2 Samueli 11:1-27
2 Samueli 11:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Hata ikawa katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Daudi alimtuma Yoabu na maofisa wake pamoja na Waisraeli wote kupigana; nao waliteka nyara Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi alibaki Yerusalemu. Siku moja, wakati wa jioni, Daudi aliamka kitandani akaenda kwenye paa ya ikulu. Alipokuwa anatembea huko juu, alimwona mwanamke mmoja akioga na mwanamke huyo alikuwa mzuri sana. Daudi akatuma mtu kuuliza mwanamke huyo ni nani. Mtu huyo akamwambia Daudi “Mwanamke huyo ni Bathsheba binti wa Eliabu, na ni mke wa Uria Mhiti.” Basi, Daudi alituma wajumbe wamlete. Basi Bathsheba akaja kwa Daudi, naye Daudi akalala naye; (mwanamke huyo alikuwa ndio tu amejitakasa baada ya hedhi yake); kisha akarudi nyumbani kwake. Mwanamke huyo akapata mimba, naye akatuma habari kwa Daudi kuwa ana mimba yake. Basi, Daudi akamtumia Yoabu ujumbe, “Mtume Uria, Mhiti kwangu.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. Uria alipofika kwake, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, watu wote, na hali ya vita. Halafu Daudi alimwambia Uria, “Rudi nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Uria alitoka nyumbani kwa mfalme, na mara mfalme akampelekea zawadi. Lakini Uria hakurudi nyumbani kwake, bali alilala pamoja na watumishi wote wa bwana wake kwenye lango la ikulu. Daudi alipoambiwa kwamba Uria hakwenda nyumbani kwake, Daudi alimwuliza Uria, “Wewe umetoka safari, kwa nini hukuenda nyumbani kwako?” Uria alimjibu Daudi “Sanduku la agano, pamoja na majeshi yote ya Israeli na Yuda yanakaa kwenye vibanda vitani. Bwana wangu Yoabu na watumishi wake wote wamepiga kambi mbugani; je ni sawa mimi niende nyumbani nikale na kunywa na kulala na mke wangu? Kama uishivyo na roho yako inavyoishi, sitafanya kitu cha namna hiyo.” Kisha, Daudi akamwambia Uria, “Basi, kaa hapa leo pia, na kesho nitakuacha urudi.” Hivyo Uria akabaki mjini Yerusalemu siku hiyo. Siku iliyofuata, Daudi alimwalika Uria kula na kunywa huko kwake, akamfanya Uria alewe. Hata hivyo, usiku ule Uria hakwenda nyumbani kwake, ila alilala kwenye kochi lake pamoja na watumishi wa bwana wake. Asubuhi yake, Daudi alimwandikia Yoabu barua akampa Uria aipeleke kwa Yoabu. Katika barua hiyo Daudi aliandika hivi: “Mweke Uria kwenye mstari wa mbele, mahali ambako mapigano ni makali kabisa, kisha umwache huko na kurudi nyuma ili apigwe, afe.” Basi, Yoabu alipokuwa anauzingira mji alimweka Uria mahali ambapo alijua wazi wanajeshi wa adui walikuwa hodari sana. Wakazi wa mji huo walitoka katika mji wao na kupigana na Yoabu. Baadhi ya watumishi wa Daudi, waliuawa. Uria Mhiti naye aliuawa pia. Kisha, Yoabu alipeleka habari zote kwa Daudi akimweleza juu ya vita. Yoabu akamwamuru huyo mtumishi aliyemtuma hivi, “Baada ya kumweleza mfalme mambo yote kuhusu vita, akikasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlikwenda karibu na mji mlipokuwa mnapigana? Hamkujua kwamba wangewapiga mishale kutoka kwenye kuta za mji wao? Nani alimuua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Si alikuwa mwanamke mmoja mjini Thebesi ambaye alitupa jiwe la kusagia kutoka kwenye ukuta nalo likamuua Abimeleki? Kwa nini basi, mlikwenda karibu na ukuta?’ Basi, wewe utamwambia hivi, ‘Hata mtumishi wako Uria Mhiti, naye amekufa.’” Yule mjumbe alikwenda kwa Daudi na kumwambia yote aliyotumwa na Yoabu ayaseme. Yule mjumbe akamwambia Daudi, “Adui zetu walituzidi nguvu, wakatoka nje ya miji na kutushambulia nyikani. Hata hivyo sisi tuliwarudisha mpaka kwenye lango la mji. Halafu wakatupiga mishale sisi watumishi wako kutoka ukutani. Baadhi ya watumishi wako waliuawa. Hata mtumishi wako Uria, Mhiti, naye amekufa.” Daudi akamwambia yule mjumbe, “Utamwambia hivi Yoabu, ‘Jambo hili lisikusumbue kwani upanga hauna macho, vita huua yeyote yule. Bali, imarisha mashambulizi dhidi ya mji, hadi umeuangamiza mji huo’. Ndivyo utakavyomtia moyo Yoabu.” Bathsheba mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe Uria amekufa, alimwombolezea mumewe. Muda wa matanga ulipokwisha, Daudi aliagiza Bathsheba achukuliwe na kupelekwa nyumbani kwake. Bathsheba akawa mke wa Daudi, naye akamzalia Daudi mtoto wa kiume. Lakini jambo hilo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi-Mungu.
2 Samueli 11:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza Waamoni, wakauzingira Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari la jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akatuma mtu akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bathsheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akatuma wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka habari na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja mzito. Ndipo Daudi akapeleka habari kwa Yoabu, akisema, Mtume kwangu Uria, Mhiti. Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita. Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake. Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako? Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili. Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake. Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hadi wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake. Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akaituma kwa mkono wa Uria. Akaandika katika barua hiyo, akasema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria, Mhiti, naye akafa. Ndipo Yoabu akapeleka ujumbe na kumwarifu Daudi habari zote za vita; akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita, kisha, ikiwa hasira ya mfalme itawaka, akakuambia, Kwa nini mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani? Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwa nini mliukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye. Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu. Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hadi mahali pa kuingilia langoni. Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye. Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo. Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe. Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mtoto wa kiume.
2 Samueli 11:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito. Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi. Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita. Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake. Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako? Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili. Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake. Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake. Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa. Ndipo Yoabu akapeleka na kumwarifu Daudi habari zote za vita; akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita, itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani? Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwani kuukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye. Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonyesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu. Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hata mahali pa kuingilia langoni. Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye. Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo. Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe. Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mwana.
2 Samueli 11:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme hutoka kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu. Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Akiwa kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura, naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria Mhiti?” Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani mwake. Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.” Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje. Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani mwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akatoka jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakuteremka kwenda nyumbani mwake. Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakuenda nyumbani,” Daudi akamuuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukuenda nyumbani?” Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani mwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo kama hilo!” Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata. Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakuenda nyumbani. Kesho yake asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka. Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.” Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali alipojua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana. Wanaume wa mji walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa; zaidi ya hayo, Uria Mhiti akafa. Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita. Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita, hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani? Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Akikuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria Mhiti amekufa.’ ” Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema. Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma hadi ingilio la mji. Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria Mhiti, mtumishi wako, amekufa.” Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.” Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea. Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akatumana aletwe nyumbani mwake. Naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilofanya Daudi lilimchukiza BWANA.