2 Samueli 1:1-27
2 Samueli 1:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya kifo cha Shauli, Daudi alirudi baada ya kuwashinda Waamaleki, akakaa Siklagi kwa muda wa siku mbili. Siku iliyofuata, mtu mmoja kutoka kambi ya Shauli, mavazi yake yakiwa yamechanwa kwa huzuni na akiwa na mavumbi kichwani alimwendea Daudi. Alipomfikia Daudi, alijitupa chini mbele yake akamsujudia. Daudi akamwambia, “Unatoka wapi?” Naye akamwambia, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.” Daudi akamwambia, “Niambie mambo yalivyokuwa huko.” Yule mtu akamjibu, “Watu wetu wameyakimbia mapigano na wengi wetu wameuawa. Zaidi ya hayo, Shauli na mwanawe Yonathani pia wameuawa.” Daudi akamwuliza yule kijana, “Unajuaje kuwa Shauli na Yonathani mwanawe wamekufa?” Yule kijana akamjibu, “Kwa bahati, nilikuwapo mlimani Gilboa. Nilimwona Shauli ameegemea mkuki wake na magari ya wapandafarasi ya adui zake yalikuwa yanamsonga sana. Shauli alipotazama nyuma, aliniona, akaniita. Nilipoitika, yeye aliniuliza mimi ni nani, nami nikamwambia kuwa mimi ni Mmaleki. Hapo, akaniambia, ‘Karibia uniue maana nimejeruhiwa vibaya na maumivu ni makali. Lakini bado ningali hai’. Hivyo, nilikwenda karibu naye na kumuua, kwa sababu nilikuwa na uhakika kuwa akianguka chini, hataweza kuishi zaidi. Lakini taji iliyokuwa kichwani pake na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, vyote nimekuletea wewe, bwana wangu.” Daudi akayashika mavazi yake na kuyararua kwa huzuni. Hata watu waliokuwa pamoja na Daudi wakafanya vivyo hivyo. Wakaomboleza, wakalia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Shauli, Yonathani mwanawe, na nchi ya Waisraeli, watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wengi wao waliuawa vitani. Daudi akamwuliza yule kijana aliyempasha habari, “Unatoka wapi?” Yeye akajibu, “Mimi ni Mmaleki, lakini ninaishi katika nchi yako kama mgeni.” Daudi akamwuliza, “Ilikuwaje wewe hukuogopa kuunyosha mkono wako na kumuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta?” Kisha, Daudi akamwita mmoja wa vijana wake akamwambia, “Muue mtu huyu!” Yule kijana alimpiga yule Mmaleki, naye akafa. Daudi akasema, “Uwajibike wewe mwenyewe kwa kifo chako, maana umejishuhudia wewe mwenyewe kwa mdomo wako ukisema, ‘Nimemuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta.’” Daudi aliimba ombolezo lifuatalo kwa ajili ya Shauli na mwanawe Yonathani. Daudi alisema watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hilo, nalo limeandikwa katika kitabu cha Yashari. Daudi aliimba, “Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa milimani pako. Jinsi gani mashujaa walivyoanguka! Jambo hilo msiuambie mji wa Gathi wala katika mitaa ya Ashkeloni. La sivyo, wanawake Wafilisti watashangilia, binti za wasiotahiriwa, watafurahi. “Enyi milima ya Gilboa, msiwe na umande au mvua juu yenu. Wala mashamba yenu daima yasitoe chochote. Maana huko ngao za shujaa zilitiwa najisi, ngao ya Shauli haikupakwa mafuta. “Upinde wa Yonathani kamwe haukurudi nyuma, upanga wa Shauli kamwe haukurudi bure, daima ziliua wengi. Naam, ziliua mashujaa. “Shauli na Yonathani, watu wa ajabu na wakupendeza. Maishani na kifoni hawakutengana. Walikuwa wepesi kuliko tai, naam, wenye nguvu kuliko simba. “Wanawake wa Israeli, mlilieni Shauli! Aliwavika mavazi mekundu ya fahari, aliyatarizi mavazi yenu kwa dhahabu. “Jinsi gani mashujaa walivyoanguka! Wamekufa wakiwa katika mapambano. Yonathani analala, akiwa ameuawa milimani. Nasikitika kwa ajili yako, ndugu yangu Yonathani. Umekuwa kwangu daima mtu wa kupendeza, pendo lako kwangu limekuwa la ajabu, la ajabu kuliko la mwanamke. “Jinsi gani mashujaa wameanguka, na silaha zao zimeachwa, hazina kazi.”
