Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 3:1-27

2 Wafalme 3:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yehoshafati wa Yuda, Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala Israeli, akatawala kutoka Samaria kwa muda wa miaka kumi na miwili. Yoramu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini yeye hakuwa mbaya kama baba na mama yake; maana alibomolea mbali mnara wa Baali uliofanywa na baba yake. Hata hivyo, Yoramu hakuacha dhambi kama mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyemtangulia ambaye alifanya dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Mfalme Mesha wa Moabu alikuwa mfuga kondoo, na kila mwaka alitoa ushuru kwa mfalme wa Israeli wanakondoo laki moja na sufu ya kondoo laki moja. Lakini Ahabu alipofariki, mfalme wa Moabu alimwasi. Kwa hiyo mfalme Yoramu akaondoka Samaria, akakusanya jeshi lote la Israeli. Akatuma ujumbe kwa mfalme Yehoshafati wa Yuda, akamwambia, “Mfalme wa Moabu ameniasi. Je, utashirikiana nami tupigane naye?” Mfalme Yehoshafati akamjibu, “Niko tayari! Mimi na wewe ni kitu kimoja; watu wangu ni kama wako, farasi wangu ni kama wako. Je, tutashambulia kutoka upande gani?” Yoramu akajibu, “Tutashambulia kutoka jangwa la Edomu.” Basi, mfalme Yoramu akaondoka pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kusafiri kwa muda wa siku saba, maji yakawaishia. Hawakuwa na maji kwa majeshi yao wala kwa wanyama wao. Hapo mfalme wa Israeli akasema, “Ole wetu! Mwenyezi-Mungu ametukusanya sote wafalme watatu atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.” Mfalme Yehoshafati akauliza, “Je, hakuna nabii yeyote hapa wa Mwenyezi-Mungu ambaye tunaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu?” Mtumishi mmoja wa mfalme Yoramu wa Israeli akajibu, “Elisha mwana wa Shafati yupo hapa. Yeye alikuwa mtumishi wa Elia.” Yehoshafati akasema, “Huyo ni nabii wa kweli.” Kisha wafalme hao watatu wakamwendea Elisha. Elisha akamwuliza mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda ukawatake shauri manabii ambao baba yako na mama yako waliwaendea.” Mfalme wa Israeli akajibu, “Sivyo! Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetuita sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.” Elisha akasema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu ambaye mimi ninamtumikia, naapa kwamba kama isingekuwa kwa heshima niliyo nayo kwa rafiki yako mfalme Yehoshafati wa Yuda, nisingekujali hata kidogo. Lakini sasa niletee mpiga kinanda.” Wakamletea mpiga kinanda. Ikawa alipopiga kinanda, nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elisha, akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Chimbeni mashimo kila mahali kote bondeni. Ingawa hamtaona upepo wala mvua, bonde litajaa maji, nanyi mtakunywa, nyinyi pamoja na ng'ombe wenu na wanyama wenu.’ Lakini hili si jambo gumu kwa Mwenyezi-Mungu; yeye atawapeni pia ushindi juu ya Moabu. Mtashinda kila mji wenye ngome na kila mji mzuri; mtaikata miti yao yote, mtaziba chemchemi zote za maji, na kuyaharibu mashamba yao yote yenye rutuba kwa kuyajaza mawe.” Kesho yake asubuhi, wakati wa kutambikia, maji yakatiririka kutoka upande wa Edomu na kujaa kila mahali bondeni. Wamoabu walipopata habari kwamba hao wafalme watatu wamekuja kuwashambulia, watu wote wawezao kuvaa silaha kuanzia vijana mpaka wazee, waliitwa, wakapewa silaha na kuwekwa mpakani tayari kwa vita. Walipoamka asubuhi iliyofuata, jua lilikuwa linametameta juu ya maji hayo; walipoyatazama yakaonekana kuwa mekundu kama damu. Wakasema, “Hii ni damu! Bila shaka hawa wafalme watatu wamepigana wao kwa wao na kuuana! Twendeni tukachukue nyara!” Lakini walipofika katika kambi ya Israeli, watu wa Israeli