2 Mambo ya Nyakati 6:1-21
2 Mambo ya Nyakati 6:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo Solomoni akasema, “Mwenyezi-Mungu alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba tukufu, mahali pa makao yako ya milele.” Kisha Solomoni akaigeukia jumuiya yote ya watu wa Israeli wakiwa wamesimama, akawabariki. Akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ameitimiza ahadi yake aliyoitoa kwa baba yangu Daudi akisema, ‘Tangu niwaondoe watu wangu kutoka nchi ya Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; na sikumchagua mtu yeyote awe mkuu wa watu wangu Israeli. Nimeuchagua mji wa Yerusalemu uwe mji ambamo nitaabudiwa, na nimemchagua Daudi awatawale watu wangu Israeli.’ “Kwa hiyo, baba yangu Daudi alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba. Hata hivyo, si wewe utakayejenga hiyo nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’” “Na sasa Mwenyezi-Mungu ametimiza ahadi yake, kwani nimekuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, na kukikalia kiti cha enzi cha Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyoahidi; pia nimejenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Katika nyumba hiyo nimeliweka sanduku la agano, ambalo ndani yake mna agano la Mwenyezi-Mungu alilofanya na watu wa Israeli.” Kisha, Solomoni alisimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu halafu mbele ya jumuiya yote ya watu wa Israeli, aliinua mikono yake juu. Solomoni alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba ambalo aliliweka katikati ya ua. Urefu na upana wake ulikuwa mita mbili na robo, na kimo chake mita moja na robo. Alipanda jukwaani na kupiga magoti mbele ya jumuiya yote ya Israeli, akainua mikono yake kuelekea mbinguni. Aliomba akisema, “Ee, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu mwingine kama wewe, mbinguni ama duniani. Wewe ni mwaminifu, kwani umetimiza agano lako na kuwaonesha fadhili zako watumishi wako wanaoishi wakikutii kwa moyo wao wote. Umetimiza ahadi uliyotoa kwa mtumishi wako baba yangu Daudi; naam, yale uliyonena umeyatimiza leo kwa uwezo wako mwenyewe. “Kwa hiyo sasa, Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninakuomba pia utimize ile ahadi uliyomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu, ukisema, ‘Siku zote utakuwa na mzawa wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, iwapo wazawa wako watafuata kwa uangalifu sheria yangu kama wewe ulivyofanya mbele yangu.’ Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakusihi utimize yote uliyomwahidi mtumishi wako Daudi. “Lakini, ee Mungu kweli utakaa humu duniani na binadamu? Hata mbingu zenyewe, wala mbingu za mbingu za juu sana hazikutoshi, itakutoshaje nyumba hii ambayo nimeijenga? Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mimi mtumishi wako, nakuomba unisikilize na kunitimizia ombi langu ninalokuomba leo. Ichunge nyumba hii mchana na usiku, mahali ambapo umechagua watu wako waliabudu jina lako. Unisikie mimi mtumishi wako ninapokuja mahali hapa kuomba. Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni na ukisha sikia, utusamehe.
2 Mambo ya Nyakati 6:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Sulemani akanena, BWANA alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Lakini nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele. Mfalme akageukia mkutano wote wa Israeli akawabariki, mkutano wote wa Israeli ukiwa umesimama. Akasema, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena kwa kinywa chake na baba yangu Daudi, akalitimiza kwa mikono yake, akasema, Tangu siku ile nilipowatoa watu wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji wowote wa kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe humo; wala sikumchagua mtu yeyote awe mkuu juu ya watu wangu Israeli; lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli. Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako; lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika uzao wako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu. Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Ndimo nilimoliweka hilo sanduku, ambalo ndani yake mna agano la BWANA, alilolifanya na wana wa Israeli. Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akainyosha mikono; (maana Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano, na kwenda juu kwake dhiraa tatu, na kuisimamisha katikati ya ua; akasimama juu yake, akapiga magoti mbele ya mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake kuelekea mbinguni); akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote; uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umtimizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi. Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; seuze nyumba hii niliyoijenga! Walakini umwangalie mtumishi wako anayoyaomba, na kusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumishi wako mbele zako; ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumishi wako, akikabili mahali hapa. Uyasikie atakayosihi mtumishi wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.
2 Mambo ya Nyakati 6:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Sulemani akanena, BWANA alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Lakini nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele. Mfalme akageuza uso wake, akawabarikia mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama. Akasema, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena kwa kinywa chake na baba yangu Daudi, akalitimiza kwa mikono yake, akasema, Tangu siku ile nilipowatoa watu wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji wo wote wa kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe humo; wala sikumchagua mtu ye yote awe mkuu juu ya watu wangu Israeli; lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli. Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako; lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu. Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Ndimo nilimoliweka hilo sanduku, ambalo ndani yake mna agano la BWANA, alilolifanya na wana wa Israeli. Akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akainyosha mikono; (maana Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake mikono mitano, na upana wake mikono mitano, na kwenda juu kwake mikono mitatu, na kuisimamisha katikati ya ua; akasimama juu yake, akapiga magoti mbele ya mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake kuelekea mbinguni); akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote; uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi. Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyoijenga! Walakini umwangalie mtumwa wako anayoyaomba, na kusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumwa wako mbele zako; ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumwa wako, akikabili mahali hapa. Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.
2 Mambo ya Nyakati 6:1-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Sulemani akasema, “BWANA alisema kwamba ataishi katika giza nene. Nimejenga Hekalu zuri kwa ajili yako, mahali pako pa kukaa milele.” Kusanyiko lote la Israeli walipokuwa wamesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. Kisha akasema: “Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mikono yake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema, ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo ili Jina langu lipate kuwamo humo, wala sikumchagua mtu yeyote kuwa kiongozi wa watu wangu Israeli. Lakini sasa nimeuchagua Yerusalemu ili Jina langu lipate kuwamo humo, na nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’ “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni mwili wako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’ “BWANA ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile BWANA alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Nimeliweka humo Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuna lile Agano la BWANA alilofanya na watu wa Israeli.” Kisha Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA machoni pa kusanyiko lote la Israeli, naye akanyoosha mikono yake. Basi Sulemani alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano na kimo chake dhiraa tatu, naye akaliweka katikati ya ukumbi wa nje. Akapanda juu ya hilo jukwaa kisha akapiga magoti mbele ya kusanyiko lote la Israeli, akanyoosha mikono yake kwelekea mbinguni. Akasema: “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote. Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo. “Sasa BWANA, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiwa waangalifu katika yote wanayoyafanya na kuenenda mbele zangu kwa kuzingatia sheria zangu kama ulivyofanya.’ Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie. “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani na wanadamu? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! Hata hivyo sikiliza dua la mtumishi wako na maombi yake ya kuhurumiwa, Ee BWANA Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambalo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia ukiwa mbinguni, makao yako, na unaposikia, samehe.