2 Wafalme 2:9-18
2 Wafalme 2:9-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Walipofika ngambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.” Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.” Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli. Elisha alipoona tukio hilo akalia, “Baba yangu, baba yangu! Gari la Israeli na wapandafarasi wake!” Basi, Elisha hakumwona tena Elia. Ndipo Elisha alipoyashika mavazi yake na kuyararua vipande viwili. Kisha akaliokota vazi la Elia lililomwangukia, akarudi na kusimama ukingoni mwa mto Yordani. Akayapiga maji kwa vazi la Elia akisema, “Yuko wapi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Elia?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika sehemu mbili, naye akavuka hadi ngambo. Wale wanafunzi wa manabii kutoka Yeriko walipomwona, walisema, “Roho ya Elia iko kwa Elisha.” Basi, wakaenda kumlaki, wakasujudu mbele yake. Wakamwambia, “Sisi watumishi wako tunao mashujaa hamsini; tafadhali waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Ikiwa roho ya Mwenyezi-Mungu imembeba na kumtupa juu ya mlima fulani au bondeni.” Elisha akajibu, “La, msiwatume.” Lakini wao waliposisitiza mpaka akaona haya, aliwaambia “Watumeni.” Hivyo wakawatuma watu hamsini, wakaenda wakamtafuta kila mahali kwa muda wa siku tatu wasimwone. Kisha wakarudi kwa Elisha aliyekuwa anawangojea huko Yeriko. Elisha akawauliza, “Je, sikuwaambieni msiende?”
2 Wafalme 2:9-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lolote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake. Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda Roho ya BWANA imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume. Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone. Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende?
2 Wafalme 2:9-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake. Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda roho ya BWANA imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume. Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone. Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende?
2 Wafalme 2:9-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?” Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.” Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hutalipata.” Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la farasi la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. Elisha aliliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akaishika nguo yake na kuirarua vipande viwili. Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani. Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa BWANA, Mungu wa Eliya?” Elisha alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka. Wale wana wa manabii kutoka Yeriko waliokuwa wakitazama wakasema, “Roho ya Eliya inamkalia Elisha.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi chini mbele yake. Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa BWANA amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.” Elisha akajibu, “Hapana, msiwatume.” Lakini wakasisitiza, hata akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata. Walipomrudia Elisha, aliyekuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?”