waliwashambulia, nao wakakimbia mbele yao. Watu wa Israeli wakawafuatia mpaka Moabu huku wakiwaua na kuibomoa miji yao. Kila walipopita penye shamba zuri, kila mtu alilirushia jiwe mpaka kila shamba likajaa mawe; kadhalika wakaziziba chemchemi zote za maji na kukata miti yote mizuri. Hatimaye, ukabaki mji mkuu wa Kir-haresethi peke yake, ambao pia wapiga kombeo waliuzingira na kuuteka. Mfalme wa Moabu alipoona kwamba vita vinamwendea vibaya, alichukua watu wake 700 wenye kupigana kwa mapanga, akikusudia kupenya majeshi ya adui zake mkabala na mfalme wa Edomu, lakini hakufaulu. Hapo akamchukua mwanawe wa kwanza ambaye angekuwa mfalme mahali pake, akamtoa kuwa sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Watu wa Israeli walipoona hayo, wakachukizwa mno. Wakauacha mji huo na kurudi nchini kwao.

2 Wafalme 3:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na nane wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka kumi na miwili. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA; ila si kama baba yake na kama mama yake; maana akaiondoa ile nguzo ya Baali aliyoifanya baba yake. Pamoja na hayo alishikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwa hizo aliwakosesha Israeli; wala hakuziacha. Basi Mesha, mfalme wa Moabu, alikuwa mfuga kondoo; naye alikuwa akimlipa mfalme wa Israeli wana-kondoo elfu mia moja na sufu ya kondoo dume elfu mia moja. Lakini ikawa, Ahabu alipokufa, mfalme wa Moabu akamwasi mfalme wa Israeli. Akatoka wakati ule ule mfalme Yoramu katika Samaria, akawahesabu Israeli wote. Akaenda akatuma kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akasema, Mfalme wa Moabu ameniasi; je! Utakwenda pamoja nami tupigane na Moabu? Akasema, Nitakwenda; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako. Akauliza, Njia ipi tuiendee? Akajibu, Njia ya jangwa la Edomu. Basi mfalme wa Israeli akaenda, na mfalme wa Yuda, na mfalme wa Edomu; wakazunguka mwendo wa siku saba; wala hapakuwa na maji kwa jeshi, wala kwa wanyama waliowafuata. Mfalme wa Israeli akasema, Ole wetu! Kwani BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hakuna nabii yeyote hapa wa BWANA ili tumwulize yeye shauri la BWANA? Akajibu mtumishi mmoja wa mfalme wa Israeli, akasema, Yupo hapa Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akimimina maji juu ya mikono yake Eliya. Yehoshafati akasema, Neno la BWANA analo huyu. Basi mfalme wa Israeli, na Yehoshafati, na mfalme wa Edomu, wakamshukia. Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu. Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe. Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake. Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki. Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng'ombe zenu, na wanyama wenu. Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu. Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe. Ikawa asubuhi, wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama, maji yakaja kwa njia ya Edomu, hata nchi ikajaa maji. Basi Wamoabi wote waliposikia ya kuwa wafalme hao wamekwea ili kupigana nao, walijikusanya pamoja, wote wawezao kuvaa silaha, na wenye umri zaidi, wakasimama mpakani. Wakaamka asubuhi na mapema, na hilo jua likametameta juu ya maji, na Wamoabi wakayaona yale maji yaliyowaelekea kuwa ni mekundu kama damu. Wakasema, Ndiyo damu hii; bila shaka hao wafalme wameharibika, wamepigana wenyewe kwa wenyewe; basi sasa, enyi Wamoabi, nyara hizo! Hata walipokuja kambini mwa Israeli, Waisraeli wakainuka wakawapiga Wamoabi, hata wakakimbia mbele yao; wakaendelea wakiwapiga Wamoabi hadi kwao. Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga. Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.

