Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 2:1-25

2 Wafalme 2:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Ikawa wakati ulipofika ambapo Mwenyezi-Mungu alitaka kumchukua Elia mbinguni katika upepo wa kisulisuli, Elia na Elisha walikuwa njiani, wakitoka Gilgali. Baadaye walipokuwa njiani, Elia alimwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Betheli.” Lakini Elisha akamwambia, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo, sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja hadi Betheli. Wanafunzi wa manabii waliokuwa huko wakamwendea Elisha, wakamwuliza, “Je, unajua kwamba leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.” Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende Yeriko.” Lakini Elisha akakataa akisema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja mpaka Yeriko. Wanafunzi wa manabii huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumwuliza, “Je, unajua kwamba hivi leo Mwenyezi-Mungu atamchukua bwana wako?” Elisha akawajibu, “Naam! Najua; nyamazeni.” Kisha Elia akamwambia Elisha, “Tafadhali wewe kaa hapa; Mwenyezi-Mungu amenituma niende mtoni Yordani.” Lakini Elisha akasema, “Naapa kwamba kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe mwenyewe uishivyo sitakuacha.” Basi, wakaenda pamoja. Manabii hamsini wakawafuata mpaka mtoni Yordani. Elia na Elisha wakasimama karibu na mto, nao manabii wakasimama mbali kidogo. Elia akalivua vazi lake, akalikunja na kuyapiga maji, maji yakagawanyika katika sehemu mbili, nao wakavuka hadi ngambo ya pili, wakapitia mahali pakavu. Walipofika ngambo, Elia akamwambia Elisha, “Niambie unalotaka nikufanyie kabla sijaondolewa kwako.” Elisha akamwambia, “Naomba sehemu maradufu ya roho yako.” Elia akajibu, “Ombi lako ni gumu, hata hivyo utakipokea kipawa changu hicho ikiwa utaniona wakati nitakapoondolewa kwako; lakini usiponiona, basi hutapewa.” Walipokuwa wanatembea na kuongea, ghafla, gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto; likawatenganisha; naye Elia akachukuliwa mbinguni katika kisulisuli. Elisha alipoona tukio hilo akalia, “Baba yangu, baba yangu! Gari la Israeli na wapandafarasi wake!” Basi, Elisha hakumwona tena Elia. Ndipo Elisha alipoyashika mavazi yake na kuyararua vipande viwili. Kisha akaliokota vazi la Elia lililomwangukia, akarudi na kusimama ukingoni mwa mto Yordani. Akayapiga maji kwa vazi la Elia akisema, “Yuko wapi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Elia?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika sehemu mbili, naye akavuka hadi ngambo. Wale wanafunzi wa manabii kutoka Yeriko walipomwona, walisema, “Roho ya Elia iko kwa Elisha.” Basi, wakaenda kumlaki, wakasujudu mbele yake. Wakamwambia, “Sisi watumishi wako tunao mashujaa hamsini; tafadhali waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Ikiwa roho ya Mwenyezi-Mungu imembeba na kumtupa juu ya mlima fulani au bondeni.” Elisha akajibu, “La, msiwatume.” Lakini wao waliposisitiza mpaka akaona haya, aliwaambia “Watumeni.” Hivyo wakawatuma watu hamsini, wakaenda wakamtafuta kila mahali kwa muda wa siku tatu wasimwone. Kisha wakarudi kwa Elisha aliyekuwa anawangojea huko Yeriko. Elisha akawauliza, “Je, sikuwaambieni msiende?” Baadaye watu wa Yeriko walimwendea Elisha, wakamwambia, “Bwana, kama uonavyo mji huu ni mzuri, lakini maji tuliyo nayo ni mabaya na yanasababisha mimba kuharibika.” Elisha akawaambia, “Tieni chumvi ndani ya bakuli jipya, kisha mniletee.” Nao wakamletea. Elisha akaenda kwenye chemchemi ya maji, akatupa chumvi hiyo ndani na kusema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeyafanya maji haya kuwa yenye kufaa; tangu sasa hayatasababisha vifo au kutoa mimba.” Na maji hayo yamekuwa ya kufaa mpaka leo, kama alivyosema Elisha. Elisha aliondoka Yeriko, akaenda Betheli. Alipokuwa njiani, vijana fulani walitoka mjini wakaanza kumzomea wakisema, “Nenda zako, nenda zako mzee kipara!” Elisha aligeuka akawatazama na kuwalaani kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Dubu wawili majike wakatoka mwituni, wakawararua vijana arubaini na wawili miongoni mwao. Elisha akaendelea na safari yake mpaka mlima Karmeli na kutoka huko akarudi Samaria.

