2 Samueli 10:9-14
2 Samueli 10:9-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Yoabu alipoona kuwa vita ni vikali dhidi yake, mbele na nyuma, aliwateua baadhi ya wanajeshi Waisraeli hodari zaidi akawapanga kukabiliana na Waaramu. Wale wanajeshi wengine waliobaki aliwaweka chini ya uongozi wa ndugu yake Abishai, naye akawapanga ili wakabiliane na Waamoni. Yoabu akamwambia Abishai, “Ikiwa Waaramu wananizidi nguvu, utanisaidia lakini kama Waamoni wanakuzidi nguvu, nitakuja kukusaidia. Lakini jipe moyo! Tupigane kiume kwa ajili ya watu wetu na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Mwenyezi-Mungu atutendee lile analoona ni jema kwake.” Basi, Yoabu na watu wake walisonga mbele kwenda kupigana na Waaramu, nao Waaramu walikimbia. Waamoni walipoona kuwa Waaramu wamekimbia, nao pia walimkimbia Abishai na kuingia mjini. Yoabu akaacha kupigana na Waamoni, akarudi Yerusalemu.
2 Samueli 10:9-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami; akawatia nguvu watu waliosalia mkononi mwa Abishai, nduguye, akawapanga juu ya Waamoni. Akasema, Wakiwa Washami hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia, lakini Waamoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakuja nikusaidie wewe. Uwe hodari, tuwe na ujasiri, kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake. Basi Yoabu na watu waliokuwa pamoja naye wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake. Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akarudi kutoka kwa wana wa Amoni, akaja Yerusalemu.
2 Samueli 10:9-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami; akawatia nguvu watu waliosalia mkononi mwa Abishai, nduguye, akawapanga juu ya wana wa Amoni. Akasema, Wakiwa Washami hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia, lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakuja nikusaidie wewe. Uwe hodari, tukajitie moyo mkuu, kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake. Basi Yoabu na watu waliokuwa pamoja naye wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake. Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akarudi kutoka kwa wana wa Amoni, akaja Yerusalemu.
2 Samueli 10:9-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu. Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni. Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itawabidi mje kunisaidia. Lakini kama Waamoni watawazidi nguvu, basi nitakuja kuwasaidia. Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. BWANA atafanya lile lililo jema machoni pake.” Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake. Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.