Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 24:1-16

2 Mambo ya Nyakati 24:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia kutoka Beer-sheba. Wakati wote kuhani Yehoyada alipokuwa hai Yoashi alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu. Yehoyada akamwoza wake wawili, nao wakamzalia watoto wa kiume na wa kike. Baadaye Yoashi aliamua kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Basi, akawaita makuhani na Walawi na kuwaamuru, “Nendeni katika miji ya Yuda, mkusanye fedha kutoka kwa Waisraeli wote ili kurekebisha nyumba ya Mungu wenu kila mwaka; harakisheni.” Lakini Walawi hawakuharakisha. Basi, mfalme akamwita kiongozi Yehoyada, akamwuliza, “Mbona hujaamrisha Walawi kukusanya kutoka kwa watu wa Yuda na Yerusalemu, kodi ambayo Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliagiza watu walipe kwa ajili ya Hema Takatifu la Mwenyezi-Mungu?” (Athalia yule mwanamke mwovu na wafuasi wake walivunja nyumba ya Mungu na kuingia ndani; na vyombo vitakatifu vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu walivitumia katika ibada za Mabaali.) Basi, mfalme aliwaamuru Walawi, wakatengeneza sanduku la matoleo na kuliweka nje ya lango la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha tangazo likatolewa kote katika Yuda na Yerusalemu, kwamba watu wote wamletee Mwenyezi-Mungu kodi ambayo Mose mtumishi wa Mungu, aliwaamuru Waisraeli walipokuwa jangwani. Wakuu wote na watu wote walifurahi wakaleta kodi yao wakaitumbukiza kwenye sanduku mpaka walipomaliza kufanya hivyo. Walawi walipopeleka sanduku hilo kwa maofisa wa mfalme, nao walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani, katibu wa mfalme pamoja na mwakilishi wa kuhani mkuu, walizitoa sandukuni, kisha wakalirudisha mahali pake. Waliendelea kufanya hivyo kila siku, wakakusanya fedha nyingi. Mfalme na Yehoyada walizitoa fedha hizo na kuwapa wale waliosimamia kazi ya urekebishaji wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao wakawaajiri waashi, maseremala warekebishe nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Waliajiri pia mafundi wa chuma na shaba ili kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hivyo mafundi hao walishughulika na kazi hiyo kwa bidii, wakairudisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika hali yake ya awali, wakaiimarisha. Walipomaliza kuitengeneza nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walimletea mfalme na Yehoyada dhahabu na fedha iliyobaki; halafu vyombo kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu vilitengenezwa kwa fedha hizo, vyombo hivyo vilikuwa vya kutumika katika huduma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, matoleo ya sadaka za kuteketeza na mabakuli ya kufukizia ubani, pia vyombo vya dhahabu na vya fedha. Watu waliendelea kutoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakati wote wa utawala wa Yehoyada. Lakini Yehoyada alizeeka na alipofikisha umri wa miaka 130, alifariki. Wakamzika katika mji wa Daudi, kwenye makaburi ya wafalme ili kuonesha heshima yao kwake kwa sababu alifanya mema katika Israeli kwa ajili ya Mungu na nyumba yake.

2 Mambo ya Nyakati 24:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala; akatawala miaka arubaini huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Sibia wa Beer-sheba. Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA siku zote za Yehoyada kuhani. Yehoyada akamwoza wake wawili, naye akazaa watoto wa kiume na wa kike. Ikawa baada ya haya, Yoashi alikuwa na nia ya kuitengeneza nyumba ya Mungu. Akawakusanya makuhani na Walawi, akawaambia, Nendeni katika miji ya Yuda, mkakusanye fedha kutoka Israeli wote, ili kuitengeneza nyumba ya Mungu wenu mwaka kwa mwaka, mkafanye bidii kuliharakisha neno hili. Lakini Walawi hawakuliharakisha. Mfalme akamwita Yehoyada mkuu wao, akamwambia, Mbona hukuwataka Walawi waitoze Yuda na Yerusalemu kodi ya Musa mtumishi wa BWANA, na ya kusanyiko la Israeli, kwa ajili ya hema ya ushuhuda? Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya BWANA wamewapatia Mabaali. Basi mfalme akaamuru, nao wakatengeneza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya BWANA. Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea BWANA kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani. Wakafurahi wakuu wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hadi wakaisha. Ikawa wakati walipoletewa kasha wasimamizi wa mfalme kwa mkono wa Walawi, nao wakaona ya kwamba kuna fedha nyingi, huja karani wa mfalme, na msimamizi wake kuhani mkuu, wakatoa yaliyomo kashani, kisha hulichukua kasha, na kulirudisha mahali pake. Ndivyo walivyofanya siku kwa siku, wakakusanya fedha tele. Na mfalme na Yehoyada waliwapa hao waliofanya kazi ya utumishi wa nyumba ya BWANA; nao wakawaajiri waashi na maseremala ili kuitengeza nyumba ya BWANA, na hao pia wafuao chuma na shaba ili kuitengeza nyumba ya BWANA. Hivyo mafundi wakafanya kazi yao, nao wakaimaliza, wakaisimamisha nyumba ya Mungu kama ilivyopasa, wakaifanya imara. Nao walipomaliza, wakaleta mbele ya mfalme na Yehoyada fedha iliyobaki, na kwavyo vikafanywa vyombo vya nyumba ya BWANA, vyombo vya utumishi, navyo vya kutolea, na miiko, na vyombo vya dhahabu na fedha. Wakatoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya BWANA, mara kwa mara, siku zote za Yehoyada. Lakini Yehoyada akawa mzee, mwenye siku nyingi, akafa; alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia moja na thelathini. Wakamzika katika mji wa Daudi kati ya wafalme, kwa sababu ametenda mema katika Israeli, na kwa Mungu, na katika nyumba yake.

