Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 11:1-21

2 Wafalme 11:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Mara Athalia, mamake mfalme Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka, akaangamiza jamii yote ya kifalme. Lakini Yehosheba binti ya mfalme Yoramu, dada yake Ahazia, alimchukua kwa siri Yoashi mwana wa Ahazia, kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha yeye pamoja na yaya wake katika chumba cha kulala. Hivyo walimficha ili Athalia asimwone na kumwua. Yoashi alikaa naye kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi. Lakini katika mwaka wa saba Yehoyada alituma ujumbe na kuwakusanya makapteni wa Wakari na walinzi; akaamuru wamjie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akafanya nao mapatano na kuwaapisha humo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaonesha Yoashi mwana wa mfalme Ahazia. Kisha akatoa amri: “Mtafanya hivi: Mtakapokuja kushika zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda ikulu; theluthi nyingine ikiwa kwenye lango la Suri na theluthi nyingine ikiwa kwenye lango nyuma ya walinzi. Hivyo ndivyo mtakavyolinda ikulu ili isivunjwe. Yale makundi mawili ambayo humaliza zamu yao siku ya Sabato yatashika zamu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kumlinda mfalme. Mtamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi na mtu yeyote atakayethubutu kuwakaribia lazima auawe. Lazima mkae na mfalme, awe anatoka au anakaa.” Makapteni walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato, basi wakamwendea kuhani Yehoyada. Kisha kuhani akawapa makapteni mikuki na ngao zilizokuwa mali ya mfalme Daudi, na ambazo zilikuwa zimewekwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao walinzi walisimama kuanzia upande wa kusini wa nyumba mpaka upande wa kaskazini wa nyumba na kuzunguka madhabahu na nyumba ili kumzunguka mfalme; kila mtu akiwa ameshika mkuki wake mkononi. Halafu akamtoa nje mwana wa mfalme, akamvika taji kichwani, na kumpa ule ushuhuda; wakamtawaza na kumpaka mafuta; wakapiga makofi na kusema, “Aishi mfalme!” Naye Athalia aliposikia sauti za walinzi pamoja na za watu wengine, aliwaendea hao watu waliokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Alipochungulia akamwona mfalme mpya amesimama karibu na nguzo kwenye lango la hekalu, kama ilivyokuwa desturi, huku makapteni na wapiga tarumbeta wakiwa kando ya mfalme; na wakazi wote wakishangilia na kupiga tarumbeta; ndipo aliporarua nguo zake na kusema kwa sauti kubwa, “Uhaini! Uhaini!” Kisha kuhani Yehoyada akaamuru makapteni wa jeshi akisema; “Mtoeni nje katikati ya askari, na ueni mtu yeyote atakayemfuata.” Kwa sababu kuhani alisema, “Asiuawe katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, wakamkamata, wakampeleka na kumpitisha kwenye Lango la Farasi kuelekea ikulu, naye akauawa huko. Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Mwenyezi-Mungu na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi-Mungu; kadhalika alifanya agano kati ya mfalme na watu. Halafu wakazi wote wakaenda kwenye nyumba ya Baali na kuibomoa, wakavunja madhabahu pamoja na sanamu zake, hata wakamuua Matani, kuhani wa Baali mbele ya madhabahu. Kuhani Yehoyada akaweka walinzi kulinda nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliwachukua makapteni, Wakari na wakazi wote; nao wakamsindikiza mfalme kutoka nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakapitia katika lango la walinzi mpaka ikulu. Naye akakikalia kiti cha enzi. Kwa hiyo, wakazi wote walijawa furaha; na mji wote ulikuwa mtulivu, baada ya Athalia kuuawa kwa upanga katika ikulu. Yoashi alianza kutawala Yuda akiwa na umri wa miaka saba.

2 Wafalme 11:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme. Ila Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa. Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa BWANA, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi. Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya BWANA; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa BWANA, akawaonesha huyo mwana wa mfalme. Akawaamuru, akasema, Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, mtakaoshika zamu siku ya sabato, mtalinda kasri ya mfalme; na theluthi mtakuwapo mlangoni pa Suri; na theluthi langoni nyuma ya walinzi; hivyo ndivyo mtalinda kasri, kuzuia watu wasiingie. Na sehemu mbili zenu, yaani, wote watokao siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya BWANA kumzunguka mfalme. Mtamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye ndani ya safu auawe; mkafuatane na mfalme, akitoka na akiingia. Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani. Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa BWANA. Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kulia ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote. Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, Mfalme na aishi. Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa BWANA; akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Uhaini! Uhaini! Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; naye yeyote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa BWANA. Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko. Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya BWANA na mfalme na watu, ili wawe watu wa BWANA; tena kati ya mfalme na watu. Watu wote wa nchi wakaiendea nyumba ya Baali, wakaiangusha; madhabahu zake na sanamu zake wakazivunjavunja kabisa, na Matani kuhani wa Baali wakamwua mbele ya madhabahu. Na Yehoyada kuhani akaweka walinzi wa nyumba ya BWANA. Akawatwaa wakuu wa mamia, na Wakari, na walinzi, na watu wote wa nchi; wakamleta mfalme kushuka nyumbani mwa BWANA, wakaja kwa njia ya mlango wa walinzi mpaka nyumba ya mfalme. Naye akakaa katika kiti cha enzi cha wafalme. Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia. Naye Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme. Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.

2 Wafalme 11:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme. Ila Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, umbu lake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa. Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa BWANA, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi. Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya BWANA; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa BWANA, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme. Akawaamuru, akasema, Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, mtakaoingia siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya mfalme; na theluthi mtakuwapo mlangoni pa Suri; na theluthi langoni nyuma ya walinzi; hivyo mtayalinda malinzi ya nyumba, kuzuia watu wasiingie. Na sehemu mbili zenu, yaani, wote watokao siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya BWANA kumzunguka mfalme. Mtamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye ndani ya safu auawe; mkafuatane na mfalme, akitoka na akiingia. Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani. Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa BWANA. Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote. Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, mfalme na aishi. Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa BWANA; akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Fitina! Fitina! Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; naye ye yote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa BWANA. Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko. Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya BWANA na mfalme na watu, ili wawe watu wa BWANA; tena kati ya mfalme na watu. Watu wote wa nchi wakaiendea nyumba ya Baali, wakaiangusha; madhabahu zake na sanamu zake wakazivunja-vunja kabisa, na Matani kuhani wa Baali wakamwua mbele ya madhabahu. Na Yehoyada kuhani akaweka maakida juu ya nyumba ya BWANA. Akawatwaa wakuu wa mamia, na Wakari, na walinzi, na watu wote wa nchi; wakamleta mfalme kushuka nyumbani mwa BWANA, wakaja kwa njia ya mlango wa walinzi mpaka nyumba ya mfalme. Naye akakaa katika kiti cha enzi cha wafalme. Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia. Naye Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme. Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.

2 Wafalme 11:1-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuangamiza jamaa yote ya mfalme. Lakini Yehosheba, binti ya Mfalme Yehoramu, aliyekuwa pia dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa. Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake katika Hekalu la BWANA kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi. Katika mwaka wa saba, Yehoyada akatumania wakuu wa vikundi vya mamia, na Wakari na walinzi, nao wakaletwa kwake katika Hekalu la BWANA. Alifanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la BWANA. Ndipo akawaonesha mwana wa mfalme. Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda jumba la kifalme, theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu. Nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika siku ya Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme. Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.” Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada. Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA. Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu. Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakampaka mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!” Athalia aliposikia kelele za walinzi pamoja na watu, akawaendea watu katika Hekalu la BWANA. Akaangalia, na tazama, mfalme alikuwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!” Kuhani Yehoyada akawaamuru majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, “Mtoeni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la BWANA.” Basi wakamkamata Athalia alipofika mahali farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuua hapo. Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya BWANA na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa BWANA. Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu. Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu. Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la BWANA. Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamteremsha mfalme kutoka Hekalu la BWANA na kwenda kwenye jumba la mfalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha ufalme; nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga nyumbani mwa mfalme. Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.