Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Petro 1:1-21

2 Petro 1:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi. Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu. Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza imani yenu kwa fadhila, fadhila yenu kwa elimu, elimu yenu kwa kuwa na kiasi, kuwa na kiasi kwa uvumilivu, uvumilivu wenu kwa uchaji wa Mungu, uchaji wenu kwa urafiki wa kindugu, na urafiki wenu wa kindugu kwa mapendo. Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani. Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe. Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu na mko imara katika ukweli mlioupokea. Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya. Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi. Basi, nitajitahidi kusudi baada ya kufariki kwangu mweze kuyakumbuka mambo haya kila wakati. Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe. Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: “Huyu ni Mwanangu mpenzi ambaye nimependezwa naye.” Tena, sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye juu ya ule mlima mtakatifu. Tena, ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong'ara mioyoni mwenu. Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu. Maana hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walitoa unabii wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Shirikisha
Soma 2 Petro 1

2 Petro 1:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo, kwa wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa kutoka kwa uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, na kwa sababu iyo hiyo jitahidini sana ili katika imani yenu mtie na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu subira, na katika subira yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani. Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe. Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo nitakuwa tayari kuwakumbusha hayo siku zote, ijapokuwa mnayajua na kuthibitishwa katika kweli mliyo nayo. Nami naona ni haki, maadamu nipo mimi katika maskani hii, kuwaamsha kwa kuwakumbusha. Nikijua kwamba kule kuwekea mbali maskani yangu kwaja upesi, kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyonionesha. Lakini nitajitahidi, ili kila wakati baada ya kufariki kwangu mpate kuyakumbuka mambo hayo. Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa iangazayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu. Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika Maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Shirikisha
Soma 2 Petro 1

2 Petro 1:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo, kwa wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani. Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe. Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo nitakuwa tayari kuwakumbusha hayo siku zote, ijapokuwa mnayajua na kuthibitishwa katika kweli mliyo nayo. Nami naona ni haki, maadamu nipo mimi katika maskani hii, kuwaamsha kwa kuwakumbusha. Nikijua kwamba kule kuwekea mbali maskani yangu kwaja upesi, kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyonionyesha. Walakini nitajitahidi, kwamba kila wakati baada ya kufariki kwangu mpate kuyakumbuka mambo hayo. Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu. Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Shirikisha
Soma 2 Petro 1

2 Petro 1:1-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo. Kwa wale ambao kupitia kwa haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu. Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya. Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa; katika utauwa, upendano wa kindugu; na katika upendano wa kindugu, upendo. Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yatawasaidia kutokosa bidii wala kutokuzaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya, haoni mbali na ni kipofu, naye amesahau kwamba ametakaswa kutoka dhambi zake za zamani. Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe, na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo. Naona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niko katika hema hili ambalo ni mwili wangu, kwa sababu najua kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Yesu Kristo alivyoliweka wazi kwangu. Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote. Tulipowafahamisha kuhusu uweza na kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake. Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.” Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu. Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuke na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Shirikisha
Soma 2 Petro 1