2 Mambo ya Nyakati 14:9-12
2 Mambo ya Nyakati 14:9-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Zera, Mwethiopia aliishambulia nchi ya Yuda akiwa na jeshi la askari 1,000,000 na magari 300, akasonga mbele hadi Maresha. Asa alitoka akaenda kupigana naye. Pande zote mbili zilijipanga katika bonde la Sefatha karibu na Maresha. Hapo Asa akamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, hakuna mwingine kama wewe, mwenye uwezo wa kulisaidia jeshi liwe dhaifu au lenye nguvu. Tusaidie, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa kuwa sisi tunakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja kupigana na jeshi hili kubwa ajabu. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe Mungu wetu; usimruhusu binadamu yeyote ashindane nawe.” Basi, Mwenyezi-Mungu aliwashinda Waethiopia mbele ya Asa na jeshi lake la watu wa Yuda. Waethiopia wakakimbia.
2 Mambo ya Nyakati 14:9-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha, Zera Mkushi alikuja kuwashambulia akiwa na jeshi la watu milioni moja na magari mia tatu akaja Maresha. Asa akatoka kukutana naye, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha. Naye Asa akamlilia BWANA, Mungu wake, akasema, BWANA, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee BWANA, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu. Basi, BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia.
2 Mambo ya Nyakati 14:9-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha, akatoka juu yao Zera Mkushi, mwenye jeshi elfu elfu, na magari mia tatu; akaja Maresha. Akatoka Asa amlaki, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha. Naye Asa akamlilia BWANA, Mungu wake, akasema, BWANA, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee BWANA, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu. Basi, BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia.
2 Mambo ya Nyakati 14:9-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Zera Mkushi akatoka kupigana dhidi yao akiwa na jeshi la watu maelfu ya maelfu na magari ya vita mia tatu, nao wakaja Maresha. Asa akatoka kumkabili, nao wakapanga vita katika Bonde la Sefatha karibu na Maresha. Kisha Asa akamlilia BWANA Mungu wake na kusema, “Ee BWANA, hakuna yeyote aliye kama wewe wa kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, kwa kuwa tunakutumainia wewe, nasi kwa jina lako tumekuja dhidi ya jeshi hili kubwa. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, usiwaache wanadamu wakushinde wewe.” BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa na Yuda. Wakushi wakakimbia