2 Samueli 1:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi; hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia. Daudi akamwambia, Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli. Daudi akamwambia, Mambo yalikuwaje? Tafadhali niambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa. Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Umejuaje ya kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa? Yule kijana aliyempa habari akasema, Nilikuwapo kwa nasibu juu ya kilima cha Gilboa, na tazama, Sauli alikuwa ameegemea fumo lake; na tazama, magari na wapanda farasi wanamfuatia kwa kasi. Naye alipotazama nyuma, akaniona, akaniita. Nikajibu, Mimi hapa. Akaniambia, U nani wewe? Nikamjibu, Mimi ni Mwamaleki. Akaniambia, Tafadhali simama karibu nami, ukaniue, maana shida imenipata; kwa sababu roho yangu ingali hai ndani yangu. Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa sababu nilijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikalitwaa lile taji lililokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu. Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye; wakaomboleza, wakalia, wakafunga hadi jioni, kwa ajili ya Sauli, na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa BWANA na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga. Naye Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Unatoka wapi wewe? Akajibu, Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki. Daudi akamwambia, Jinsi gani hukuogopa kuunyosha mkono wako umwangamize masihi wa BWANA? Ndipo Daudi akamwita mmoja wa vijana, akamwambia, Mwendee, ukamwangukie. Basi akampiga hadi akafa. Daudi akamwambia, Damu yako na iwe juu ya kichwa chako mwenyewe; maana umejishuhudia nafsi yako ukisema, Nimemwua masihi wa BWANA. Basi Daudi akamwomboleza Sauli, na Yonathani, mwanawe, maombolezo haya; (kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yashari), akasema, Wana wa Yuda na wafundishwe haya, Walio fahari yako, Ee Israeli Juu ya mahali pako palipoinuka wameuawa; Jinsi mashujaa walivyoanguka! Msiyahubiri mambo haya katika Gathi, Msiyatangaze katika njia za Ashkeloni; Wasije wakashangilia binti za Wafilisti, Binti za wasiotahiriwa wakasimanga. Enyi milima ya Gilboa, visiwepo juu yenu Umande wala mvua, wala mashamba ya matoleo; Maana ndipo ilipotupwa kwa aibu ngao ya shujaa, Ngao yake Sauli, pasipo kutiwa mafuta. Kutoka kwa damu yao waliouawa, Kutoka kwa shahamu yao mashujaa, Upinde wa Yonathani haukurudi nyuma, Wala upanga wa Sauli haukurudi bure. Sauli na Yonathani walipendwa na kupendeza Maishani wala mautini hawakutengwa; Walikuwa wepesi kuliko tai, Walikuwa hodari kuliko simba. Enyi binti za Israeli, mlilieni Huyo Sauli, ambaye aliwavika Mavazi mekundu kwa anasa, Akazipamba nguo zenu dhahabu. Jinsi mashujaa walivyoanguka Katikati ya vita! Ee Yonathani, wewe umeuawa Juu ya mahali pako palipoinuka. Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana; Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake. Jinsi mashujaa walivyoanguka, Na silaha za vita zilivyoangamia!
2 Samueli 1:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi; hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia. Daudi akamwambia, Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli. Daudi akamwambia, Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa. Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Umejuaje ya kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa? Yule kijana aliyempa habari akasema, Nalikuwapo kwa nasibu juu ya kilima cha Gilboa, na tazama, Sauli alikuwa ameegemea fumo lake; na tazama, magari na wapanda farasi wanamfuatia kwa kasi. Naye alipotazama nyuma, akaniona, akaniita. Nikajibu, Mimi hapa. Akaniambia, U nani wewe? Nikamjibu, Mimi ni Mwamaleki. Akaniambia, Tafadhali simama karibu nami, ukaniue, maana shida imenipata; kwa sababu roho yangu ingali hai ndani yangu. Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa sababu nalijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikaitwaa ile taji iliyokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu. Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye; wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli, na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa BWANA na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga. Naye Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Watoka wapi wewe? Akajibu, Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki. Daudi akamwambia, Jinsi gani hukuogopa kuunyosha mkono wako umwangamize masihi wa BWANA? Ndipo Daudi akamwita mmoja wa vijana, akamwambia, Mwendee, ukamwangukie. Basi akampiga hata akafa. Daudi akamwambia, Damu yako na iwe juu ya kichwa chako mwenyewe; maana umejishuhudia nafsi yako ukisema, Nimemwua masihi wa BWANA. Basi Daudi akamwomboleza Sauli, na Yonathani, mwanawe, maombolezo haya; (kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yashari), akasema, Wana wa Yuda na wafundishwe haya, Walio fahari yako, Ee Israeli Juu ya mahali pako palipoinuka wameuawa; Jinsi mashujaa walivyoanguka! Msiyahubiri mambo haya katika Gathi, Msiyatangaze katika njia za Ashkeloni; Wasije wakashangilia binti za Wafilisti, Binti za wasiotahiriwa wakasimanga. Enyi milima ya Gilboa, visiwepo juu yenu Umande wala mvua, wala mashamba ya matoleo; Maana ndipo ilipotupwa kwa aibu ngao ya shujaa, Ngao yake Sauli, pasipo kutiwa mafuta. Kutoka kwa damu yao waliouawa, Kutoka kwa shahamu yao mashujaa, Upinde wa Yonathani haukurudi nyuma, Wala upanga wa Sauli haukurudi bure. Sauli na Yonathani walipendwa na kupendeza Maishani wala mautini hawakutengwa; Walikuwa wepesi kuliko tai, Walikuwa hodari kuliko simba. Enyi binti za Israeli, mlilieni Huyo Sauli, ambaye aliwavika Mavazi mekundu kwa anasa, Akazipamba nguo zenu dhahabu. Jinsi mashujaa walivyoanguka Katikati ya vita! Ee Yonathani, wewe umeuawa Juu ya mahali pako palipoinuka Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana; Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake. Jinsi mashujaa walivyoanguka, Na silaha za vita zilivyoangamia!