2 Wafalme 2:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, hapo BWANA alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha. Eliya akamwambia Elisha, Tafadhali, kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Betheli. Elisha akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha, Basi wakashuka mpaka Betheli. Basi wana wa manabii, waliokuwako Betheli, wakatoka kuonana na Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akasema, Naam, najua; nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Nao wakafika Yeriko. Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Yordani. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea mbele wote wawili. Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani. Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lolote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake. Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda Roho ya BWANA imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume. Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone. Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende? Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena. Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa! Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la BWANA. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arubaini na wawili miongoni mwao. Akatoka huko akaenda mlima wa Karmeli, na toka huko akarudi mpaka Samaria.

2 Wafalme 2:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, hapo BWANA alipopenda kumpandisha Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha. Eliya akamwambia Elisha, Tafadhali, kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Betheli. Elisha akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha, Basi wakashuka mpaka Betheli. Basi wana wa manabii, waliokuwako Betheli, wakatoka kuonana na Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akasema, Naam, najua; nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana BWANA amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Nao wakafika Yeriko. Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa BWANA atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni. Eliya akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana BWANA amenituma niende mpaka Yordani. Akasema, Kama BWANA aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea mbele wote wawili. Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani. Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake. Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda roho ya BWANA imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume. Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone. Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende? Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena. Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa! Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la BWANA. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao. Akatoka huko akaenda mlima wa Karmeli, na toka huko akarudi mpaka Samaria.

2 Wafalme 2:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya na Elisha walikuwa njiani wakitoka Gilgali. Eliya akamwambia Elisha, “Kaa hapa. BWANA amenituma Betheli.” Lakini Elisha akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja. Wana wa manabii waliokuwa Betheli wakamjia Elisha na kumuuliza, “Je, unajua kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?” Elisha akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze kuhusu jambo hilo.” Kisha Eliya akamwambia, “Baki hapa, Elisha. BWANA amenituma Yeriko.” Naye akajibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko. Wana wa manabii waliokuwa Yeriko wakamwendea Elisha na kumuuliza, “Je, unajua kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?” Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.” Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa. BWANA amenituma kwenda Yordani.” Naye akamjibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja. Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali Eliya na Elisha waliposimama kando ya Mto Yordani. Eliya akatoa vazi lake, akalikunja na kupiga maji nalo. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu. Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?” Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.” Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hutalipata.” Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la farasi la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. Elisha aliliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akaishika nguo yake na kuirarua vipande viwili. Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani. Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa BWANA, Mungu wa Eliya?” Elisha alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka. Wale wana wa manabii kutoka Yeriko waliokuwa wakitazama wakasema, “Roho ya Eliya inamkalia Elisha.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi chini mbele yake. Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa BWANA amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.” Elisha akajibu, “Hapana, msiwatume.” Lakini wakasisitiza, hata akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata. Walipomrudia Elisha, aliyekuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?” Watu wa mji wakamwambia Elisha, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu anavyoona, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haina mazao.” Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea. Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ” Nayo yale maji yakaponywa hadi leo, sawasawa na neno la Elisha alilokuwa amesema. Kutoka huko Elisha akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakasema, “Paa, wewe mwenye upara! Paa, wewe mwenye upara!” Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la BWANA. Kisha dubu jike wawili wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao. Naye akaondoka huko, akaenda Mlima Karmeli, na kutoka huko akarudi Samaria.