2 Mambo ya Nyakati 10:1-19
2 Mambo ya Nyakati 10:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu, ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme. Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (wakati huo alikuwa bado anaishi Misri alikokwenda alipomkimbia Solomoni) alitoka Misri. Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na Waisraeli wote walimwendea Rehoboamu na kumwambia, “Baba yako alitutwika mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.” Rehoboamu akawajibu, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” Basi wakaondoka. Baadaye, Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa Solomoni, baba yake, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?” Wazee hao wakamjibu, “Ukiwahurumia watu hawa, ukiwafurahisha na kusema nao maneno mazuri, hapo watakuwa watumishi wako daima.” Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee na badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake. Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia, ‘Punguza mzigo ambao baba yako alitutwika?’” Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia ‘Baba yako alitutwika mzigo mzito, lakini wewe utupunguzie,’ wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo cha mwisho ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu. Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’” Basi katika siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza. Naye mfalme Rehoboamu akawajibu kwa ukali, akapuuza shauri la wazee, na kufuata shauri la vijana wenzake. Basi akasema, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba” Hivyo mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mungu ili Mwenyezi-Mungu atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu, mwana wa Nebati kwa njia ya Ahiya wa Shilo. Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali walimwambia, “Tuna sehemu gani kwa Daudi? Hatuna urithi katika mwana wa Yese. Kila mmoja na arudi nyumbani kwake, enyi watu wa Israeli. Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.” Hivyo watu wote wa Israeli wakarudi makwao. Lakini Rehoboamu alitawala watu wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda. Kisha mfalme Rehoboamu alipomtuma Hadoramu aliyekuwa mnyapara mkuu wa kazi za kulazimishwa, watu wa Israeli walimpiga mawe, wakamuua. Ndipo Rehoboamu alipopanda gari lake haraka akakimbilia Yerusalemu. Hivyo, watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya maasi dhidi ya utawala wa ukoo wa Daudi mpaka leo.
2 Mambo ya Nyakati 10:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme. Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia tendo hilo (maana alikuwa Misri, alikokwenda alipomkimbia mfalme Sulemani) Yeroboamu akarudi kutoka Misri. Wakatuma ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao. Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mnanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa? Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, hapo watakuwa watumishi wako siku zote. Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana wa rika yake, waliokuwa washauri wake. Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, kongwa alilotutwika baba yako utufanyie liwe jepesi. Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya kongwa letu kuwa zito, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana, akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. Basi mfalme hakuwasikia watu wale; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni. Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; kila mtu aende zake hemani, enyi Israeli, sasa itunze nyumba yako mwenyewe ewe Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao. Lakini kuhusu wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao. Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakampiga kwa mawe hadi akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu. Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo.
2 Mambo ya Nyakati 10:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme. Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri. Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao. Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa? Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote. Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, waliosimama mbele yake. Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako. Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu akiwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana, akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni. Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli, kila mtu; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao. Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao. Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakamtupia mawe, hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu. Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo.
2 Mambo ya Nyakati 10:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wameenda huko kumfanya mfalme. Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Sulemani), akarudi kutoka Misri. Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu; yeye na Waisraeli wote wakamwendea Rehoboamu na kumwambia, “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.” Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao. Kisha Mfalme Rehoboamu akataka ushauri kwa wazee ambao walimtumikia Sulemani baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri niwajibu nini watu hawa?” Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.” Lakini Rehoboamu akakataa ushauri aliopewa na wazee, na akataka ushauri kwa vijana wa rika lake waliokuwa wakimtumikia. Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu’?” Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Watu hawa walikuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ Wewe waambie, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.’ ” Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Alikataa ushauri aliopewa na wazee, akafuata ushauri wa vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwapiga mijeledi; mimi nitawapiga kwa nge.” Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Mungu ili kutimiza neno ambalo BWANA alikuwa amenena na Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia kwa Ahiya Mshiloni. Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme: “Je, tuna fungu gani kwa Daudi? Tuna urithi gani kwa mwana wa Yese? Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli, angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!” Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao. Lakini kwa habari ya Waisraeli walioishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado. Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoniramu aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu akafanikiwa kuingia kwenye gari lake la vita, akatorokea Yerusalemu. Hivyo, Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.