2 Samueli 11:1-5
2 Samueli 11:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Hata ikawa katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Daudi alimtuma Yoabu na maofisa wake pamoja na Waisraeli wote kupigana; nao waliteka nyara Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi alibaki Yerusalemu. Siku moja, wakati wa jioni, Daudi aliamka kitandani akaenda kwenye paa ya ikulu. Alipokuwa anatembea huko juu, alimwona mwanamke mmoja akioga na mwanamke huyo alikuwa mzuri sana. Daudi akatuma mtu kuuliza mwanamke huyo ni nani. Mtu huyo akamwambia Daudi “Mwanamke huyo ni Bathsheba binti wa Eliabu, na ni mke wa Uria Mhiti.” Basi, Daudi alituma wajumbe wamlete. Basi Bathsheba akaja kwa Daudi, naye Daudi akalala naye; (mwanamke huyo alikuwa ndio tu amejitakasa baada ya hedhi yake); kisha akarudi nyumbani kwake. Mwanamke huyo akapata mimba, naye akatuma habari kwa Daudi kuwa ana mimba yake.
2 Samueli 11:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza Waamoni, wakauzingira Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari la jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akatuma mtu akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bathsheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akatuma wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka habari na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja mzito.
2 Samueli 11:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito.
2 Samueli 11:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme hutoka kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu. Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Akiwa kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura, naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria Mhiti?” Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani mwake. Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.”