2 Wafalme 3:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na nane wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka kumi na miwili. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA; ila si kama baba yake na kama mama yake; maana akaiondoa ile nguzo ya Baali aliyoifanya baba yake. Pamoja na hayo alishikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwa hizo aliwakosesha Israeli; wala hakuziacha. Basi Mesha, mfalme wa Moabu, alikuwa mfuga kondoo; naye alikuwa akimlipa mfalme wa Israeli sufu ya wana-kondoo elfu mia, na ya kondoo waume elfu mia. Lakini ikawa, Ahabu alipokufa, mfalme wa Moabu akamwasi mfalme wa Israeli. Akatoka wakati ule ule mfalme Yoramu katika Samaria, akawahesabu Israeli wote. Akaenda akatuma kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akasema, Mfalme wa Moabu ameniasi; je! Utakwenda pamoja nami tupigane na Moabu? Akasema, Nitakwenda; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi zangu ni kama farasi zako. Akauliza, Njia ipi tuiendee? Akajibu, Njia ya jangwa la Edomu. Basi mfalme wa Israeli akaenda, na mfalme wa Yuda, na mfalme wa Edomu; wakazunguka mwendo wa siku saba; wala hapakuwa na maji kwa jeshi, wala kwa wanyama waliowafuata. Mfalme wa Israeli akasema, Ole wetu! Kwani BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hapana hapa nabii wa BWANA, ili tumwulize BWANA kwa yeye? Akajibu mtumishi mmoja wa mfalme wa Israeli, akasema, Yupo hapa Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akimimina maji juu ya mikono yake Eliya. Yehoshafati akasema, Neno la BWANA analo huyu. Basi mfalme wa Israeli, na Yehoshafati, na mfalme wa Edomu, wakamshukia. Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu. Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe. Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake. Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki. Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng’ombe zenu, na wanyama wenu. Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu. Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe. Ikawa asubuhi, wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama, maji yakaja kwa njia ya Edomu, hata nchi ikajaa maji. Basi Wamoabi wote waliposikia ya kuwa wafalme hao wamekwea ili kupigana nao, walijikusanya pamoja, wote wawezao kuvaa silaha, na wenye umri zaidi, wakasimama mpakani. Wakaamka asubuhi na mapema, na hilo jua likameta-meta juu ya maji, na Wamoabi wakayaona yale maji yaliyowaelekea kuwa ni mekundu kama damu. Wakasema, Ndiyo damu hii; bila shaka hao wafalme wameharibika, wamepigana kila mtu na mwenziwe; basi sasa, enyi Wamoabi, nyara hizo! Hata walipokuja matuoni kwa Israeli, Waisraeli wakainuka wakawapiga Wamoabi, hata wakakimbia mbele yao; wakaendelea wakiwapiga-piga Wamoabi hata kwao. Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga. Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.

