2 Wafalme 6:8-12
2 Wafalme 6:8-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati mmoja kulikuwa na hali ya vita kati ya Aramu na Israeli. Basi, mfalme wa Aramu akashauriana na maofisa wake kuhusu mahali watakaposhambulia. Lakini Elisha akampelekea habari mfalme wa Israeli ajihadhari na mahali hapo, kwa kuwa Waaramu walikuwa tayari kupashambulia. Basi, mfalme wa Israeli akapeleka askari wake karibu na mahali alipoambiwa. Elisha aliendelea kumwonya mfalme naye mfalme alijiweka katika hali ya tahadhari. Jambo hilo lilifanyika mara nyingi. Mfalme wa Aramu akafadhaishwa sana na hali hiyo; akawaita maofisa wake, akawauliza, “Niambieni nani kati yenu anayetusaliti kwa mfalme wa Israeli?” Mmoja wao akajibu, “Hakuna anayetusaliti, ee mfalme. Anayehusika ni Elisha, nabii aliyeko huko Israeli. Yeye humwambia mfalme wa Israeli chochote unachosema hata ukiwa katika chumba chako cha kulala.”
2 Wafalme 6:8-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.
2 Wafalme 6:8-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.
2 Wafalme 6:8-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.” Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Elisha alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo. Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?” Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Elisha, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.”