Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 13:1-24

2 Wafalme 13:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mwaka wa ishirini na tatu wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli, akaendelea kutawala huko Samaria muda wa miaka kumi na saba. Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyewakosesha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Yehoahazi hakuacha matendo hayo mabaya. Mwenyezi-Mungu alikasirika, akawafanya watu wa Israeli washindwe vitani mara kwa mara na mfalme Hazaeli wa Aramu na mwanawe Ben-hadadi. Yehoahazi akamsihi Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu alipoona jinsi mfalme wa Aramu alivyowadhulumu watu wa Israeli alisikia maombi yake. (Mwenyezi-Mungu akawapa watu wa Israeli kiongozi ambaye aliwakomboa kutoka kwa Washamu, ndipo wakakaa kwa amani kama vile walivyokuwa hapo awali. Hata hivyo hawakuacha kutenda dhambi ambazo mfalme Yeroboamu aliwakosesha watu wa Israeli; lakini waliendelea na dhambi zao na sanamu ya mungu wa kike Ashera ilihifadhiwa huko Samaria.) Yehoahazi hakuwa na majeshi, ila tu wapandafarasi hamsini, magari kumi na askari wa miguu 10,000. Hii ilikuwa ni kwa sababu mfalme wa Aramu alikuwa ameyaangamiza majeshi ya Israeli na kuyakanyaga chini kama mavumbi. Matendo mengine yote ya Yehoahazi na ushujaa wake yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Yehoahazi alifariki na kuzikwa huko Samaria, naye mwanawe Yehoashi akawa mfalme mahali pake. Katika mwaka wa thelathini na saba wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoashi mwanawe Yehoahazi, alianza kutawala Israeli huko Samaria, na enzi yake ikaendelea kwa miaka kumi na sita. Yehoashi pia alitenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati ambaye aliwapotosha watu wa Israeli. Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Yehoashi alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria, naye mwanawe Yeroboamu wa pili akatawala mahali pake. Nabii Elisha aliugua ugonjwa mbaya sana. Alipokuwa karibu kufa, mfalme Yehoashi wa Israeli alimtembelea. Alipomfikia Elisha, alilia, akisema, “Baba yangu, baba yangu! Magari ya Israeli na wapandafarasi wake!” Elisha akamwamuru, “Hebu lete upinde na mishale!” Yehoashi akavileta. Elisha akamwambia ajitayarishe kupiga mishale. Mfalme akajitayarisha na Elisha akaiweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Mfalme alifuata maagizo ya nabii na kufungua dirisha ambalo lilielekea Aramu. Elisha akatoa amri “Tupa mshale!” Mara tu mfalme alipotupa mshale, nabii akasema, “Wewe ndio mshale wa Mwenyezi-Mungu, ambao kwao atapata ushindi juu ya Waaramu. Utapigana na Waaramu huko Afeka mpaka uwashinde.” Ndipo Elisha akamwambia mfalme achukue mishale mingine na kuipiga chini. Mfalme akapiga mishale chini mara tatu, kisha akaacha. Elisha alikasirika sana, akamwambia mfalme, “Mbona hukupiga mara tano au sita? Hivyo ungewaangamiza Waaramu kabisa. Lakini sasa utawashinda mara tatu tu.” Elisha alifariki, akazikwa. Kila mwaka, makundi ya Wamoabu yalikuja kuishambulia nchi ya watu wa Israeli. Wakati mmoja, wakati wa mazishi, watu waliona kundi mojawapo la watu waliobeba maiti wakamtupa yule maiti kaburini mwa Elisha na kukimbia. Mara maiti huyo alipogusa mifupa ya Elisha, alifufuka na kusimama wima. Mfalme Hazaeli wa Aramu aliwanyanyasa sana watu wa Israeli wakati wote wa enzi ya Yehoahazi. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwarehemu na kuwaonea huruma. Aliwaangalia kwa wema kwa sababu ya agano lake na Abrahamu, Isaka na Yakobo. Hakuwaangamiza wala hajawaacha kamwe mpaka leo. Hazaeli mfalme wa Aramu alipofariki, Ben-hadadi mwanawe alitawala mahali pake.

2 Wafalme 13:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia, mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kumi na saba. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, akayafuata makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; wala hakuyaacha. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli mfalme wa Shamu, na mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli, siku zote. Naye Yehoahazi akamsihi BWANA, BWANA akamsikiliza; kwa kuwa aliyaona mateso ya Israeli, jinsi mfalme wa Shamu alivyowatesa. (BWANA akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza. Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa katika Samaria). Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa. Basi mambo yote ya Yehoahazi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Yehoahazi akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoashi mwanawe akatawala mahali pake. Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria, akatawala miaka kumi na sita. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo. Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake aliopigania na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli. Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akateremka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza. Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha. Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu. Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka. Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu. Na Hazaeli mfalme wa Shamu akawaonea Israeli siku zote za Yehoahazi. Lakini BWANA akawahurumia, akawasikitikia, na kuwaangalia, kwa ajili ya agano lake na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, wala hakutaka kuwaangamiza, wala hakuwatupa usoni pake bado. Akafa Hazaeli mfalme wa Shamu, na Ben-hadadi mwanawe akatawala mahali pake.

