2 Mambo ya Nyakati 14:1-8
2 Mambo ya Nyakati 14:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na Asa mwanawe akatawala mahali pake. Wakati wa Asa, kulikuwa na amani nchini kwa muda wa miaka kumi. Asa alitenda yaliyokuwa mazuri na mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Aliondoa nchini madhabahu za kigeni na mahali pa kuabudia miungu mingine, akabomoa minara na kuzikatakata sanamu za Ashera. Aliwaamuru watu wa Yuda wamtafute Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, na kuzitii sheria na amri. Pia aliondoa mahali pote pa kuabudia miungu mingine na meza za kufukizia ubani kutoka katika miji yote ya Yuda; halafu ufalme wake ulikuwa na amani chini ya utawala wake. Alijenga miji yenye ngome katika Yuda wakati huo wa amani, na kwa muda wa miaka kadhaa, hapakutokea vita kwa maana Mwenyezi-Mungu alimpa amani. Naye akawaambia watu wa Yuda, “Na tuiimarishe miji kwa kuizungushia kuta na minara na malango yenye makomeo. Nchi bado imo mikononi mwetu kwa maana tumeyatenda mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, naye ametupa amani pande zote.” Basi wakajenga, wakafanikiwa. Mfalme Asa alikuwa na jeshi la askari 300,000 kutoka Yuda, wenye ngao na mikuki, na wengine 280,000 kutoka Benyamini, wenye ngao na pinde. Wote walikuwa watu mashujaa sana.
2 Mambo ya Nyakati 14:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi. Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake; maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakatakata maashera; akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu BWANA alimpa amani. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ingali ipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta BWANA, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa. Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda elfu mia tatu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, elfu mia mbili na themanini; hao wote walikuwa mashujaa.
2 Mambo ya Nyakati 14:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi. Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake; maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera; akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu BWANA amemstarehesha. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta BWANA, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa. Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda mia tatu elfu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, mia mbili na themanini elfu; hao wote walikuwa mashujaa.
2 Mambo ya Nyakati 14:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Naye Abiya akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika siku zake, nchi ikawa na amani kwa miaka kumi. Asa akatenda yaliyo mema na haki machoni pa BWANA Mungu wake. Akaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu pa kuabudia, akayavunja yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Maashera. Akawaamuru Yuda kumtafuta BWANA, Mungu wa baba zao, na kutii sheria zake na amri zake. Akaondoa mahali pa juu pa kuabudia na madhabahu za kufukizia uvumba kwenye kila mji katika Yuda, nao ufalme ulikuwa na amani katika utawala wake. Akajenga miji yenye ngome katika Yuda, wakati nchi ikiwa na amani. Hakuna mtu yeyote aliyepigana vita naye katika miaka hiyo, kwa kuwa BWANA alimpa amani. Mfalme akawaambia Yuda, “Tuijenge hii miji na tuizungushie kuta, pamoja na minara, malango na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tumemtafuta BWANA Mungu wetu, tulimtafuta naye ametupatia amani kila upande.” Hivyo wakajenga na wakafanikiwa. Asa alikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu kutoka Yuda, wenye ngao kubwa na mikuki, na jeshi la watu elfu mia mbili na themanini kutoka Benyamini, wenye ngao ndogo na pinde. Watu hawa wote walikuwa wapiganaji hodari.