Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 26:1-15

2 Mambo ya Nyakati 26:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia mwanawe Amazia akiwa mwenye umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake. Halafu baada ya kifo cha baba yake aliujenga upya mji wa Elothi na kuurudisha kwa Yuda. Uzia alianza kutawala akiwa na umri wa miaka kumi na sita; akatawala kwa muda wa miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Yekolia wa Yerusalemu. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake. Alimtumikia Mwenyezi-Mungu kwa uaminifu wakati wa kuishi kwa Zekaria, aliyemfundisha kumtii Mungu. Kadiri alivyomtafuta Mungu, Mungu alimfanikisha. Uzia aliondoka akapiga vita dhidi ya Wafilisti, akazibomoa kuta za miji ya Gathi, Yabne na Ashdodi. Akajenga miji katika eneo la Ashdodi na kwingineko nchini Filistia. Mungu alimsaidia kuwashinda Wafilisti, Waarabu waliokaa Gurbaali na Wameuni. Waamoni walimlipa kodi, na sifa zake zikaenea hadi Misri, kwa sababu alipata nguvu. Tena Uzia alijenga minara katika Yerusalemu penye Lango la Pembeni, Lango la Bondeni na Pembeni na kuiimarisha. Hata nyikani pia alijenga minara, akachimba mabwawa mengi, maana alikuwa na mifugo mingi kwenye sehemu za miinuko na tambarare. Alikuwa na wakulima wa watunza mizabibu milimani, na katika ardhi yenye rutuba kwani alipenda kilimo. Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililojiandaa tayari kwa vita. Lilikuwa limegawanywa katika vikosi mbalimbali, na orodha yao iliwekwa na katibu Yeieli, na Maaseya, ofisa, nao wote walikuwa chini ya uongozi wa Hanania, mmoja wa makamanda wake mfalme. Jumla, viongozi wote wa majeshi walikuwa 2,600. Chini yao, kulikuwa na jeshi la askari 307,500, wenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na adui yeyote wa mfalme. Uzia aliwapa askari hao ngao, mikuki, kofia za chuma, deraya, pinde na mawe kwa ajili ya kupiga kwa kombeo. Huko Yerusalemu mafundi wake walimtengenezea mitambo ya kurushia mishale na mawe makubwamakubwa. Sifa zake zilienea kila mahali, nguvu zake zikaongezeka zaidi kwa sababu ya msaada mwingi alioupata kutoka kwa Mungu.

2 Mambo ya Nyakati 26:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, naye alikuwa mwenye miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa Amazia babaye. Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze. Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Amazia babaye. Akajitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta BWANA, Mungu alimfanikisha. Akatoka akapigana na Wafilisti, akauvunja ukuta wa Gathi, na ukuta wa Yabne, na ukuta wa Ashdodi; akajenga miji katika Ashdodi na katikati ya Wafilisti. Mungu akamsaidia juu ya Wafilisti, na juu ya Waarabu waliokaa Gur-baali, na juu ya Wameuni. Na Waamoni wakampa Uzia zawadi; likaenea jina lake mpaka Misri; alipata nguvu nyingi. Tena Uzia akaujengea Yerusalemu minara, penye Lango la Pembeni, na penye Lango la Bondeni, na ugeukapo ukuta, akaitia nguvu. Akajenga minara tena nyikani, akachimba mabwawa mengi, maana alikuwa na ng'ombe tele; katika Shefela pia, na katika nchi tambarare; tena alikuwa na wakulima na watunza mizabibu milimani, na katika mashamba ya neema; maana yeye alipenda ukulima. Zaidi ya hayo Uzia alikuwa na jeshi la watu wa kupigana, waliokwenda vitani vikosi vikosi, kulingana na hesabu walivyohesabu na Yeieli mwandishi, na Maaseya msimamizi, chini ya mkono wa Hanania, mmojawapo wa makamanda wa mfalme. Hesabu yote ya wakuu wa nyumba za mababa, watu mashujaa, ilikuwa elfu mbili na mia sita. Na chini ya mkono wao kulikuwa na jeshi la askari, elfu mia tatu na saba, na mia tano, ambao walipigana vita kwa nguvu nyingi, kumsaidia mfalme juu ya adui. Uzia akawapatia jeshi lote ngao na mikuki, na chapeo, na deraya za madini, na nyuta, na mawe ya kupiga kwa teo. Huko Yerusalemu akatengeneza mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu mastadi, iwekwe juu ya minara na juu ya buruji, ili kurusha mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.

2 Mambo ya Nyakati 26:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, naye alikuwa mwenye miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa Amazia babaye. Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze. Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Amazia babaye. Akajitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta BWANA, Mungu alimfanikisha. Akatoka akapigana na Wafilisti, akauvunja ukuta wa Gathi, na ukuta wa Yabne, na ukuta wa Ashdodi; akajenga miji katika Ashdodi na katikati ya Wafilisti. Mungu akamsaidia juu ya Wafilisti, na juu ya Waarabu waliokaa Gur-baali, na juu ya Wameuni. Na Waamoni wakampa Uzia zawadi; likaenea jina lake mpaka pa kuingilia Misri; kwa kuwa akaongezeka nguvu mno. Tena Uzia akaujengea Yerusalemu minara, penye lango la pembeni, na penye lango la bonde, na ugeukapo ukuta, akaitia nguvu. Akajenga minara tena nyikani, akachimba mabirika mengi, maana alikuwa na ng’ombe tele; katika Shefela pia, na katika nchi tambarare; tena alikuwa na wakulima na watunza mizabibu milimani, na katika mashamba ya neema; maana yeye alipenda ukulima. Zaidi ya hayo Uzia alikuwa na jeshi la watu wa kupigana, waliokwenda vitani vikosi vikosi, sawasawa na hesabu walivyohesabiwa na Yeieli mwandishi, na Maaseya msimamizi, chini ya mkono wa Hanania, mmojawapo wa maakida wa mfalme. Hesabu yote ya wakuu wa nyumba za mababa, watu mashujaa, ilikuwa elfu mbili na mia sita. Na chini ya mkono wao kulikuwa na jeshi la askari, mia tatu na saba elfu, na mia tano, ambao walipigana vita kwa nguvu nyingi, kumsaidia mfalme juu ya adui. Uzia akawafanyizia jeshi lote ngao na mikuki, na chapeo, na deraya za madini, na nyuta, na mawe ya kupiga kwa teo. Akafanya katika Yerusalemu mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu wastadi, iwekwe juu ya minara na juu ya buruji, ili kutupa mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.

2 Mambo ya Nyakati 26:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake. Ndiye aliijenga upya Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala na baba zake. Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na mbili. Mama yake aliitwa Yekolia, kutoka Yerusalemu. Akatenda yaliyo mema machoni pa BWANA, vile Amazia baba yake alivyofanya. Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta BWANA, Mungu alimfanikisha. Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi, na mahali pengine katikati ya Wafilisti. Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni. Waamoni wakamletea Uzia ushuru, na umaarufu wake ukaenea hadi mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa na nguvu sana. Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome. Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilima na katika nchi tambarare. Alikuwa na watu waliofanya kazi katika mashamba yake, na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo. Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmoja wa maafisa wa mfalme. Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza wapiganaji walikuwa elfu mbili na mia sita. Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu na saba na mia tano waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake. Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, dirii, pinde na mawe ya kombeo. Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno hadi akawa na nguvu sana.