2 Mambo ya Nyakati 24:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala; akatawala miaka arobaini huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Sibia wa Beer-sheba. Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA siku zote za Yehoyada kuhani. Yehoyada akamwoza wake wawili, naye akazaa wana na binti. Ikawa baada ya haya, Yoashi alikuwa na nia ya kuitengeneza nyumba ya Mungu. Akawakusanya makuhani na Walawi, akawaambia, Nendeni mijini mwa Yuda, mkakusanye katika Israeli wote fedha, ili kuitengeneza nyumba ya Mungu wenu mwaka kwa mwaka, mkafanye bidii kuliharakisha neno hili. Walakini Walawi hawakuliharakisha. Mfalme akamwita Yehoyada mkuu wao, akamwambia, Mbona hukuwataka Walawi waitoze Yuda na Yerusalemu kodi ya Musa mtumishi wa BWANA, na ya kusanyiko la Israeli, kwa ajili ya hema ya ushuhuda? Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya BWANA wamewapatia mabaali. Basi mfalme akaamuru, nao wakafanyiza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya BWANA. Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea BWANA kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani. Wakafurahi maakida wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hata wakaisha. Ikawa wakati walipoletewa kasha wasimamizi wa mfalme kwa mkono wa Walawi, nao wakaona ya kwamba kuna fedha nyingi, huja karani wa mfalme, na msimamizi wake kuhani mkuu, wakatoa yaliyomo kashani, kisha hulichukua kasha, na kulirudisha mahali pake. Ndivyo walivyofanya siku kwa siku, wakakusanya fedha tele. Na mfalme na Yehoyada waliwapa hao waliofanya kazi ya utumishi wa nyumba ya BWANA; nao wakawaajiri waashi na maseremala ili kuitengeza nyumba ya BWANA, na hao pia wafuao chuma na shaba ili kuitengeza nyumba ya BWANA. Hivyo mafundi wakafanya kazi yao, nao wakaimaliza, wakaisimamisha nyumba ya Mungu kama ilivyopasa, wakaifanya imara. Nao walipokwisha, wakaleta mbele ya mfalme na Yehoyada fedha iliyobaki, vikafanyizwa kwayo vyombo vya nyumba ya BWANA, vyombo vya utumishi, navyo vya kutolea, na miiko, na vyombo vya dhahabu na fedha. Wakatoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya BWANA, daima, siku zote za Yehoyada. Lakini Yehoyada akawa mzee, mwenye umri mwingi, akafa; alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia na thelathini. Wakamzika katika mji wa Daudi kati ya wafalme, kwa sababu ametenda mema katika Israeli, na kwa Mungu, na katika nyumba yake.

2 Mambo ya Nyakati 24:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba. Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA miaka yote ya Yehoyada kuhani. Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike. Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la BWANA. Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi. Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Musa mtumishi wa BWANA pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema la Ushuhuda?” Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa BWANA kwa mabaali. Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la BWANA. Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu, kwamba inapasa wamletee BWANA kodi ambayo Musa, mtumishi wa BWANA, alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani. Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha hadi likajaa. Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana. Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la BWANA. Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la BWANA, pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la BWANA. Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la BWANA likarudi katika hali yake ya awali, na wakaliimarisha. Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la BWANA: Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada akiwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la BWANA. Basi Yehoyada alikuwa mzee aliyeshiba siku alipofariki. Alikufa akiwa na umri wa miaka mia moja na thelathini. Wakamzika pamoja na wafalme katika Mji wa Daudi, kwa sababu ya mema aliyokuwa ametenda katika Israeli kwa ajili ya Mungu na Hekalu lake.