Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 23:1-7

2 Wafalme 23:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha mfalme alituma wajumbe, nao wakamkusanyia viongozi wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Naye mfalme akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu akifuatana na watu wote wa Yuda na wakazi wote wa Yerusalemu, na makuhani pamoja na manabii, watu wote wadogo kwa wakubwa. Basi, akawasomea maneno ya kitabu cha agano kilichopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu mfalme akasimama karibu na nguzo na kufanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu, kumfuata Mwenyezi-Mungu, kushika amri zake, maamuzi na masharti yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kutenda maneno yote ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hicho cha agano. Watu wote wakaungana katika kufanya agano. Kisha Yosia akaamuru kuhani mkuu Hilkia na makuhani wasaidizi wake na mabawabu watoe katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitu vilivyotengenezwa kwa ajili ya Baali, Ashera na kwa ajili ya sayari; aliviteketeza nje ya Yerusalemu katika bonde la Kidroni na kupeleka majivu yake huko Betheli. Kisha akawaondoa makuhani wote waliobarikiwa na wafalme wa Yuda ili kufukiza ubani katika mahali pa kuabudia katika miji ya Yuda na kuzunguka Yerusalemu; pia na wale waliofukiza ubani kwa Baali, jua, mwezi, nyota na sayari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliondoa Ashera kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nje ya Yerusalemu, akaipeleka mpaka kijito cha Kidroni. Huko akaiteketeza na kuisaga mpaka ikawa mavumbi, nayo mavumbi yake akayatawanya juu ya makaburi ya watu. Alibomoa nyumba za mahanithi zilizokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, mahali ambamo wanawake walifuma mapazia ya Ashera.

2 Wafalme 23:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya Kitabu cha Agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile. Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akaviteketeza kwa moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli. Akawaondosha wale makuhani walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni. Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuipondaponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu. Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.

2 Wafalme 23:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile. Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli. Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni. Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu. Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.

2 Wafalme 23:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda kwenda hekaluni mwa BWANA pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, kilichokuwa kimepatikana katika Hekalu la BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za BWANA: kwamba atamfuata BWANA na kuzishika amri zake, maagizo na sheria zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, na hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka Hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu hadi Betheli. Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka Hekalu la BWANA, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wasio na cheo. Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada, zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA, nyumba ambazo wanawake walifumia pazia kwa ajili ya Ashera.