2 Samueli 12:7-15
2 Samueli 12:7-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Mimi nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli na kukuokoa mikononi mwa Shauli. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake zake wawe wako, tena nikakupa watu wa Israeli na wa Yuda uwatawale. Na kama haya yangekuwa kidogo mno kwako ningekuongezea mara mbili zaidi ya hayo. Kwa nini basi, umedharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu ukafanya uovu huu mbele yangu? Umemuua Uria Mhiti, kwa upanga, ukamchukua mke wake kuwa mkeo. Umewatumia Waamoni kumwua Uria vitani! Kwa hiyo basi, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria Mhiti, kuwa mkeo, mauaji hayataondoka katika jamaa yako’. Sikiliza, Mwenyezi-Mungu asema, ‘Tazama, nitazusha maafa katika jamaa yako mwenyewe. Nitawachukua wake zako ukiona kwa macho yako mwenyewe na kumpa jirani yako, naye atalala nao hadharani. Wewe ulifanya jambo hilo kwa siri, lakini mimi nitayafanya haya mbele ya Waisraeli wote hadharani.’” Basi, Daudi akamwambia Nathani, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu.” Nathani akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amekusamehe dhambi yako, nawe hutakufa. Hata hivyo, kwa kuwa kwa tendo lako umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu, mtoto wako atakufa.” Kisha Nathani akarudi nyumbani kwake.
2 Samueli 12:7-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nilikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa kutoka kwa mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo mengine mengi. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa Waamoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. BWANA asema hivi, Angalia, nitakuzushia uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako hadharani. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na hadharani. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa mgonjwa sana.
2 Samueli 12:7-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. BWANA asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa hawezi sana.
2 Samueli 12:7-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba yote ya Israeli na ya Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi. Kwa nini ulilidharau neno la BWANA kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria Mhiti kwa upanga, na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni. Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe, kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria Mhiti kuwa mkeo.’ “Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Kutoka kwa nyumba yako mwenyewe nitaleta maafa juu yako. Mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako mchana mwangavu. Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu mbele ya Israeli yote.’ ” Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya BWANA.” Nathani akamjibu, “BWANA amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za BWANA kuonesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.” Baada ya Nathani kurudi nyumbani mwake, BWANA akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua.