2 Wakorintho 5:1-5
2 Wakorintho 5:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana tunajua kwamba hema hii ambamo tunaishi sasa hapa duniani yaani mwili wetu, itakapongolewa, Mungu atatupa makao mengine mbinguni, nyumba ya milele isiyotengenezwa kwa mikono. Na sasa, katika hali hii, tunaugua tukitazamia kwa hamu kubwa kuvikwa makao yetu yaliyo mbinguni. Naam, tunapaswa kuvikwa namna hiyo ili tusije tukasimama mbele ya Mungu bila vazi. Tukiwa bado katika hema hii ya duniani, tunalia kwa kukandamizwa; si kwamba tunataka kuuvua mwili huu wa kufa, ila tuna hamu ya kuvalishwa ule usiokufa, ili kile chenye kufa kimezwe kabisa na uhai. Mungu mwenyewe alitutayarishia mabadiliko hayo, naye ametupa Roho wake awe dhamana ya yote aliyotuwekea.
2 Wakorintho 5:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni. Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni; ikiwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tuko uchi. Kwa sababu sisi tulio katika maskani hii twapumua kwa shida, tukilemewa; si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa, ili kitu kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima. Basi yeye aliyetufanya kwa ajili ya neno lilo hilo ni Mungu, aliyetupa arabuni ya Roho.
2 Wakorintho 5:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni. Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni; ikiwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tu uchi. Kwa sababu sisi tulio katika maskani hii twaugua, tukilemewa; si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa, ili kitu kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima. Basi yeye aliyetufanya kwa ajili ya neno lilo hilo ni Mungu, aliyetupa arabuni ya Roho.
2 Wakorintho 5:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa maana twajua kama hema letu la dunia tunayoishi likiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. Katika hema hili twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, kwa kuwa tukishavikwa hatutaonekana tena kuwa uchi. Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hili twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima. Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo, naye ametupatia Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.