2 Mambo ya Nyakati 1:1-13
2 Mambo ya Nyakati 1:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Solomoni, mwanawe mfalme Daudi, alijiimarisha katika utawala wake, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wake alikuwa pamoja naye, akambariki na kumfanya awe mkuu sana. Mfalme Solomoni aliwaita makamanda wote wa vikosi vya maelfu na vya mamia, waamuzi, na viongozi wote wa koo za Israeli. Kisha akaandamana nao hadi mahali pa ibada huko Gibeoni. Walikwenda huko kwa sababu hapo ndipo mahali lilipokuwa hema la mkutano la Mungu alilolitengeneza Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, nyikani. (Lakini, sanduku la Mungu lilikuwa Yerusalemu katika hema ambalo mfalme Daudi alilipigilia alipolileta kutoka Kiriath-yearimu). Tena, madhabahu ya shaba iliyotengenezwa na Bezaleli, mwana wa Uri na mjukuu wa Huri, pia ilikuwa huko Gibeoni mbele ya hema takatifu la Mwenyezi-Mungu. Hapo mfalme Solomoni na watu wote wakamwomba Mwenyezi-Mungu. Solomoni alipanda mbele ya madhabahu ya shaba iliyokuwa kwenye hema la mkutano. Hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akatoa tambiko 1,000 za kuteketezwa juu ya madhabahu hayo. Usiku huo, Mungu alimtokea Solomoni, akamwambia, “Omba chochote, nami nitakupa.” Solomoni akamwambia Mungu, “Ulimwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, na umenijalia kuwa mfalme mahali pake. Sasa, ee Mungu, Mwenyezi-Mungu, itimize ahadi uliyompa baba yangu Daudi. Umenitawaza niwe mfalme juu ya watu hawa walio wengi kama mavumbi. Kwa hiyo, nakuomba unipe hekima na maarifa ili niweze kuwatawala watu wako vizuri. La sivyo, nitawezaje kuwatawala hawa watu wako walio wengi hivi?” Mungu akamjibu Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili uliloomba limo moyoni mwako, na wala hukuomba mali, wala utajiri, wala heshima wala hukuomba wanaokuchukia waangamizwe, wala maisha marefu, lakini umeomba hekima na maarifa ili uwatawale vizuri watu wangu ambao nimekupa uwe mfalme wao, ninakupa hekima na maarifa. Pia, nitakupa utajiri, mali na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote aliyekuwako kabla yako na mfalme mwingine yeyote atakayetawala baada yako.” Basi, Solomoni aliondoka mahali hapo pa kuabudia, huko Gibeoni, lilipokuwa hema la mkutano, akarudi Yerusalemu. Akaitawala Israeli.
2 Mambo ya Nyakati 1:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alijiimarisha katika ufalme wake, naye BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno. Sulemani akawaita Israeli wote, na makamanda wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila kiongozi wa Israeli, na wakuu wa familia. Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo lilipokuwako hema la kukutania la Mungu, alilolifanya Musa mtumishi wa BWANA jangwani. Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu. Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanya Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea. Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu yake. Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwatawala watu wako hawa walio wengi? Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha ya wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwatawala watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo. Basi Sulemani akatoka mahali pa juu pa Gibeoni, toka mbele ya Hema la kukutania, akaja mpaka Yerusalemu; akatawala Israeli.
2 Mambo ya Nyakati 1:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alithibitishwa katika ufalme wake, naye BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno. Sulemani akasema na Israeli wote, na maakida wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila shehe wa Israeli wote, wakuu wa nyumba za mababa. Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo ilipokuwako hema ya kukutania ya Mungu, aliyoifanya Musa mtumishi wa BWANA jangwani. Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu. Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanyiza Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea. Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu yake. Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi? Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo. Akaja Sulemani kutoka mahali pa juu pa Gibeoni, toka mbele ya hema ya kukutania, mpaka Yerusalemu; akatawala juu ya Israeli.
2 Mambo ya Nyakati 1:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sulemani mwana wa Daudi alijiimarisha katika ufalme wake, kwa kuwa BWANA Mungu wake alikuwa pamoja naye, naye akamfanya mkuu sana. Ndipo Sulemani akasema na Waisraeli wote, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, waamuzi na viongozi wote katika Israeli, pamoja na wakuu wa jamaa. Naye Sulemani na kusanyiko lote wakakwea hadi mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. Hema la Kukutania la Mungu, ambalo Musa mtumishi wa BWANA alikuwa amelitengeneza huko jangwani, lilikuwa Gibeoni. Basi Daudi alikuwa amelipandisha Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu hadi mahali alipokuwa amepatengeneza kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa amesimamisha hema kwa ajili ya hilo Sanduku huko Yerusalemu. Lakini yale madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, alikuwa ametengeneza yalikuwa huko Gibeoni mbele ya Maskani ya BWANA Mungu, hivyo Sulemani na kusanyiko lote walimtafuta Mungu huko. Sulemani akapanda huko yalikokuwa madhabahu ya shaba mbele za BWANA katika Hema la Kukutania, na kutoa dhabihu elfu moja za sadaka za kuteketezwa juu yake. Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani na kumwambia, “Omba lolote utakalo nikupe.” Sulemani akamjibu Mungu, “Umemwonesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake. Sasa, BWANA Mungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi. Nakuomba unipe hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?” Mungu akamwambia Sulemani, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.” Ndipo Sulemani akaenda Yerusalemu kutoka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kutoka mbele ya Hema la Kukutania. Naye akatawala Israeli.