2 Mambo ya Nyakati 22:1-12
2 Mambo ya Nyakati 22:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakazi wa Yerusalemu walimpa Ahazia, mwana mdogo wa Yehoramu, ufalme, atawale mahali pa baba yake kwa sababu wakubwa wake wote waliuawa na kikundi fulani kilichokuja kambini pamoja na Waarabu. Hivyo, Ahazia mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, akatawala. Ahazia, alianza kutawala akiwa mwenye umri wa miaka arubaini na miwili, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri. Kwa sababu mama yake alikuwa mshauri wake katika kutenda maovu, naye pia alifuata mienendo ya jamaa ya Ahabu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile jamaa ya Ahabu ilivyofanya kwani hao ndio waliokuwa washauri wake baada ya kifo cha baba yake, hata aangamie. Hata alifuata shauri lao, akaenda pamoja na mfalme Yehoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-gileadi. Nao Washamu walimjeruhi Yoramu. Kisha akarudi Yezreeli ili apate kutibiwa majeraha aliyoyapata huko Rama, wakati alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alimtembelea Yoramu mwana wa Ahabu huko Yezreeli kwa sababu alikuwa mgonjwa. Lakini hiyo ilikuwa imepangwa na Mungu kuwa maangamizi yampate Ahazia kwa njia hiyo ya kumtembelea Yoramu. Maana alipofika huko, alitoka pamoja na Yoramu kwenda kupigana na Yehu mwana wa Nimshi ambaye Mwenyezi-Mungu alimteua kuuangamiza uzao wa Ahabu. Wakati Yehu alipokuwa akiwahukumu jamaa ya Ahabu alikutana na wakuu wa Yuda pamoja na wana wa ndugu zake Ahazia, waliomtumikia Ahazia, akawaua. Alimtafuta Ahazia, naye akakamatwa akiwa amejificha huko Samaria. Walimleta hadi kwa Yehu, akauawa. Waliuzika mwili wake kwani walisema, “Yeye ni mjukuu wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta Mwenyezi-Mungu kwa moyo wake wote.” Hapakubaki hata mtu mmoja wa jamaa ya Ahazia ambaye angeweza kuwa falme. Mara Athalia, mamake Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka akaangamiza jamii yote ya kifalme ya Yuda. Lakini Yehosheba, binti ya mfalme Yehoramu alimchukua Yoashi, akamtwaa kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha yeye pamoja na yaya wake, katika chumba cha kulala. Hivyo Yehosheba, binti ya mfalme Yehoramu, mke wa kuhani Yehoadani, kwa sababu alikuwa dadaye Ahazia, alimficha Yoashi ili Athalia asimuue. Naye alikaa nao kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mungu wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi.
2 Mambo ya Nyakati 22:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nao wakazi wa Yerusalemu walimfanya Ahazia mwanawe mdogo awe mfalme mahali pake; maana wakubwa wake wote wamekwisha kuuawa na kikosi cha watu waliokuja kambini pamoja na Waarabu. Hivyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akatawala. Ahazia alikuwa na umri wa miaka arubaini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri. Yeye naye akazifuata njia za nyumba ya Ahabu; kwa kuwa mamaye alikuwa mshauri wake katika kufanya maovu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kama nyumba ya Ahabu; kwa kuwa hao walikuwa washauri wake, baada ya kifo cha baba yake, hata aangamie. Naye akaenda kwa mashauri yao, akafuatana na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli ili kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-gileadi; nao Washami wakamjeruhi Yoramu. Akarudi Yezreeli ili aponye majeraha waliyomjeruhi huko Rama, alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akashuka amtazame Yoramu mwana wa Ahabu, katika Yezreeli, kwa sababu alikuwa mgonjwa. Basi kuangamia kwake Ahazia kulitokana na Mungu, kwa vile alivyomwendea Yoramu; kwa kuwa alipofika, akatoka pamoja na Yoramu juu ya Yehu mwana wa Nimshi, ambaye BWANA alimtia mafuta ili awakatilie mbali nyumba ya Ahabu. Ikawa, Yehu alipokuwa akiwafanyia hukumu nyumba ya Ahabu, aliwakuta wakuu wa Yuda, na wana wa nduguze Ahazia, wakimtumikia Ahazia, akawaua. Akamtafuta Ahazia, wakamkamata, (naye alikuwa amejificha Samaria,) wakamleta kwa Yehu, wakamwua; wakamzika, kwa maana wakasema, Huyu ni mwana wa Yehoshafati, huyo aliyemtafuta BWANA kwa moyo wake wote. Wala nyumba ya Ahazia hawakuwa na uwezo wa kuushika ufalme. Basi Athalia, mama wa Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaangamiza jamaa yote ya kifalme ya nyumba ya Yuda. Ila Yehosheba, binti mfalme, akamtwaa Yoashi, mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa, akamweka yeye na yaya wake katika chumba cha kulala. Basi Yehosheba, binti mfalme Yehoramu, mkewe Yehoyada kuhani, (naye alikuwa dada yake Ahazia,) akamficha ili Athalia, asimwue. Akawako pamoja nao, amefichwa nyumbani mwa Mungu, miaka sita. Na Athalia akaitawala nchi.
2 Mambo ya Nyakati 22:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nao wenyeji wa Yerusalemu walimfanya Ahazia mwanawe mdogo awe mfalme mahali pake; maana wakubwa wote wamekwisha kuuawa na kikosi cha watu waliokuja matuoni pamoja na Waarabu. Hivyo akatawala Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda. Ahazia alikuwa na umri wa miaka arobaini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri. Yeye naye akaziendea njia za nyumba ya Ahabu; kwa kuwa mamaye alikuwa mshauri wake katika kufanya maovu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kama nyumba ya Ahabu; kwa kuwa hao walikuwa washauri wake, alipokwisha kufa babaye, hata aangamie. Naye akaenda kwa mashauri yao, akafuatana na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli ili kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-gileadi; nao Washami wakamjeruhi Yoramu. Akarudi Yezreeli ili aponye jeraha walizomjeruhi huko Rama, alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akashuka amtazame Yoramu mwana wa Ahabu, katika Yezreeli, kwa sababu alikuwa hawezi. Basi kuangamia kwake Ahazia kulitokana na Mungu, kwa vile alivyomwendea Yoramu; kwa kuwa alipofika, akatoka pamoja na Yoramu juu ya Yehu mwana wa Nimshi, ambaye BWANA alimtia mafuta ili awakatilie mbali nyumba ya Ahabu. Ikawa, Yehu alipokuwa akiwafanyia hukumu nyumba ya Ahabu, aliwakuta wakuu wa Yuda, na wana wa nduguze Ahazia, wakimtumikia Ahazia, akawaua. Akamtafuta Ahazia, wakamkamata, (naye alikuwa amejificha Samaria,) wakamleta kwa Yehu, wakamwua; wakamzika, kwa maana wakasema, Huyu ni mwana wa Yehoshafati, huyo aliyemtafuta BWANA kwa moyo wake wote. Wala nyumba ya Ahazia hawakuwa na uwezo wa kuushika ufalme. Basi Athalia, mama wa Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaangamiza wazao wote wa kifalme wa nyumba ya Yuda. Ila Yehosheba, binti mfalme, akamtwaa Yoashi, mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa wana wa mfalme waliouawa, akamweka yeye na yaya wake katika chumba cha kulala. Basi Yehosheba, binti mfalme Yehoramu, mkewe Yehoyada kuhani, (naye alikuwa umbu lake Ahazia,) akaficha usoni pa Athalia, asimwue. Akawako pamoja nao, amefichwa nyumbani mwa Mungu, miaka sita. Na Athalia akaitawala nchi.
2 Mambo ya Nyakati 22:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Watu wa Yerusalemu wakamfanya Ahazia, mdogo wa wote wa wana wa Yerohamu, kuwa mfalme mahali pa baba yake, kwa sababu washambuliaji wa ghafula walioingia kambini pamoja na Waarabu, walikuwa wamewaua wana wakubwa wote wa Yehoramu. Kwa hiyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akaanza kutawala. Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri. Ahazia naye akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, kwa sababu mama yake alimshawishi kutenda uovu. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA kama walivyokuwa wamefanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa baada ya kufa kwa baba yake, nyumba ya Ahabu ndio walikuwa washauri wake, kwa uangamivu wake. Pia akafuata ushauri wao alipoenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu. Hivyo akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu. Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa. Mungu alisababisha anguko la Ahazia kutokana na Ahazia kwenda kumwona Yoramu. Ahazia alipowasili, wakatoka pamoja na Yoramu ili kwenda kukutana na Yehu mwana wa Nimshi, ambaye BWANA alikuwa amempaka mafuta kuangamiza nyumba ya Ahabu. Yehu alipokuwa anatekeleza hukumu juu ya nyumba ya Ahabu, akawakuta wakuu wa Yuda na wana wa jamaa ya Ahazia waliokuwa wanamhudumia Ahazia, naye akawaua. Ndipo akaenda kumsaka Ahazia, nao watu wake wakamkamata alipokuwa amejificha huko Samaria. Akaletwa kwa Yehu, naye Yehu akamuua. Wakamzika, kwani walisema, “Alikuwa mwana wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta BWANA kwa moyo wake wote.” Hivyo hapakuwa na mtu mwenye uwezo katika nyumba ya Ahazia aliyeweza kushika ufalme. Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuangamiza jamaa yote ya mfalme ya nyumba ya Yuda. Lakini Yehosheba, binti Mfalme Yehoramu, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala. Kwa kuwa Yehosheba, aliyekuwa binti Mfalme Yehoramu, na pia alikuwa mke wa kuhani Yehoyada, alikuwa dada yake Ahazia, akamficha huyo mtoto ili Athalia asimuue. Alibaki amefichwa pamoja nao katika Hekalu la Mungu kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.