2 Samueli 12:1-25
2 Samueli 12:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi Mwenyezi-Mungu akamtuma nabii Nathani kwa Daudi. Nathani alimwendea Daudi, akamwambia, “Kulikuwa na wanaume wawili katika mji mmoja; mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo wengi na ng'ombe wengi. Lakini yule maskini alikuwa na mwanakondoo mdogo mmoja jike, ambaye alikuwa amemnunua. Alimtunza, naye akakua nyumbani mwake pamoja na watoto wake. Alimlisha mwanakondoo huyo chakula kilekile kama chake na kunywea kikombe chake naye pia alikuwa akimpakata kifuani. Mwanakondoo huyo alikuwa kama binti kwa yule mtu maskini. Siku moja, yule tajiri alifikiwa na mgeni. Basi, tajiri huyo hakutaka kuchukua mmoja wa kondoo wake mwenyewe au ng'ombe wake, amchinjie mgeni wake, ila alikwenda na kumnyanganya yule maskini mwanakondoo wake, akamchinjia mgeni wake.” Daudi aliposikia hayo, akawaka hasira dhidi ya yule tajiri. Akamwambia nabii Nathani, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai kwamba mtu aliyefanya jambo hilo anastahili kufa! Ni lazima amlipe yule maskini mwanakondoo huyo, tena mara nne, kwani ametenda jambo baya na hakuwa na huruma!” Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Mimi nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli na kukuokoa mikononi mwa Shauli. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake zake wawe wako, tena nikakupa watu wa Israeli na wa Yuda uwatawale. Na kama haya yangekuwa kidogo mno kwako ningekuongezea mara mbili zaidi ya hayo. Kwa nini basi, umedharau neno langu mimi Mwenyezi-Mungu ukafanya uovu huu mbele yangu? Umemuua Uria Mhiti, kwa upanga, ukamchukua mke wake kuwa mkeo. Umewatumia Waamoni kumwua Uria vitani! Kwa hiyo basi, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria Mhiti, kuwa mkeo, mauaji hayataondoka katika jamaa yako’. Sikiliza, Mwenyezi-Mungu asema, ‘Tazama, nitazusha maafa katika jamaa yako mwenyewe. Nitawachukua wake zako ukiona kwa macho yako mwenyewe na kumpa jirani yako, naye atalala nao hadharani. Wewe ulifanya jambo hilo kwa siri, lakini mimi nitayafanya haya mbele ya Waisraeli wote hadharani.’” Basi, Daudi akamwambia Nathani, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu.” Nathani akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amekusamehe dhambi yako, nawe hutakufa. Hata hivyo, kwa kuwa kwa tendo lako umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu, mtoto wako atakufa.” Kisha Nathani akarudi nyumbani kwake. Mwenyezi-Mungu alimpiga mtoto ambaye Bathsheba mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa mgonjwa. Daudi alimwomba Mungu mtoto apate nafuu. Alikwenda chumbani kwake, na usiku kucha akalala sakafuni. Wazee waliokuwa wanamwangalia katika jumba hilo walimfuata na kumsihi aamke, lakini yeye alikataa, na hakula chakula chochote pamoja nao. Juma moja baadaye, mtoto huyo akafa. Watumishi wa Daudi waliogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwani walifikiri, “Mtoto huyo alipokuwa hai, tulizungumza naye, lakini hakutusikiliza. Sasa, tutamwambiaje kuwa mtoto wake amekufa? Huenda akajidhuru.” Daudi alipowaona watumishi wake wananongonezana, akagundua kuwa mtoto wake amekufa. Hivyo, akawauliza, “Je, mtoto amekufa?” Nao wakamjibu, “Naam! Amekufa.” Kisha, Daudi aliinuka kutoka sakafuni, akaoga, akajipaka mafuta na kubadilisha mavazi yake. Halafu akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu. Kisha akarudi nyumbani na alipotaka chakula, akapewa, naye akala. Ndipo watumishi wake wakamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilofanya? Mtoto alipokuwa hai, wewe ulifunga na kumlilia. Lakini alipokufa, umeinuka, ukala chakula.” Daudi akawajibu, “Ni kweli mtoto alipokuwa hai, nilifunga na kulia. Nilifanya hivyo kwani nilifikiri, ‘Nani anajua? Huenda Mwenyezi-Mungu akanirehemu ili mtoto aishi’. Lakini sasa amekufa, ya nini nifunge? Je, mimi naweza kumrudisha duniani? Siku moja, nitakwenda huko alikokwenda, lakini yeye hawezi kurudi kwangu.” Halafu Daudi akamfariji Bathsheba mkewe. Akalala naye, naye akapata mimba na kujifungua mtoto wa kiume, ambaye Daudi alimwita Solomoni. Mwenyezi-Mungu alimpenda mtoto huyo, naye akamtuma nabii Nathani kwa Daudi kuwa amwite mtoto huyo Yedidia kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.
2 Samueli 12:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana-kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Kisha msafiri mmoja akamfikia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikia, bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nilikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa kutoka kwa mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo mengine mengi. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa Waamoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. BWANA asema hivi, Angalia, nitakuzushia uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako hadharani. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na hadharani. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa mgonjwa sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala chini usiku kucha. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue kutoka chini; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; si atajidhuru, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa? Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong'onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa. Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa BWANA, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala. Watumishi wake wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula. Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nilifunga, nikalia; kwa maana nilisema, Ni nani ajuaye kama BWANA atanihurumia, mtoto apate kuishi? Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi. Naye Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye BWANA akampenda; akapeleka kwa mkono wa Nathani, nabii, naye akamwita jina lake Yedidia, kwa ajili ya BWANA.
2 Samueli 12:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. BWANA asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa hawezi sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa? Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong’onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa. Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa BWANA, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala. Watumishi wake wakamwambia, Ni neno gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula. Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nalifunga, nikalia; kwa maana nalisema, Ni nani ajuaye kwamba BWANA atanihurumia, mtoto apate kuishi? Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi. Naye Daudi akamfariji Bath-sheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye BWANA akampenda; akapeleka kwa mkono wa Nathani, nabii, naye akamwita jina lake Yedidia, kwa ajili ya BWANA.
2 Samueli 12:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwa na watu wawili; mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ngʼombe, lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake, hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake. “Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri hakuchukua mmoja wa kondoo au ngʼombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.” Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama BWANA aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.” Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli. Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba yote ya Israeli na ya Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi. Kwa nini ulilidharau neno la BWANA kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria Mhiti kwa upanga, na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni. Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe, kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria Mhiti kuwa mkeo.’ “Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Kutoka kwa nyumba yako mwenyewe nitaleta maafa juu yako. Mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako mchana mwangavu. Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu mbele ya Israeli yote.’ ” Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya BWANA.” Nathani akamjibu, “BWANA amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za BWANA kuonesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.” Baada ya Nathani kurudi nyumbani mwake, BWANA akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua. Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha. Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao. Ilipotimia siku ya saba, yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.” Daudi akaona kuwa watumishi wake wananongʼonezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?” Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.” Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya BWANA, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani mwake, akaomba wamwandalie chakula, naye akala. Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.” Akajibu, “Mtoto alipokuwa angali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? BWANA aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’ Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitaenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.” Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe; akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina Sulemani. BWANA alimpenda Sulemani. Kwa kuwa BWANA alimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidia kwa ajili ya BWANA.