Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 14:1-15

2 Mambo ya Nyakati 14:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na Asa mwanawe akatawala mahali pake. Wakati wa Asa, kulikuwa na amani nchini kwa muda wa miaka kumi. Asa alitenda yaliyokuwa mazuri na mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Aliondoa nchini madhabahu za kigeni na mahali pa kuabudia miungu mingine, akabomoa minara na kuzikatakata sanamu za Ashera. Aliwaamuru watu wa Yuda wamtafute Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, na kuzitii sheria na amri. Pia aliondoa mahali pote pa kuabudia miungu mingine na meza za kufukizia ubani kutoka katika miji yote ya Yuda; halafu ufalme wake ulikuwa na amani chini ya utawala wake. Alijenga miji yenye ngome katika Yuda wakati huo wa amani, na kwa muda wa miaka kadhaa, hapakutokea vita kwa maana Mwenyezi-Mungu alimpa amani. Naye akawaambia watu wa Yuda, “Na tuiimarishe miji kwa kuizungushia kuta na minara na malango yenye makomeo. Nchi bado imo mikononi mwetu kwa maana tumeyatenda mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, naye ametupa amani pande zote.” Basi wakajenga, wakafanikiwa. Mfalme Asa alikuwa na jeshi la askari 300,000 kutoka Yuda, wenye ngao na mikuki, na wengine 280,000 kutoka Benyamini, wenye ngao na pinde. Wote walikuwa watu mashujaa sana. Zera, Mwethiopia aliishambulia nchi ya Yuda akiwa na jeshi la askari 1,000,000 na magari 300, akasonga mbele hadi Maresha. Asa alitoka akaenda kupigana naye. Pande zote mbili zilijipanga katika bonde la Sefatha karibu na Maresha. Hapo Asa akamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, hakuna mwingine kama wewe, mwenye uwezo wa kulisaidia jeshi liwe dhaifu au lenye nguvu. Tusaidie, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa kuwa sisi tunakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja kupigana na jeshi hili kubwa ajabu. Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe Mungu wetu; usimruhusu binadamu yeyote ashindane nawe.” Basi, Mwenyezi-Mungu aliwashinda Waethiopia mbele ya Asa na jeshi lake la watu wa Yuda. Waethiopia wakakimbia. Asa pamoja na wanajeshi wake wakawafuatilia mpaka Gerari, wakawaua Waethiopia wengi sana, asibaki hata mmoja, kwani walikuwa wamekwisha shindwa na Mwenyezi-Mungu pamoja na jeshi lake. Jeshi la Yuda lilichukua nyara nyingi sana. Liliharibu miji yote iliyokuwa kandokando ya Gerari, kwa kuwa watu waliokuwamo katika miji hiyo waliingiwa na hofu ya Mwenyezi-Mungu. Jeshi lilichukua mali nyingi kutoka katika miji hiyo kwa sababu kulikuwamo mali nyingi sana. Lilishambulia pia wachungaji, likachukua kondoo wengi na ngamia. Kisha likarejea Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 14:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi. Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake; maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakatakata maashera; akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu BWANA alimpa amani. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ingali ipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta BWANA, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa. Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda elfu mia tatu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, elfu mia mbili na themanini; hao wote walikuwa mashujaa. Kisha, Zera Mkushi alikuja kuwashambulia akiwa na jeshi la watu milioni moja na magari mia tatu akaja Maresha. Asa akatoka kukutana naye, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha. Naye Asa akamlilia BWANA, Mungu wake, akasema, BWANA, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee BWANA, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu. Basi, BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia. Asa na watu waliokuwa pamoja naye wakawafuata mpaka Gerari; wakawaua Wakushi wengi sana asipone hata mmoja; kwa sababu waliangamizwa mbele za BWANA, na mbele ya jeshi lake; na hao wakachukua mateka wengi sana. Wakaipiga miji yote kandokando ya Gerari; maana hofu ya BWANA ikawajia; nao wakaiteka nyara miji yote, kwa maana zilikuwamo ndani yake nyara nyingi mno. Wakazipiga pia hema za ng'ombe, wakachukua kondoo wengi na ngamia, wakarudi Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 14:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi. Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake; maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera; akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake. Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu BWANA amemstarehesha. Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta BWANA, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa. Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda mia tatu elfu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, mia mbili na themanini elfu; hao wote walikuwa mashujaa. Kisha, akatoka juu yao Zera Mkushi, mwenye jeshi elfu elfu, na magari mia tatu; akaja Maresha. Akatoka Asa amlaki, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha. Naye Asa akamlilia BWANA, Mungu wake, akasema, BWANA, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee BWANA, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu. Basi, BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia. Asa na watu waliokuwa pamoja naye wakawafuata mpaka Gerari; nao wengi wakaanguka wa Wakushi hata wasiweze kupona; kwa sababu waliangamizwa mbele za BWANA, na mbele ya jeshi lake; na hao wakachukua mateka mengi sana. Wakaipiga miji yote kando-kando ya Gerari; maana hofu ya BWANA ikawajia; nao wakaiteka nyara miji yote, kwa maana zilikuwamo ndani yake nyara nyingi mno. Wakazipiga pia hema za ng’ombe, wakachukua kondoo wengi na ngamia, wakarudi Yerusalemu.

2 Mambo ya Nyakati 14:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Naye Abiya akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika siku zake, nchi ikawa na amani kwa miaka kumi. Asa akatenda yaliyo mema na haki machoni pa BWANA Mungu wake. Akaziondoa madhabahu za kigeni na mahali pa juu pa kuabudia, akayavunja yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Maashera. Akawaamuru Yuda kumtafuta BWANA, Mungu wa baba zao, na kutii sheria zake na amri zake. Akaondoa mahali pa juu pa kuabudia na madhabahu za kufukizia uvumba kwenye kila mji katika Yuda, nao ufalme ulikuwa na amani katika utawala wake. Akajenga miji yenye ngome katika Yuda, wakati nchi ikiwa na amani. Hakuna mtu yeyote aliyepigana vita naye katika miaka hiyo, kwa kuwa BWANA alimpa amani. Mfalme akawaambia Yuda, “Tuijenge hii miji na tuizungushie kuta, pamoja na minara, malango na makomeo. Nchi bado ni yetu, kwa sababu tumemtafuta BWANA Mungu wetu, tulimtafuta naye ametupatia amani kila upande.” Hivyo wakajenga na wakafanikiwa. Asa alikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu kutoka Yuda, wenye ngao kubwa na mikuki, na jeshi la watu elfu mia mbili na themanini kutoka Benyamini, wenye ngao ndogo na pinde. Watu hawa wote walikuwa wapiganaji hodari. Zera Mkushi akatoka kupigana dhidi yao akiwa na jeshi la watu maelfu ya maelfu na magari ya vita mia tatu, nao wakaja Maresha. Asa akatoka kumkabili, nao wakapanga vita katika Bonde la Sefatha karibu na Maresha. Kisha Asa akamlilia BWANA Mungu wake na kusema, “Ee BWANA, hakuna yeyote aliye kama wewe wa kuwasaidia wasio na nguvu dhidi ya wenye nguvu. Utusaidie, Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, kwa kuwa tunakutumainia wewe, nasi kwa jina lako tumekuja dhidi ya jeshi hili kubwa. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, usiwaache wanadamu wakushinde wewe.” BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa na Yuda. Wakushi wakakimbia, naye Asa na jeshi lake wakawafuatia hadi Gerari. Idadi kubwa ya Wakushi ilianguka hata wasiweze kuinuka tena, wakapondapondwa mbele za BWANA na majeshi yake. Watu wa Yuda wakachukua nyara nyingi sana; wakaangamiza vijiji vyote vya Gerari, kwa kuwa kicho cha BWANA kilikuwa kimewaangukia. Wakateka nyara vijiji hivi vyote, kwani kulikuwa na nyara nyingi huko. Pia wakashambulia kambi za wachunga makundi ya wanyama wakachukua na kuyaswaga makundi ya kondoo, mbuzi na ngamia. Kisha wakarudi Yerusalemu.