2 Samueli 1:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya kifo cha Sauli, Daudi alirudi kutoka kuwashinda Waamaleki, na akakaa siku mbili huko Siklagi. Siku ya tatu akaja mtu mwenye nguo zilizoraruka na mavumbi kichwani mwake kutoka kambi ya Sauli. Alipomjia Daudi, akajitupa chini ili kumpa heshima. Daudi akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?” Akamjibu, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.” Daudi akamuuliza, “Ni nini kilichotokea? Niambie.” Akasema, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wao walianguka na kufa. Naye Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa.” Ndipo Daudi akamwambia huyo kijana aliyemletea taarifa, “Je, umefahamu vipi kwamba Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?” Yule kijana akasema, “Nilijipata huko Mlima Gilboa, naye Sauli alikuwa huko akiegemea mkuki wake, na magari ya vita na wapanda farasi wa upande wa adui wakawa wamemkaribia sana. Alipogeuka na kuniona, akaniita, nami nikasema, ‘Je, nifanye nini?’ “Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’ “Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’ “Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’ “Kwa hiyo nikamkaribia na kumuua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.” Ndipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua. Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga hadi jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi la BWANA na nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga. Daudi akamwambia yule kijana aliyemletea taarifa, “Wewe unatoka wapi?” Akamjibu, “Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.” Daudi akamuuliza, “Kwa nini hukuogopa kuinua mkono wako ili kumwangamiza mpakwa mafuta wa BWANA?” Kisha Daudi akamwita mmoja wa watu wake na kumwambia, “Nenda ukamuue!” Kwa hiyo akampiga, naye akafa. Kwa maana Daudi alikuwa amemwambia, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako mwenyewe. Kinywa chako mwenyewe kimeshuhudia dhidi yako uliposema, ‘Nilimuua mpakwa mafuta wa BWANA.’ ” Daudi akafanya maombolezo haya kuhusu Sauli na Yonathani mwanawe, naye akaagiza kwamba watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hili la upinde (ambalo limeandikwa katika Kitabu cha Yashari): “Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa juu ya mahali pako palipoinuka. Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka! “Msilisimulie hili katika Gathi, msilitangaze hili katika barabara za Ashkeloni, binti za Wafilisti wasije wakafurahia, binti za hao wasiotahiriwa wasije wakashangilia. “Enyi milima ya Gilboa, msipate umande wala mvua, wala mashamba yanayozaa sadaka ya nafaka. Kwa maana huko ndiko ngao ya mwenye nguvu iliponajisiwa, ngao ya Sauli haitapakwa tena mafuta. “Kutokana na damu ya waliouawa, kutokana na miili ya wenye nguvu, ule upinde wa Yonathani haukugeuka nyuma. Upanga wa Sauli haukurudi bure. Sauli na Yonathani: maishani walipendwa na kuneemeka, na katika kifo hawakutengana. Walikuwa wepesi kuliko tai, walikuwa na nguvu kuliko simba. “Enyi binti za Israeli, lieni kwa ajili ya Sauli, ambaye aliwavika nguo nyekundu na maridadi, ambaye alirembesha mavazi yenu kwa mapambo ya dhahabu. “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka vitani! Yonathani ameuawa mahali pako palipoinuka. Nahuzunika kwa ajili yako, Yonathani ndugu yangu, kwangu ulikuwa mpendwa sana. Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, wa ajabu kuliko ule wa wanawake. “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka! Silaha za vita zimeangamia!”