Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 23:1-10

2 Wafalme 23:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha mfalme alituma wajumbe, nao wakamkusanyia viongozi wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Naye mfalme akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu akifuatana na watu wote wa Yuda na wakazi wote wa Yerusalemu, na makuhani pamoja na manabii, watu wote wadogo kwa wakubwa. Basi, akawasomea maneno ya kitabu cha agano kilichopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu mfalme akasimama karibu na nguzo na kufanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu, kumfuata Mwenyezi-Mungu, kushika amri zake, maamuzi na masharti yake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, kutenda maneno yote ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hicho cha agano. Watu wote wakaungana katika kufanya agano. Kisha Yosia akaamuru kuhani mkuu Hilkia na makuhani wasaidizi wake na mabawabu watoe katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitu vilivyotengenezwa kwa ajili ya Baali, Ashera na kwa ajili ya sayari; aliviteketeza nje ya Yerusalemu katika bonde la Kidroni na kupeleka majivu yake huko Betheli. Kisha akawaondoa makuhani wote waliobarikiwa na wafalme wa Yuda ili kufukiza ubani katika mahali pa kuabudia katika miji ya Yuda na kuzunguka Yerusalemu; pia na wale waliofukiza ubani kwa Baali, jua, mwezi, nyota na sayari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliondoa Ashera kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nje ya Yerusalemu, akaipeleka mpaka kijito cha Kidroni. Huko akaiteketeza na kuisaga mpaka ikawa mavumbi, nayo mavumbi yake akayatawanya juu ya makaburi ya watu. Alibomoa nyumba za mahanithi zilizokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, mahali ambamo wanawake walifuma mapazia ya Ashera. Akakusanya makuhani wote kutoka miji ya Yuda na akapatia najisi mahali pa juu makuhani walikofukiza ubani, kutoka Geba mpaka Beer-sheba; naye akabomoa mahali pa juu palipokuwa upande wa kushoto wa lango la mji penye malango yaliyokuwa kwenye njia ya kuingilia lango la Yoshua mtawala wa mji. Makuhani hao hawakufikia madhabahu ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu, lakini walikula mikate isiyotiwa chachu waliyopewa na jamaa zao. Mfalme Yosia pia alipatia najisi mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipoitwa Tofethi katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu yeyote asimchome mwanawe au bintiye kuwa tambiko kwa Moleki.

2 Wafalme 23:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya Kitabu cha Agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile. Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akaviteketeza kwa moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli. Akawaondosha wale makuhani walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni. Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuipondaponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu. Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera. Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, mtawala wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji. Lakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa BWANA katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao. Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki.

2 Wafalme 23:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile. Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli. Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni. Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu. Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera. Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, liwali wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji. Walakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa BWANA katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao. Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki.

2 Wafalme 23:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda kwenda hekaluni mwa BWANA pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, kilichokuwa kimepatikana katika Hekalu la BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za BWANA: kwamba atamfuata BWANA na kuzishika amri zake, maagizo na sheria zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, na hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka Hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu hadi Betheli. Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka Hekalu la BWANA, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wasio na cheo. Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada, zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA, nyumba ambazo wanawake walifumia pazia kwa ajili ya Ashera. Yosia akawaleta makuhani wote wa BWANA kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji. Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia hawakuhudumu katika madhabahu ya BWANA katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu pamoja na ndugu zao. Kisha mfalme akapanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe wa kiume au wa kike katika moto kwa Moleki.