2 Wakorintho 1:12-24
2 Wakorintho 1:12-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Sisi tunajivunia kitu kimoja: Dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali na neema ya Mungu. Tunawaandikia nyinyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa, maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea nyinyi fahari. Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu. Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea. Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema “Ndiyo” na “Siyo” papo hapo? Mungu ni ukweli tupu; basi, kile tulichowaambia nyinyi si jambo la “Ndiyo” na “Siyo”. Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa “Ndiyo” na “Siyo;” bali yeye daima ni “Ndiyo” ya Mungu. Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa “Ndiyo”. Kwa sababu hiyo, “Amina” yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu. Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na nyinyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu; ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea. Mungu ndiye shahidi wangu; yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho kwa sababu tu ya kuwahurumieni. Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; nyinyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.
2 Wakorintho 1:12-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi. Maana hatuwaandikii ninyi neno, ila yale msomayo, au kuyakiri; nami natarajia ya kuwa mtayakiri hayo hata mwisho; vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kuwa sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana wetu Yesu. Nami nikiwa na tumaini hilo nilitaka kufika kwenu hapo kwanza, ili mpate karama ya pili; na kupita kwenu na kuendelea mpaka Makedonia; na tena toka Makedonia kurudi kwenu na kusafirishwa nanyi kwenda Yudea. Basi, nilipokusudia hayo, je! Nilitumia kigeugeu? Au hayo niyakusudiayo, nayakusudia kwa jinsi ya mwili kwamba iwe hivi kwangu, kusema Ndiyo, ndiyo, na Siyo, siyo? Lakini kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Ndiyo na Siyo. Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, yaani, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na Siyo; bali katika yeye ni Ndiyo. Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia mhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu. Lakini mimi namwita Mungu awe shahidi juu ya roho yangu, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijafika Korintho. Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama.
2 Wakorintho 1:12-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi. Maana hatuwaandikii ninyi neno, ila yale msomayo, au kuyakiri; nami nataraji ya kuwa mtayakiri hayo hata mwisho; vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kwamba sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana wetu Yesu. Nami nikiwa na tumaini hilo nalitaka kufika kwenu hapo kwanza, ili mpate karama ya pili; na kupita kwenu na kuendelea mpaka Makedonia; na tena toka Makedonia kurudi kwenu na kusafirishwa nanyi kwenda Uyahudi. Basi, nilipokusudia hayo, je! Nalitumia kigeugeu? Au hayo niyakusudiayo, nayakusudia kwa jinsi ya mwili kwamba iwe hivi kwangu, kusema Ndiyo, ndiyo, na Siyo, siyo? Lakini kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Ndiyo na siyo. Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, yaani, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo. Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu. Lakini mimi namwita Mungu awe shahidi juu ya roho yangu, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijafika Korintho. Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama.
2 Wakorintho 1:12-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi haya ndio majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeishi katika ulimwengu kwa utakatifu na uaminifu unaotoka kwa Mungu, na hasa katika uhusiano wetu na ninyi. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu. Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba, kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Yesu. Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili. Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia, na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Yudea. Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo? Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajakuwa “Ndiyo” na “Siyo”. Kwa kuwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silvano, na Timotheo tulimhubiri kwenu, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo”, bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo”. Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Kristo ni “Ndiyo”. Kwa sababu hii, ni kwake yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu. Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Kristo. Alitupaka mafuta kwa kututia muhuri wake na kutupatia Roho wake mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia yote aliyotuahidi. Namwita Mungu awe shahidi wangu kwamba sikurudi Korintho kwa sababu niliwahurumia ninyi. Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi ili mfurahi, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.