2 Wakorintho 12:11-21
2 Wakorintho 12:11-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Nimekuwa kama mpumbavu, lakini nyinyi mmenilazimisha kuwa hivyo. Nyinyi ndio mngalipaswa kunisifu. Maana, ingawa mimi si kitu, kwa vyovyote, mimi si mdogo kuliko hao “mitume wakuu.” Miujiza na maajabu yaoneshayo wazi kwamba mimi ni mtume yalifanyika miongoni mwenu kwa uvumilivu wote. Je, mlipungukiwa nini zaidi kuliko makanisa mengine, isipokuwa tu kwamba mimi kwa upande wangu sikuwasumbueni kupata msaada wenu? Samahani kwa kuwakoseeni haki hiyo! Sasa niko tayari kabisa kuja kwenu mara ya tatu, na sitawasumbua. Maana ninachotafuta si mali zenu, bali ni nyinyi wenyewe. Ni kawaida ya wazazi kuwawekea watoto wao akiba, na si watoto kuwawekea wazazi wao. Mimi ni radhi kabisa kutumia nilicho nacho, na hata kujitolea mimi mwenyewe kabisa, kwa faida ya roho zenu. Je, mtanipenda kidogo ati kwa kuwa mimi nawapenda nyinyi mno? Basi, mtakubali kwamba sikuwa mzigo kwenu. Lakini labda mtu mwingine atasema: “Kwa vile Paulo ni mwerevu, amewafanyieni ulaghai.” Je, mimi niliwanyonyeni kwa njia ya mjumbe yeyote niliyemtuma kwenu? Mimi nilimwita Tito, nikamtuma kwenu na ndugu yetu mwingine. Je, Tito aliwanyonyeni? Je, hamjui kwamba sisi tumekuwa tukiongozwa na roho yuleyule, na mwenendo wetu ni mmoja? Labda mnafikiri kwamba mpaka sasa tumekuwa tukijitetea wenyewe mbele yenu! Lakini, tunasema mambo haya mbele ya Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. Mambo hayo yote, wapenzi wangu, ni kwa ajili ya kuwajenga nyinyi. Naogopa, huenda nitakapokuja kwenu nitawakuta katika hali nisiyopenda, nami itanilazimu kuwa katika hali msiyoipenda. Naogopa huenda kukawa na ugomvi, wivu, uhasama, ubishi, masengenyo, kunongona, majivuno na fujo kati yenu. Naogopa huenda hapo nitakapokuja safari ijayo Mungu wangu atanifanya niaibike mbele yenu, nami nitaomboleza kwa ajili ya wengi wa wale waliotenda dhambi lakini hawakujuta huo uchafu, tamaa zao mbaya na uzinzi waliokuwa wamefanya.
2 Wakorintho 12:11-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lolote, nijapokuwa si kitu. Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika subira yote, kwa ishara na maajabu na miujiza. Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe kosa hili. Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto. Nami nitakuwa radhi kutumia na kutumiwa kwa ajili yenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa? Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu niliwapata kwa hila. Je! Mtu yeyote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo niliwatoza kitu? Nilimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile? Mnadhani hata sasa ya kuwa najitetea kwenu! Mbele za Mungu twanena katika Kristo. Na hayo yote, wapenzi, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi. Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia; nami nitakapokuja tena, Mungu wangu asije akanidhili kwenu, nami nikawasikitikia wengi waliokosa tangu hapo, wasiutubie uchafu, na uasherati, na uovu walioufanya.
2 Wakorintho 12:11-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lo lote, nijapokuwa si kitu. Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika saburi yote, kwa ishara na maajabu na miujiza. Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe udhalimu huu. Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto. Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa? Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu naliwapata kwa hila. Je! Mtu ye yote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo naliwatoza kitu? Nalimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile? Mwadhani hata sasa ya kuwa najidhuru kwenu! Mbele za Mungu twanena katika Kristo. Na hayo yote, wapenzi, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi. Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong’onezo, na majivuno, na ghasia; nami nitakapokuja tena, Mungu wangu asije akanidhili kwenu, nami nikawasikitikia wengi waliokosa tangu hapo, wasiutubie uchafu, na uasherati, na ufisadi walioufany
2 Wakorintho 12:11-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nimejifanya mjinga, lakini mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ilinipasa kusifiwa na ninyi, kwa sababu mimi si dhalili kuliko wale “mitume walio bora”, ingawa mimi si kitu. Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi. Je, ninyi ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila tu kwamba mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili! Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara ya tatu. Nami sitawalemea, kwa sababu sihitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi. Kwa kuwa watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao. Hivyo nitafurahi kutumia kila kitu nilicho nacho kwa ajili yenu, hata mwili wangu pia. Je, ninavyozidi kuwapenda, ndivyo upendo wenu kwangu unavyopungua? Iwe iwavyo, kwa vyovyote vile, mimi sikuwalemea. Lakini wengine wanadhani mimi ni mjanja, nami niliwapata kwa hila! Je, nilijipatia faida kwa kumtumia mtu yeyote niliyemtuma kwenu? Nilimshawishi Tito aje kwenu, nami nilimtuma pamoja na ndugu yetu. Je, Tito aliwatumia ninyi ili kujipatia faida? Je, hatukuenenda kwa roho moja, na kwa hatua zile zile? Je, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Kristo. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu. Kwa kuwa nina hofu kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko. Nina hofu kwamba nitakapokuja tena kwenu, Mungu wangu atanidhili mbele yenu, nami nitasikitishwa na wengi waliotenda dhambi mbeleni, na wala hawajatubu kwa uchafu wao, uasherati, na ufisadi walioushiriki.