2 Wafalme 13:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia, mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kumi na saba. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, akayafuata makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; wala hakuyaacha. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli mfalme wa Shamu, na mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli, siku zote. Naye Yehoahazi akamsihi BWANA, BWANA akamsikiliza; kwa kuwa aliyaona mateso ya Israeli, jinsi mfalme wa Shamu alivyowatesa. (BWANA akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza. Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa vivyo katika Samaria). Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa. Basi mambo yote ya Yehoahazi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Yehoahazi akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoashi mwanawe akatawala mahali pake. Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria, akatawala miaka kumi na sita. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo. Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake aliopigania na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli. Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza. Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha. Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu. Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka. Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu. Na Hazaeli mfalme wa Shamu akawaonea Israeli siku zote za Yehoahazi. Lakini BWANA akawahurumia, akawasikitikia, na kuwaangalia, kwa ajili ya agano lake na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, wala hakutaka kuwaangamiza, wala hakuwatupa usoni pake bado. Akafa Hazaeli mfalme wa Shamu, na Ben-hadadi mwanawe akatawala mahali pake.

2 Wafalme 13:1-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wa Yoashi mwana wa Ahazia mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka kumi na saba. Akafanya maovu machoni pa BWANA kwa kufuata dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, na wala hakuziacha. Kwa hiyo hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Israeli na kwa muda mrefu akawaweka chini ya utawala wa Hazaeli mfalme wa Aramu, na Ben-Hadadi mwanawe. Ndipo Yehoahazi akamsihi BWANA ampe rehema, naye BWANA akamsikiliza, kwa maana aliona jinsi mfalme wa Aramu alivyokuwa akiwatesa Israeli vikali. BWANA akamtoa mwokozi kwa ajili ya Israeli, nao wakaokoka kutoka mamlaka ya Aramu. Hivyo Waisraeli wakaishi katika nyumba zao wenyewe kama ilivyokuwa hapo awali. Lakini hawakuziacha dhambi za nyumba ya Yeroboamu, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, bali wakaendelea kuzitenda. Nguzo ya Ashera pia iliendelea kusimama katika Samaria. Hapakubaki kitu chochote katika jeshi la Yehoahazi isipokuwa wapanda farasi hamsini, magari kumi ya vita na askari wa miguu elfu kumi, kwa kuwa mfalme wa Aramu alikuwa amewaangamiza hao wengine na kuwafanya kama mavumbi wakati wa kupura nafaka. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoahazi, yote aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Yehoahazi akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Yehoashi mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika mwaka wa thelathini na saba wa utawala wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala Israeli huko Samaria, naye akatawala miaka kumi na sita. Alifanya maovu machoni pa BWANA, na hakuacha dhambi yoyote kati ya zile za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, bali aliendelea kuzitenda. Na kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, yote aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Yehoashi akalala na baba zake, naye Yeroboamu akawa mfalme baada yake. Yehoashi akazikwa Samaria na wafalme wa Israeli. Wakati huu, Elisha alikuwa anaugua ugonjwa ambao baadaye ulimuua. Yehoashi mfalme wa Israeli akashuka kwenda kumwona na kumlilia. Akalia, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Elisha akasema, “Leta upinde na baadhi ya mishale,” naye mfalme akafanya hivyo. Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Shika upinde mikononi mwako.” Alipokwisha kuuchukua, Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. Elisha akasema, “Fungua dirisha la mashariki,” naye akalifungua. Elisha akasema, “Piga mshale!” Naye akapiga mshale. Elisha akasema, “Mshale wa ushindi wa BWANA, mshale wa ushindi juu ya Aramu! Utawaangamiza Waaramu kabisa huko Afeki.” Kisha akasema, “Chukua mishale,” naye mfalme akaichukua. Elisha akamwambia, “Piga ardhi kwa hiyo mishale.” Akaipiga mara tatu, halafu akaacha. Mtu wa Mungu akamkasirikia na akasema, “Ungepiga chini mara tano au sita, ndipo ungeishinda Aramu na kuiangamiza kabisa. Lakini sasa utaishinda mara tatu tu.” Elisha akafa, nao wakamzika. Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli. Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Elisha. Ile maiti ilipogusa mifupa ya Elisha, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake. Hazaeli mfalme wa Aramu aliwatesa Israeli wakati wote wa utawala wa Yehoahazi. Lakini BWANA akawarehemu na akawahurumia, akaonesha kujishughulisha nao kwa sababu ya agano lake na Abrahamu, Isaka na Yakobo. Hadi leo, hajawaangamiza wala kuwafukuza mbele zake. Hazaeli mfalme wa Shamu akafa, naye Ben-Hadadi mwanawe akawa mfalme baada yake.