2 Wafalme 16:1-20
2 Wafalme 16:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika mwaka wa kumi na saba wa enzi ya Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Hakufanya mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama Daudi babu yake alivyofanya, bali alifuata mienendo ya wafalme wa Israeli. Isitoshe, hata alimpitisha mwanawe motoni kuwa tambiko, akifuata desturi mbaya za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini. Ahazi alitoa sadaka na kufukiza ubani mahali pa juu, vilimani na chini ya kila mti mbichi. Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walitokea ili kupigana vita dhidi ya Yerusalemu, nao walimzingira Ahazi, lakini hawakuweza kumshinda. (Wakati huo, mfalme wa Edomu aliuteka akawarudishia Waedomu mji wa Elathi na kuwafukuza watu wa Yuda waliokaa humo. Nao Waedomu wakaingia Elathi na kufanya makao yao huko mpaka sasa.) Basi Ahazi akatuma watu kwa mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru wakiwa na ujumbe huu: “Mimi ni mtumishi wako mwaminifu. Njoo uniokoe kutoka kwa wafalme wa Aramu na Israeli ambao wananishambulia.” Ahazi akachukua fedha na dhahabu iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na hazina iliyokuwa katika nyumba ya mfalme na kumpelekea kama zawadi mfalme wa Ashuru. Tiglath-pileseri, akiitikia ombi la Ahazi, aliushambulia mji wa Damasko na kuuteka. Akamuua mfalme Resini na kuwapeleka mateka Kiri. Mfalme Ahazi alipokwenda Damasko kukutana na mfalme Tiglath-pileseri, aliona madhabahu huko. Basi, akamtumia kuhani Uria mfano kamili na mchoro wa madhabahu hiyo. Uria akajenga madhabahu hiyo kulingana na mfano huo na kuimaliza kabla ya Ahazi kurejea nyumbani. Ahazi aliporejea kutoka Damasko, aliiona hiyo madhabahu; basi akaikaribia madhabahu na kutoa sadaka juu yake. Alitoa sadaka yake ya kuteketezwa, ya nafaka, na ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka ya amani. Madhabahu ya shaba ambayo iliwekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, aliiondoa mbele ya nyumba kutoka nafasi yake katikati ya madhabahu yake na nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka kwenye nafasi iliyokuwa upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Kisha alimwamuru Uria, “Tumia hii madhabahu yangu kubwa kwa kuteketeza sadaka za asubuhi na sadaka za nafaka za jioni, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka za mfalme na za watu wote na pia sadaka za divai za watu. Irashie damu ya wanyama wote wa kuteketezwa ambao wametolewa sadaka. Lakini ile madhabahu ya shaba nitaitumia mimi kwa kuuliza kauli ya Mungu.” Naye Uria akafuata maagizo ya mfalme. Mfalme Ahazi aliziondoa papi zilizokuwa zimesimamishwa huko, akaondoa birika lililoitwa bahari ambalo lilikuwa juu ya wale fahali kumi na wawili wa shaba na kuliweka juu ya msingi wa mawe. Nalo jukwaa lililotumika siku ya Sabato lililokuwa limejengwa ndani ya nyumba pamoja na kivutio cha nje, mfalme alivihamisha kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya mfalme wa Ashuru. Matendo mengine yote ya mfalme Ahazi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Ahazi akafa na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi, naye Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 16:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa kumi na saba wa Peka mwana wa Remalia Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; wala hakufanya mema machoni pa BWANA Mungu wake, kama Daudi babaye. Lakini aliiendea njia ya wafalme wa Israeli, hata akampitisha mwanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Kisha akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti mbichi. Hapo ndipo akakwea Resini mfalme wa Shamu pamoja na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli juu ya Yerusalemu ili wapigane; wakamhusuru Ahazi, ila hawakuweza kumshinda. Wakati huo Resini mfalme wa Shamu akawarudishia Washami Elathi, akawafukuza Wayahudi kutoka Elathi; nao Washami wakaja Elathi, wakakaa humo hata leo. Basi Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akasema, Mimi ni mtumishi, tena mwana wako; kwea, ukaniokoe mkononi mwa mfalme wa Shamu, na mkononi mwa mfalme wa Israeli, walioniinukia. Ahazi akatwaa fedha na dhahabu iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, akazipeleka kwa mfalme wa Ashuru kuwa zawadi. Na huyo mfalme wa Ashuru akamsikia; mfalme wa Ashuru akapanda juu ya Dameski, akautwaa, akawahamisha watu wake mateka mpaka Kiri, akamwua Resini. Naye mfalme Ahazi akaenda Dameski ili aonane na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akaiona ile madhabahu iliyokuwako Dameski. Mfalme Ahazi akamletea Uria kuhani namna yake ile madhabahu, na cheo chake, kama ilivyokuwa kazi yake yote. Naye Uria kuhani akajenga madhabahu; sawasawa na yote aliyomletea mfalme Ahazi kutoka Dameski; ndivyo alivyoifanya Uria kuhani iwe tayari atakaporudi mfalme Ahazi kutoka Dameski. Na mfalme aliporudi kutoka Dameski, mfalme akaiona ile madhabahu; mfalme akakaribia madhabahuni, na kutoa sadaka juu yake. Akaiteketeza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, akamimina sadaka yake ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka zake za amani, juu ya madhabahu. Na ile madhabahu ya shaba iliyokuwako mbele za BWANA, akaileta kutoka mbele ya nyumba, kutoka kati ya madhabahu yake mwenyewe na nyumba ya BWANA, akaiweka upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Mfalme Ahazi akamwamuru Uria kuhani, akisema, Juu ya madhabahu hiyo kubwa uiteketeze sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, na sadaka ya unga ya jioni, na sadaka ya mfalme ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji; ukanyunyize juu yake damu yote ya sadaka ya kuteketezwa, na damu yote ya dhabihu; bali madhabahu ya shaba itakuwa kwangu mimi ili niiulizie. Akafanya hivyo Uria kuhani, sawasawa na yote aliyoyaamuru mfalme Ahazi. Mfalme Ahazi akakata papi za vitako, akaliondoa lile birika juu yake; akaiteremsha ile bahari itoke juu ya ng'ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya sakafu ya mawe. Na ukumbi wa sabato walioujenga katika hiyo nyumba, na mahali pa kuingia pake mfalme palipokuwapo nje, akavigeuza kuikabili nyumba ya BWANA, kwa sababu ya mfalme wa Ashuru. Basi mambo yote ya Ahazi yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Ahazi akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 16:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa kumi na saba wa Peka mwana wa Remalia Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; wala hakufanya mema machoni pa BWANA Mungu wake, kama Daudi babaye. Lakini aliiendea njia ya wafalme wa Israeli, hata akampitisha mwanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Kisha akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti mbichi. Hapo ndipo akakwea Resini mfalme wa Shamu pamoja na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli juu ya Yerusalemu ili wapigane; wakamhusuru Ahazi, ila hawakuweza kumshinda. Wakati huo Resini mfalme wa Shamu akawarudishia Washami Elathi, akawafukuza Wayahudi kutoka Elathi; nao Washami wakaja Elathi, wakakaa humo hata leo. Basi Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akasema, Mimi ni mtumishi, tena mwana wako; kwea, ukaniokoe mkononi mwa mfalme wa Shamu, na mkononi mwa mfalme wa Israeli, walioniinukia. Ahazi akatwaa fedha na dhahabu iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, akazipeleka kwa mfalme wa Ashuru kuwa zawadi. Na huyo mfalme wa Ashuru akamsikia; mfalme wa Ashuru akapanda juu ya Dameski, akautwaa, akawahamisha watu wake mateka mpaka Kiri, akamwua Resini. Naye mfalme Ahazi akaenda Dameski ili aonane na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akaiona ile madhabahu iliyokuwako Dameski. Mfalme Ahazi akamletea Uria kuhani namna yake ile madhabahu, na cheo chake, kama ilivyokuwa kazi yake yote. Naye Uria kuhani akajenga madhabahu; sawasawa na yote aliyomletea mfalme Ahazi kutoka Dameski; ndivyo alivyoifanya Uria kuhani iwe tayari atakaporudi mfalme Ahazi kutoka Dameski. Na mfalme aliporudi kutoka Dameski, mfalme akaiona ile madhabahu; mfalme akakaribia madhabahuni, na kutoa sadaka juu yake. Akaiteketeza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, akamimina sadaka yake ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka zake za amani, juu ya madhabahu. Na ile madhabahu ya shaba iliyokuwako mbele za BWANA, akaileta kutoka mbele ya nyumba, kutoka kati ya madhabahu yake mwenyewe na nyumba ya BWANA, akaiweka upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Mfalme Ahazi akamwamuru Uria kuhani, akisema, Juu ya madhabahu hiyo kubwa uiteketeze sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, na sadaka ya unga ya jioni, na sadaka ya mfalme ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji; ukanyunyize juu yake damu yote ya sadaka ya kuteketezwa, na damu yote ya dhabihu; bali madhabahu ya shaba itakuwa kwangu mimi ili niiulizie. Akafanya hivyo Uria kuhani, sawasawa na yote aliyoyaamuru mfalme Ahazi. Mfalme Ahazi akakata papi za matako, akaliondoa lile birika juu yake; akaitelemsha ile bahari itoke juu ya ng’ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya sakafu ya mawe. Na ukumbi wa sabato walioujenga katika hiyo nyumba, na mahali pa kuingia pake mfalme palipokuwapo nje, akavigeuza kuikabili nyumba ya BWANA, kwa sababu ya mfalme wa Ashuru. Basi mambo yote ya Ahazi yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Ahazi akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 16:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa kumi na saba wa utawala wa Peka mwana wa Remalia, Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa BWANA Mungu wake. Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, na hata akamtoa kafara mwanawe katika moto, akifuata njia za machukizo za mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele ya Waisraeli. Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda. Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli wakaondoka kwenda kupigana dhidi ya Yerusalemu na kumzingira Ahazi kwa jeshi, lakini hawakuweza kumshinda. Wakati ule, Resini mfalme wa Aramu akaurudisha mji wa Elathi kwa Aramu kwa kuwafukuza watu wa Yuda. Kisha Waedomu wakahamia Elathi, nao wanaishi huko hadi leo. Ahazi akatuma wajumbe kumwambia Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru kwamba, “Mimi ni mtumishi na mtumwa wako. Njoo na uniokoe kutoka mkononi mwa mfalme wa Aramu na wa mfalme wa Israeli, ambao wananishambulia.” Naye Ahazi akachukua fedha na dhahabu zilizopatikana ndani ya Hekalu la BWANA na katika hazina ya jumba la mfalme, na kuzituma kama zawadi kwa mfalme wa Ashuru. Mfalme wa Ashuru akamwitikia kwa kushambulia Dameski na kuiteka. Akawahamishia wenyeji wake huko Kiri, na kumuua Resini. Kisha Mfalme Ahazi akaenda Dameski kukutana na Tiglath-Pileseri wa Ashuru. Akaona madhabahu huko Dameski, naye akamtumia Uria kuhani mchoro wa hayo madhabahu, pamoja na maelezo ya mpango kamili wa ujenzi wake. Kwa hiyo Uria kuhani akajenga madhabahu kulingana na mipango yote ambayo Mfalme Ahazi alikuwa ameituma kutoka Dameski, na akamaliza ujenzi kabla ya Mfalme Ahazi kurudi. Mfalme aliporudi kutoka Dameski na kuona hayo madhabahu, akayasogelea na kutoa sadaka juu yake. Akatoa sadaka yake ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, akamimina sadaka ya kinywaji na kunyunyizia damu ya sadaka zake za amani juu ya hayo madhabahu. Mfalme Ahazi akayaondoa madhabahu ya zamani ya shaba kutoka hapo mbele ya Hekalu la BWANA, yaliyokuwa yamesimama kati ya ingilio la Hekalu na hayo madhabahu mapya, naye akayaweka upande wa kaskazini mwa hayo madhabahu mapya. Ndipo Mfalme Ahazi akatoa amri zifuatazo kwa Uria kuhani: “Juu ya hayo madhabahu kubwa mapya, toa sadaka ya asubuhi ya kuteketezwa na sadaka ya jioni ya nafaka, sadaka ya mfalme ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, pamoja na sadaka yao ya nafaka na sadaka yao ya kinywaji. Unyunyize juu ya hayo madhabahu damu yote ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu. Lakini mimi nitatumia hayo madhabahu ya zamani ya shaba kwa ajili ya kutafuta uongozi.” Naye Uria kuhani akafanya kama Mfalme Ahazi alivyoagiza. Mfalme Ahazi akaondoa mbao za pembeni na kuondoa masinia kwenye vile vishikilio vilivyohamishika. Akaondoa ile Bahari kutoka mafahali wa shaba walioishikilia, na kuiweka kwenye kitako cha jiwe. Kwa heshima ya mfalme wa Ashuru, akaliondoa pia pazia la Sabato lililokuwa limewekwa ndani ya Hekalu, na akaondoa ile njia ya kifalme ya kuingia kwenye Hekalu la BWANA. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ahazi na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Ahazi akalala na baba zake, naye akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Hezekia mwanawe akawa mfalme baada yake.