1 Timotheo 5:1-16
1 Timotheo 5:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Usimkemee mwanamume mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana wa kiume kama ndugu zako, wanawake wazee kama mama zako, na vijana wa kike kama dada zako, kwa usafi wote. Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli. Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu. Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana. Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai. Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama. Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini. Usimtie katika orodha ya wajane mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu, na awe mwenye sifa nzuri: Aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema. Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena, na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali. Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema. Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili maadui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu. Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani. Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa.
1 Timotheo 5:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na wanaume vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku. Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai. Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama. Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini. Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja; na awe ameshuhudiwa kwa matendo mema; katika kulea watoto, kuwa mkaribishaji, kuwaosha watakatifu miguu, kuwasaidia wateswao, na kujitolea kutenda wema katika hali zote. Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizungukazunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, watunze nyumba zao; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu. Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani. Mwanamke aaminiye, akiwa na jamaa walio wajane wa kweli, na awasaidie mwenyewe, kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli.
1 Timotheo 5:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku. Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai. Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama. Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini. Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja; naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema. Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu. Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani. Mwanamke aaminiye, akiwa ana wajane, na awasaidie mwenyewe, Kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli.
1 Timotheo 5:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako; nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote. Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli. Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo inavyompendeza Mungu. Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie. Lakini mjane aishiye kwa anasa amekufa, ingawa anaishi. Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo yeyote wa kulaumiwa. Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini. Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na amekuwa mke wa mume mmoja; awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna. Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena. Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza. Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema. Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani. Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.