2 Wafalme 3:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Yehoramu mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, naye akatawala kwa miaka kumi na mbili. Akafanya maovu machoni pa BWANA, lakini sio kama baba yake na mama yake walivyokuwa wamefanya. Akaondoa nguzo ya ibada ya Baali ambayo baba yake alikuwa ameitengeneza. Hata hivyo akashikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, wala hakuziacha. Basi Mesha mfalme wa Moabu alikuwa mfuga kondoo; naye akatakiwa kumlipa mfalme wa Israeli ushuru wa wana-kondoo elfu mia moja, na sufu ya kondoo dume elfu mia moja. Lakini baada ya Ahabu kufa, mfalme wa Moabu aliasi dhidi ya mfalme wa Israeli. Kwa hiyo wakati ule Mfalme Yehoramu akaondoka kutoka Samaria na kukusanya Israeli yote tayari kwenda vitani. Akapeleka pia ujumbe ufuatao kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda: “Mfalme wa Moabu ameasi dhidi yangu. Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Moabu?” Akajibu, “Nitaenda pamoja nawe. Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.” Akauliza, “Je, tutashambulia kupitia njia gani?” Akajibu, “Kupitia Jangwa la Edomu.” Hivyo mfalme wa Israeli akaondoka akiwa pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kuzunguka kwa siku saba, jeshi likawa limeishiwa maji kwa matumizi yao na kwa ajili ya wanyama waliokuwa nao. Mfalme wa Israeli akapaza sauti, akasema, “Nini! Je, BWANA ametuita sisi wafalme watatu ili tu kututia mikononi mwa Moabu?” Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa BWANA hapa, ili tuweze kumuuliza BWANA kupitia kwake?” Afisa mmoja wa mfalme wa Israeli akajibu, “Elisha mwana wa Shafati yuko hapa. Ndiye alikuwa akimimina maji juu ya mikono ya Eliya.” Yehoshafati akasema, “Neno la BWANA liko pamoja naye.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli na Yehoshafati pamoja na mfalme wa Edomu wakamwendea. Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda kwa manabii wa baba yako na manabii wa mama yako.” Mfalme wa Israeli akajibu, “La, sivyo, kwa sababu ni BWANA ametuita pamoja sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa Moabu.” Elisha akasema, “Hakika kama BWANA wa majeshi aishivyo, ninayemtumikia, kama si kwa heshima niliyo nayo kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, nisingekujali hata kidogo. Lakini sasa, nileteeni mpiga kinubi.” Mpiga kinubi alipokuwa akipiga, mkono wa BWANA ukaja juu ya Elisha, naye akasema, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA, ‘Chimbeni bonde hili lijae mahandaki.’ Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo BWANA: Hamtaona upepo wala mvua, lakini bonde hili litajaa maji, nanyi pamoja na ngʼombe wenu na wanyama wenu wengine mtakunywa. Hili ni jambo rahisi machoni pa BWANA. Pia ataitia Moabu mikononi mwenu. Mtaushinda kila mji wenye ngome na kila mji mkubwa. Mtakata kila mti ulio mzuri, mtaziba chemchemi zote, na kuharibu kila shamba zuri kwa mawe.” Kesho yake asubuhi, karibu na wakati wa kutoa dhabihu ya asubuhi, tazama, maji yakawa yanatiririka kutoka upande wa Edomu! Nayo nchi ikajaa maji. Basi Wamoabu wote walikuwa wamesikia kuwa wale wafalme wamekuja kupigana dhidi yao. Hivyo kila mtu, kijana na mzee, ambaye angeweza kushika silaha akaitwa na kuwekwa mpakani. Walipoamka asubuhi na mapema, jua likawa linamulika juu ya maji. Wamoabu waliokuwa upande wa pili wakaona maji ni mekundu, kama damu. Wamoabu wakasema, “Ile ni damu! Lazima hao wafalme wamepigana na kuchinjana wao kwa wao. Sasa Moabu, twendeni tukateke nyara!” Lakini Wamoabu walipofika kwenye kambi ya Israeli, Waisraeli wakainuka na kuwapiga hata wakakimbia. Nao Waisraeli wakaivamia nchi na kuwachinja Wamoabu. Wakaiharibu miji, kila mtu akatupa jiwe juu ya kila shamba zuri hadi likafunikwa. Wakaziba chemchemi zote na kukata kila mti mzuri. Kir-Haresethi peke yake ndio uliobaki na mawe yake yakiwa mahali pake. Lakini hata hivyo watu waliokuwa na makombeo wakauzunguka na kuushambulia. Mfalme wa Moabu alipoona kuwa vita vimekuwa vikali dhidi yake, akachukua watu mia saba wenye panga ili kuingia kwa mfalme wa Edomu, lakini wakashindwa. Ndipo akamchukua mwanawe mzaliwa wake wa kwanza, ambaye angekuwa mfalme baada yake, akamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Ghadhabu ikawa kubwa dhidi ya Israeli; wakajiondoa kwake na kurudi katika nchi yao wenyewe.