Tamari alikuwa amevaa vazi refu lenye mikono mirefu kwani hivyo ndivyo walivyovaa mabikira wa mfalme zamani hizo. Basi, Tamari alijipaka majivu kichwani, akalipasua vazi lake, akaweka mikono yake kichwani, halafu akaondoka huku analia kwa sauti. Kaka yake, Absalomu, alipomwona, alimwuliza, “Je, Amnoni kaka yako amelala nawe? Tulia dada yangu. Yeye ni kaka yako. Usilitie jambo hilo moyoni mwako.” Hivyo, Tamari aliishi katika nyumba ya Absalomu akiwa na huzuni na mpweke. Mfalme Daudi aliposikia jambo hilo alikasirika sana. Absalomu alimchukia Amnoni sana hata hakusema naye, kwa sababu alimshika kwa nguvu dada yake Tamari akalala naye.

2 Samueli 13:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na dada yake mzuri, aliyeitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya yule dada yake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lolote. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, dada ya kaka yangu, Absalomu. Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake. Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake. Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula. Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate. Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Ndipo watu wote wakaondoka. Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoiandaa, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, dada yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinilazimishe; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Lakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamlazimisha, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunifukuza ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamtoa nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti. Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu. Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana. Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumlazimisha dada yake Tamari.

2 Samueli 13:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote. Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, umbu la ndugu yangu, Absalomu. Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake. Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake. Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula. Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate. Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Wakatoka kila mtu kwake. Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti. Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu. Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana. Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari.

2 Samueli 13:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ikawa baada ya hayo, Amnoni mwana wa Daudi akampenda Tamari, dada yake Absalomu mwana wa Daudi, aliyekuwa mzuri wa sura. Amnoni akasumbuka sana kuhusu Tamari hata akaugua, kwa kuwa Tamari alikuwa bikira, na ilionekana kwamba haiwezekani Amnoni kumfanyia jambo lolote. Basi Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi. Yonadabu alikuwa mtu wa hila nyingi sana. Akamuuliza Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme; kwa nini siku baada ya siku unaonekana kukonda? Hutaniambia?” Amnoni akamwambia, “Ninampenda Tamari, dada yake Absalomu ndugu yangu.” Yonadabu akamwambia, “Nenda ukalale kitandani na ujifanye kuwa mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona mwambie, ‘Ningependa Tamari dada yangu aje kunipatia chochote ili nile. Tafadhali mruhusu aje na kuniandalia chakula mbele yangu ningali ninamwona, ili nipate kula kutoka mkononi mwake.’ ” Kwa hiyo Amnoni akalala kitandani kujifanya mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia, “Ningependa dada yangu Tamari aje na kuniandalia mikate maalum mbele yangu, ili nipate kula toka mkononi mwake.” Daudi akampelekea Tamari ujumbe huko kwenye jumba la kifalme, kusema: “Nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni ukamwandalie chakula.” Kwa hiyo Tamari akaenda nyumbani mwa nduguye Amnoni, ndugu aliyekuwa amelala. Tamari akachukua unga uliotiwa chachu akaukanda, akaiandaa mikate mbele yake na kuioka. Tamari akaondoa mikate kwenye kikaango ili ampatie Amnoni, lakini akakataa kula. Amnoni akamwambia, “Mtoe nje kila mtu aliye hapa.” Kwa hiyo kila mmoja akaondoka. Ndipo Amnoni akamwambia Tamari, “Leta mkate hapa ndani ya chumba changu ili nipate kula kutoka mkononi mwako.” Basi Tamari akachukua mikate aliyoiandaa na kumletea Amnoni ndugu yake ndani ya chumba chake. Lakini alipompelekea ili ale, akamkamata kwa nguvu na kumwambia, “Njoo ulale nami, dada yangu.” Akamwambia, “Usifanye hivyo, ndugu yangu! Usinitende jeuri! Jambo la namna hii halistahili kufanyika katika Israeli! Usitende jambo hili ovu. Kwa upande wangu je, itakuwaje? Nitaipeleka wapi aibu yangu? Pia kwa upande wako, itakuwaje? Utakuwa kama mmoja wa wapumbavu waovu katika Israeli. Tafadhali zungumza na mfalme; hatakukatalia wewe kunioa.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, na kwa kuwa alikuwa na nguvu kuliko Tamari, akamtenda jeuri. Kisha Amnoni akamchukia Tamari, kwa machukio makuu sana. Kwa kweli, Amnoni alimchukia kuliko alivyokuwa amempenda. Amnoni akamwambia, “Inuka na utoke nje!” Tamari akamwambia, “Hapana! Kunifukuza itakuwa vibaya kuliko yale uliyonitendea.” Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza. Akamwita mtumishi wake mahsusi na kumwambia, “Mtoe huyu mwanamke hapa na ufunge mlango nyuma yake.” Kwa hiyo, mtumishi wake akamtoa nje na kufunga mlango nyuma yake. Tamari alikuwa amevaa joho lililopambwa vizuri, kwa maana lilikuwa aina ya mavazi yaliyovaliwa na binti za mfalme waliokuwa mabikira. Tamari akajitia majivu kichwani mwake na kurarua lile joho alilokuwa amevaa. Akaweka mkono wake kichwani, akaenda zake akilia kwa sauti. Absalomu nduguye akamuuliza, “Je, huyo Amnoni ndugu yako, amekutana nawe kimwili? Sasa nyamaza dada yangu; yeye ni ndugu yako. Usilitie jambo hili moyoni.” Naye Tamari akaishi nyumbani mwa Absalomu nduguye, akiwa mwanamke mwenye huzuni. Mfalme Daudi aliposikia mambo haya yote, akakasirika sana. Absalomu hakusema neno lolote, zuri au baya, kwa Amnoni; alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake.