Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 14:1-14

2 Wafalme 14:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mwaka wa pili wa enzi ya Yehoashi mwana wa Yehoahazi huko Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alipoanza kutawala alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, naye alitawala katika Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwa kama babu yake Daudi. Bali alifanya mambo yote kama Yoashi baba yake; isipokuwa mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani mahali hapo. Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani, aliwaua watumishi waliomuua mfalme, baba yake. Lakini hakuwaua watoto wa wauaji; kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria za Mose, Mwenyezi-Mungu anapotoa amri akisema, “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.” Amazia aliwaua Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi; aliutwaa kwa nguvu mji wa Sela na kuuita Yoktheeli, na hivi ndivyo unavyoitwa mpaka sasa. Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli akisema, “Njoo tupambane.” Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia mfalme wa Israeli, akisema, “Siku moja mbaruti wa Lebanoni uliuambia mwerezi, wa huko Lebanoni pia, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu.’ Lakini mnyama wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mbaruti huo. Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?” Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda. Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yehoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi; halafu akauendea Yerusalemu na kuubomoa ukuta wake kutoka Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200. Alichukua dhahabu yote na fedha, hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu; pia alichukua mateka, kisha akarudi Samaria.

2 Wafalme 14:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na tisa katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi. Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ikawa, mara ufalme ulipokuwa imara mkononi mwake, aliwaua watumishi wale waliomwua mfalme baba yake; ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Torati ya Musa, kama alivyoamuru BWANA, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe. Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo. Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso. Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti. Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe? Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda. Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, dhiraa mia nne. Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria.

2 Wafalme 14:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi. Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ikawa, mara ufalme ulipokuwa imara mkononi mwake, aliwaua watumishi wale waliomwua mfalme baba yake; ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, kama alivyoamuru BWANA, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe. Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo. Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso. Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti. Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe? Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda. Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, mikono mia nne. Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria.

2 Wafalme 14:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu. Akatenda yaliyo mema machoni pa BWANA, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Baada ya ufalme kuimarika mkononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake. Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Musa ambako BWANA aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.” Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo. Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tukabiliane uso kwa uso.” Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani mwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?” Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani mwake. Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa mia nne. Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la BWANA na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria.