1 Timotheo 4:1-10
1 Timotheo 4:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Roho asema waziwazi kwamba siku za baadaye watu wengine wataitupilia mbali imani; watazitii roho danganyifu na kufuata mafundisho ya pepo. Mafundisho ya namna hiyo yanaenezwa na watu waongo wadanganyifu, ambao dhamiri zao ziko kama zimechomwa kwa chuma cha moto. Watu hao hufundisha kwamba ni makosa kuoa na pia kula vyakula fulani. Lakini Mungu aliviumba vyakula hivyo, ili wale walio waumini na ambao wanapata kuujua ukweli, wavitumie kwa shukrani. Kila kitu alichoumba Mungu ni chema, wala hakuna kinachohitaji kukataliwa, bali vyote vipokelewe kwa sala ya shukrani, kwa sababu neno la Mungu na sala hukifanya kitu hicho kikubalike kwa Mungu. Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli ambayo wewe umeyafuata. Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uhai katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini.
1 Timotheo 4:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine wataikana imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba. Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoefu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata. Bali hadithi za kale, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Maana, mazoezi ya viungo vya mwili yana manufaa kidogo, lakini utauwa una manufaa ya kila aina; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa; kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa wale waaminio.
1 Timotheo 4:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba. Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoevu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata. Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa; kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio.
1 Timotheo 4:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli. Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba. Ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata. Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee; badala yake, jizoeze kuwa mtauwa. Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao. Hili ni neno la kuaminiwa tena lastahili kukubaliwa kabisa. Nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi, kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.