1 Timotheo 4:6-12
1 Timotheo 4:6-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli ambayo wewe umeyafuata. Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uhai katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini. Wape maagizo hayo na mafundisho hayo. Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: Katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi.
1 Timotheo 4:6-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoefu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata. Bali hadithi za kale, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Maana, mazoezi ya viungo vya mwili yana manufaa kidogo, lakini utauwa una manufaa ya kila aina; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa; kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa wale waaminio. Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha. Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.
1 Timotheo 4:6-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoevu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata. Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa; kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio. Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha. Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.
1 Timotheo 4:6-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata. Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee; badala yake, jizoeze kuwa mtauwa. Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao. Hili ni neno la kuaminiwa tena lastahili kukubaliwa kabisa. Nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi, kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio. Mambo haya yaagize na kuyafundisha. Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi.