Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 17:1-41

2 Wafalme 17:1-41 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa enzi ya mfalme Ahazi wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka tisa. Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa siyo kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Mfalme Shalmanesa wa Ashuru alimshambulia; naye Hoshea akawa mtumishi wake na kumlipa ushuru. Lakini wakati mmoja Hoshea alituma wajumbe kwa mfalme wa Misri akiomba msaada; ndipo akaacha kulipa ushuru kwa mfalme Shalmanesa wa Ashuru kama alivyozoea kufanya kila mwaka. Shalmanesa alipoona hivi alimfunga Hoshea kwa minyororo na kumweka gerezani. Kisha mfalme wa Ashuru akaivamia nchi nzima na kuufikia mji wa Samaria na kuuzingira kwa muda wa miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea, mfalme wa Ashuru aliuteka Samaria, na kuwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru, baadhi yao akawaweka katika mji wa Hala, wengine karibu na mto Habori, mto Gozani na wengine katika miji ya Media. Haya yote yalitendeka kwa sababu watu wa Israeli walimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, ambaye aliwatoa kutoka mikononi mwa mfalme wa Misri, pia waliabudu miungu mingine, na kufuata njia za mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli, na kufanya matendo ya wafalme wa Israeli waliyoyaingiza nchini. Watu wa Israeli walitenda kwa siri mambo yasiyokuwa mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walijenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ya uongo katika kila mji, kuanzia mnara wa walinzi mashambani hadi katika mji wenye ngome. Juu ya kila kilima na chini ya kila mti wenye majani mabichi, walijenga nguzo za mawe na sanamu za mungu wa kike Ashera, na wakafukiza ubani kwenye madhabahu zote za miungu ya uongo kufuatia desturi za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao maovu, na walitumikia sanamu ambazo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza, akisema, “Msifanye hivyo.” Mwenyezi-Mungu alituma manabii na waonaji kuionya Israeli na Yuda akisema, “Acheni njia zenu mbaya mkatii amri zangu na maagizo yangu kufuatana na sheria nilizowapa babu zenu, na ambazo niliwapeni kupitia kwa watumishi wangu manabii.” Lakini wao hawakutii; walikuwa wagumu kama babu zao ambao hawakumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walikataa kutii maagizo yake; hawakushika agano alilofanya na babu zao; licha ya kupuuza maonyo yake, waliabudu sanamu zisizokuwa na maana mpaka hata wao wenyewe hawakuwa na maana tena; walifuata desturi za mataifa yaliyowazunguka: Walipuuza amri za Mwenyezi-Mungu; wala hawakuzizingatia. Walivunja amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakatengeneza sanamu za miungu ya ndama wawili wa kusubu; vilevile wakatengeneza sanamu za mungu wa kike Ashera wakaabudu na vitu vyote vya angani na wakamtumikia Baali. Waliwatambika watoto wao wa kiume na wa kike kwa miungu ya uongo; wakataka shauri kwa watabiri na wachawi. Walinuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakamkasirisha sana. Basi, Mwenyezi-Mungu akawakasirikia sana watu wa Israeli na kuwafukuza kabisa mbele yake; hakuacha mtu isipokuwa kabila la Yuda peke yake. Lakini hata watu wa Yuda hawakutii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao; bali walifuata desturi zilizoletwa na watu wa Israeli. Mwenyezi-Mungu aliwakataa Waisraeli wote; akawaadhibu na kuwaacha mikononi mwa adui wakali, na kisha akawafukuza mbele yake. Baada ya Mwenyezi-Mungu kutenga watu wa Israeli kutoka ukoo wa Daudi, walimtawaza Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme. Naye Yeroboamu aliwafanya watu wa Israeli kumwacha Mwenyezi-Mungu na kutenda dhambi kubwa sana. Waisraeli walitenda dhambi alizotenda Yeroboamu; hawakuweza kuziacha, hadi hatimaye Mwenyezi-Mungu akawafukuza kutoka mbele yake, kama vile alivyokuwa amesema kupitia kwa watumishi wake wote manabii. Kwa hiyo watu wa Israeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe mpaka Ashuru ambako wanakaa hata sasa. Kisha mfalme wa Ashuru akachukua watu kutoka Babuloni, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria mahali pa watu wa Israeli waliopelekwa uhamishoni. Wakaitwaa miji hiyo na kukaa humo. Basi ilitokea kwamba walipoanza kukaa humo, hawakumwabudu Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akatuma simba miongoni mwao, nao wakawaua baadhi yao. Halafu watu walimwambia mfalme wa Ashuru, “Mataifa uliyochukua na kuyaweka katika miji ya Samaria hayakujua hukumu za Mungu wa nchi hiyo, kwa hiyo Mungu huyo alituma simba ambao wanawaua.” Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru, “Mrudishe kuhani mmoja kati ya wale tuliowaleta mateka; mrudishe aende na kukaa huko, ili awafundishe watu sheria ya Mungu wa nchi hiyo.” Kwa hiyo mmoja wa makuhani waliotekwa nyara toka Samaria alikwenda na kukaa Betheli, na huko aliwafundisha watu jinsi ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Lakini mataifa yote katika miji yalimoishi yalijitengenezea miungu yao na kuiweka mahali pa juu ambako watu wa Samaria walikuwa wametengeneza. Watu wa Babuloni walitengeneza vinyago vya Sukoth-benothi; Wakuthi vinyago vya Nergali; Wahamathi vinyago vya Ashima; Waiva vinyago vya Nibhazi na Tartaki; na Wasefarvaimu walitoa watoto wao kuwa sadaka za kuteketezwa kwa miungu yao Adrameleki na Anameleki. Watu hawa vilevile walimwabudu Mwenyezi-Mungu. Waliteua kutoka kati yao watu wa kila aina na kuwafanya makuhani kutumika katika mahali pa juu na kutoa sadaka huko kwa niaba yao. Hivi walimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini wakati huohuo waliwaabudu pia miungu yao waliyoichukua kutoka nchi zao. Hata sasa wanatenda kama walivyofanya hapo awali. Hawamwabudu Mwenyezi-Mungu, na wala hawafuati masharti, maagizo, sheria au amri ambazo yeye Mwenyezi-Mungu aliwaamuru wana wa Yakobo; ambaye alimpa jina Israeli. Mwenyezi-Mungu alikuwa amefanya agano nao na kuwaamuru, “Msiabudu miungu mingine; msiisujudie, msiitumikie wala msiitambikie. Mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, ambaye niliwatoa huko Misri kwa uwezo na nguvu nyingi. Mtanisujudia mimi na kunitolea sadaka. Wakati wote mtatii masharti, maongozi, sheria na amri ambazo niliandika kwa ajili yenu, siku zote mtakuwa waangalifu kuzitenda. Msiiabudu miungu mingine, wala msisahau agano nililofanya nanyi; msiiabudu miungu mingine, bali mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu.” Lakini watu hao hawakusikiliza, bali waliendelea kutenda kama walivyofanya hapo awali. Basi mataifa haya yalimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini pia yalitumikia sanamu zao za kusubu; na mpaka sasa hivi, wazawa wao wanaendelea kutenda hivyo kama walivyotenda babu zao.

2 Wafalme 17:1-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa Ahazi mfalme wa Yuda Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka tisa. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Naye Shalmanesa mfalme wa Ashuru akakwea juu yake, Hoshea akawa mtumishi wake, akampa kodi. Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni. Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao BWANA aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya BWANA, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma. Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao BWANA aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe BWANA; wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili. Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao. Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao. Wakaziacha amri zote za BWANA, Mungu wao, wajitengenezea sanamu za kusubu, yaani, ndama wawili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali. Wakawapitisha watoto wao, wa kiume na wa kike, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza wenyewe wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila la Yuda peke yake. Hata na watu wa Yuda hawakuyashika maagizo ya BWANA, Mungu wao, lakini walikwenda katika amri za Israeli walizokuwa wamezifanya wenyewe. Basi BWANA akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake. Maana aliwatenga mbali Israeli na nyumba ya Daudi; nao wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme; Yeroboamu akawavuta Israeli wasimfuate BWANA, akawakosesha kosa kubwa. Nao wana wa Israeli wakaendelea katika dhambi zote za Yeroboamu alizozifanya; hawakujiepusha nazo; hata BWANA akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo. Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake. Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha BWANA; kwa hiyo BWANA akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi. Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi. Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha BWANA. Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa. Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima, Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Basi hivyo wakamcha BWANA, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu. Wakamcha BWANA, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao. Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi BWANA, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri BWANA aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli; hao ambao BWANA alifanya agano nao, akawaamuru, akasema, Msiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuitumikia, wala kuitolea sadaka; ila yeye BWANA, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri kwa nguvu nyingi, na kwa mkono ulionyoshwa, yeye ndiye mtakayemcha, yeye ndiye mtakayemsujudia, yeye ndiye mtakayemtolea sadaka; na sheria, na hukumu, na torati, na amri, alizowaandikia, hizo ndizo mtakazozishika na kuzifanya hata milele; wala msiche miungu mingine. Na hilo agano nililofanya nanyi, msilisahau; wala msiche miungu mingine; lakini BWANA, Mungu wenu, ndiye mtakayemcha; naye atawaokoa mikononi mwa adui zenu wote. Walakini hawakusikia, bali wakafanya sawasawa na kawaida zao za kwanza. Basi mataifa hawa wakamcha BWANA, tena wakaziabudu sanamu zao za kuchongwa; na wana wao vile vile, na wana wa wana wao; kama walivyofanya baba zao, wao nao hufanya vivyo hivyo hata leo.

2 Wafalme 17:1-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa Ahazi mfalme wa Yuda Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kenda. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Naye Shalmanesa mfalme wa Ashuru akakwea juu yake, Hoshea akawa mtumishi wake, akampa kodi. Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni. Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu. Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao BWANA aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya BWANA, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma. Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao BWANA aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe BWANA; wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili. Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao. Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao. Wakaziacha amri zote za BWANA, Mungu wao, wakajifanyizia sanamu za kusubu, yaani, ndama mbili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali. Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake. Hata na watu wa Yuda hawakuyashika maagizo ya BWANA, Mungu wao, lakini walikwenda katika amri za Israeli walizokuwa wamezifanya wenyewe. Basi BWANA akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake. Maana aliwatenga mbali Israeli na nyumba ya Daudi; nao wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme; Yeroboamu akawavuta Israeli wasimfuate BWANA, akawakosesha kosa kubwa. Nao wana wa Israeli wakaendelea katika dhambi zote za Yeroboamu alizozifanya; hawakujiepusha nazo; hata BWANA akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo. Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake. Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha BWANA; kwa hiyo BWANA akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi. Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi. Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha BWANA. Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa. Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima, Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Basi hivyo wakamcha BWANA, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu. Wakamcha BWANA, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao. Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi BWANA, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri BWANA aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli; hao ambao BWANA alifanya agano nao, akawaamuru, akasema, Msiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuitumikia, wala kuitolea sadaka; ila yeye BWANA, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri kwa nguvu nyingi, na kwa mkono ulionyoshwa, yeye ndiye mtakayemcha, yeye ndiye mtakayemsujudia, yeye ndiye mtakayemtolea sadaka; na sheria, na hukumu, na torati, na amri, alizowaandikia, hizo ndizo mtakazozishika na kuzifanya hata milele; wala msiche miungu mingine. Na hilo agano nililofanya nanyi, msilisahau; wala msiche miungu mingine; lakini BWANA, Mungu wenu, ndiye mtakayemcha; naye atawaokoa mikononi mwa adui zenu wote. Walakini hawakusikia, bali wakafanya sawasawa na kawaida zao za kwanza. Basi mataifa hawa wakamcha BWANA, tena wakaziabudu sanamu zao za kuchongwa; na wana wao vile vile, na wana wa wana wao; kama walivyofanya baba zao, wao nao hufanya vivyo hivyo hata leo.

2 Wafalme 17:1-41 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka tisa. Akafanya maovu machoni pa BWANA, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia. Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akaenda na kumshambulia Mfalme Hoshea, ambaye hapo awali alikuwa akimlipa ushuru kwa sababu alikuwa mtumishi wake. Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri. Wala hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumfunga gerezani. Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuuzingira kwa miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawakalisha huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi. Yote haya yalitukia kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wao, aliyekuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine, na kufuata desturi za mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta. Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya BWANA Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, walijijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote. Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda. Wakafukiza uvumba kila mahali pa juu pa kuabudia, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha BWANA. Wakatumikia sanamu, ingawa BWANA alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.” BWANA akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na Sheria yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii, na ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu, manabii.” Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumwamini BWANA Mungu wao. Walizikataa amri zake, na agano alilolifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa BWANA alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya.” Wakayaacha maagizo yote ya BWANA Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali. Wakawatoa kafara watoto wao wa kiume na wa kike katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa BWANA, wakamghadhibisha. Basi BWANA akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki. Hata hivyo, Yuda nao hawakuzishika amri za BWANA Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli walikuwa wamezianzisha. Kwa hiyo BWANA aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kwenye uwepo wake. Alipokwisha kuwatenga Israeli mbali na nyumba ya Daudi, wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme wao. Yeroboamu akawashawishi Israeli waache kumfuata BWANA na akawasababisha kutenda dhambi kuu. Nao Israeli wakadumu katika dhambi zote za Yeroboamu mwana wa Nebati, nao hawakuziacha hadi BWANA alipowaondoa kwenye uwepo wake, kama vile alivyokuwa ameonya kupitia watumishi wake wote manabii. Hivyo watu wa Israeli wakaondolewa kutoka nchi yao kwenda uhamishoni Ashuru, nao wako huko hata leo. Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake. Wakati walianza kuishi humo, hawakumwabudu BWANA, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu. Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.” Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.” Basi mmoja wa makuhani aliyekuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli, akawafundisha jinsi ya kumwabudu BWANA. Hata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka katika nyumba za ibada za sanamu ambazo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu pa kuabudia. Watu kutoka Babeli wakatengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakatengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakatengeneza Ashima; Waavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Walimwabudu BWANA, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa ibada kwenye mahali pa juu pa kuabudia. Walimwabudu BWANA, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka. Hadi leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu BWANA wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo BWANA aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli. BWANA alipofanya agano na Waisraeli, aliwaamuru: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu. Bali imewapasa kumwabudu BWANA aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu, na kwake yeye mtatoa dhabihu. Imewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine. Msisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine. Bali, mtamwabudu BWANA Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.” Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali. Hata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu BWANA, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Hadi leo watoto wao na wajukuu wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.