Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 23:26-37

2 Wafalme 23:26-37 Biblia Habari Njema (BHN)

Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu hakuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, kwa sababu hasira yake iliwaka dhidi ya Yuda kwa ajili ya vitendo vya kukasirisha, ambavyo Manase alifanya dhidi yake. Naye Mwenyezi-Mungu alisema, “Nitawafukuza watu wa Yuda kutoka mbele yangu kama vile nilivyofanya kwa watu wa Israeli; nitaukataa mji wa Yerusalemu ambao niliuchagua niliposema, ‘Jina langu litakuwa humo.’” Matendo mengine ya Yosia na yale yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Wakati wa kutawala kwake, Farao Neko wa Misri alikwenda mpaka mto Eufrate ili kukutana na mfalme wa Ashuru. Naye mfalme Yosia akaondoka ili kupambana naye; lakini Farao Neko alipomwona alimuua kule Megido. Maofisa wake wakaibeba maiti yake katika gari na kuirejesha Yerusalemu walikomzika katika kaburi lake mwenyewe. Kisha watu wa Yuda wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia wakampaka mafuta na kumtawaza kuwa mfalme mahali pa baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, akatawala kwa miezi mitatu huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Hamutali binti Yeremia wa Libna. Yehoahazi alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama babu zake walivyofanya. Ili asiendelee kutawala huko Yerusalemu, Farao Neko alimtia nguvuni huko Ribla katika nchi ya Hamathi, akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za madini ya fedha na kilo 34 za dhahabu. Farao Neko akamtawaza Eliakimu mwana wa mfalme Yosia mahali pa baba yake Yosia, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Lakini alimchukua Yehoahazi mbali mpaka Misri na kufia huko. Mfalme Yehoyakimu alimpa Farao fedha na dhahabu, lakini aliitoza nchi kodi ili aweze kutekeleza matakwa ya Farao ya kupewa fedha. Aliwatoza wananchi fedha na dhahabu. Kila mmoja alitoa kiasi alichokadiria mfalme, naye akampa Farao Neko. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, na alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake lilikuwa Zebida binti Pedaya wa Ruma. Yehoyakimu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama waliyoyafanya babu zake wote.

2 Wafalme 23:26-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini BWANA hakuuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, ambayo kwayo hasira yake iliwaka juu ya Yuda, kwa sababu ya machukizo yote ambayo Manase amemchukiza. BWANA akasema Nitawahamisha Yuda pia mbali nami, kama nilivyowahamisha Israeli, nami nitautupa mji huu niliouchagua, naam, Yerusalemu, na nyumba ile niliyoinena, Jina langu litakuwa humo. Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Katika siku zake, Farao Neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana na mfalme wa Ashuru, akafika mto Frati; naye mfalme Yosia akaenda kupigana naye; naye mfalme wa Misri akamwua huko Megido, hapo alipoonana naye. Watumishi wake wakamchukua garini, amekwisha kufa, kutoka Megido, wakamleta Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake mwenyewe. Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta, wakamtawaza awe mfalme badala ya baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali binti Yeremia wa Libna. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake. Naye Farao Neko akamfunga huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ili asitawale huko Yerusalemu. Akaitoza nchi kodi talanta mia moja za fedha na talanta ya dhahabu. Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia awe mfalme mahali pa Yosia babaye, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu, lakini akamwondoa Yehoahazi; akaenda naye Misri, naye akafa huko. Na Yehoyakimu akampa Farao dhahabu na fedha; lakini akaitoza nchi kodi, ili apate kutoa zile fedha kwa amri yake Farao; akawatoza fedha na dhahabu watu wa nchi, kila mtu kwa kodi yake, ili ampe Farao Neko. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Zebida binti Pedaya wa Ruma. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.

2 Wafalme 23:26-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Walakini BWANA hakuuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, ambayo kwayo hasira yake iliwaka juu ya Yuda, kwa sababu ya machukizo yote ambayo Manase amemchukiza. BWANA akasema Nitawahamisha Yuda pia mbali nami, kama nilivyowahamisha Israeli, nami nitautupa mji huu niliouchagua, naam, Yerusalemu, na nyumba ile niliyoinena, Jina langu litakuwa humo. Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Katika siku zake, Farao-neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana na mfalme wa Ashuru, akafika mto Frati; naye mfalme Yosia akaenda kupigana naye; naye mfalme wa Misri akamwua huko Megido, hapo alipoonana naye. Watumishi wake wakamchukua garini, amekwisha kufa, kutoka Megido, wakamleta Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake mwenyewe. Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta, wakamtawaza awe mfalme badala ya baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali binti Yeremia wa Libna. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake. Naye Farao-neko akamfunga huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ili asitawale huko Yerusalemu. Akaitoza nchi kodi talanta mia za fedha na talanta ya dhahabu. Farao-neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia awe mfalme mahali pa Yosia babaye, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu, lakini akamwondoa Yehoahazi; akaenda naye Misri, naye akafa huko. Na Yehoyakimu akampa Farao dhahabu na fedha; lakini akaitoza nchi kodi, ili apate kutoa zile fedha kwa amri yake Farao; akawatoza fedha na dhahabu watu wa nchi, kila mtu kwa kodi yake, ili ampe Farao-neko. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Zebida binti Pedaya wa Ruma. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.

2 Wafalme 23:26-37 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hata hivyo, BWANA hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha. Hivyo BWANA akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’” Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda hadi Mto Frati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumuua huko Megido. Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake katika gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu, wakamzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakampaka mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna. Akafanya maovu machoni mwa BWANA, kama baba zake walivyofanya. Farao Neko akamfunga kwa minyororo huko Ribla katika nchi ya Hamathi ili asiweze kutawala huko Yerusalemu, naye akatoza kodi ya talanta mia moja za fedha, na talanta moja ya dhahabu katika Yuda. Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, na kulibadilisha jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini akamchukua Yehoahazi na kumpeleka Misri, naye akafia huko. Yehoyakimu akamlipa Farao Neko ile fedha na dhahabu aliyodai. Ili kuweza kufanya hivyo, Yehoyakimu akatoza nchi kodi na kulipiza fedha na dhahabu kutoka kwa watu wa nchi kulingana na makadirio ya mapato yao. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Zebida binti Pedaya kutoka Ruma. Naye akafanya maovu machoni mwa BWANA, kama baba zake walivyokuwa wamefanya.